Idadi ya waliofariki kwenye maandamano Kenya yafikia 16

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waandamanaji katikati ya mji wa nairobi siku ya Jumatano tarehe 25 Juni
Muda wa kusoma: Dakika 3

Idadi ya raia waliofariki kutokana na maandamano ya siku ya Jumatano nchini Kenya imefikia watu 16.

Kwa mujibu wa Shirika la haki za kibinadamu Amnesty International wengi wamejuriwa ambapo miongoni mwa waliopoteza maisha, chanzo cha vifo vyao vimetokana na majeraha ya ya risasi.

Mkurugenzi mkuu wa Amnesty International Irungu Houghton anasema kwamba idadi hiyo imethibitishwa na tume ya kitaifa ya haki za kibinadamu nchini Kenya.

Maelfu ya vijana katika maeneo mbalimbali ya Kenya waliandamana kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano mengine ya kupingwa muswada wa fedha yaliyosababisha mauaji ya zaidi ya watu 60.

Maandamano hayo yalifanyika mwaka jana mwezi Juni 25, ambapo mbali na vifo hivyo yalisababisha mamia kujeruhiwa.

Mapema siku ya Jumatano, polisi walifunga barabara kuu zinazoelekea katika mji mkuu wa Nairobi, huku majengo ya serikali yakiwa yamezingirwa na waya wa seng'enge.

Kulingana na jarida la The Citizen Online, maelfu ya waandamanaji, wengi wakiwa vijana, walipeperusha bendera na mabango ya Kenya yenye picha za waandamanaji waliouawa mwaka jana na kuimba "Ruto lazima aondoke".

"Nimekuja hapa kama kijana wa Kenya kuandamana, ni haki yetu kwa ajili ya Wakenya wenzetu waliouawa mwaka jana. Polisi wako hapa... wanastahili kutulinda lakini wanatuua," Eve, mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ambaye hana kazi aliambia AFP.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Ni muhimu sana kwamba vijana waadhimishe Juni 25 kwa sababu walipoteza watu wanaofanana nao, wanaozungumza kama wao... wanaopigania utawala bora," alisema Angel Mbuthia, mwenyekiti wa ligi ya vijana wa chama cha upinzani cha Jubilee.

Huku hayo yakijiri Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen anasema maafisa 300 wa polisi walijeruhiwa Jumatano wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na vijana ambayo yalifanyika maeneo tofauti ya Kenya.

Akihutubia vyombo vya habari kuhusu hali ya usalama kufuatia maandamano hayo, Murkomen alisema shambulio dhidi ya vyombo vya usalama—ambalo lilihusisha uvamizi wa vituo kadhaa vya polisi—ni sehemu ya mpango wa "wapangaji mapinduzi" wa kuyumbisha nchi.

"Kuna maafisa wa polisi 300 waliojeruhiwa na raia takriban 100. Kwa ujumla watu 400 walijeruhiwa," alisema Murkomen.

Aliendelea: "Kutokana na maandamano ya jana, tulishuhudia visa ambapo vituo vya polisi vinalengwa... nahisi, uteketezaji wa vituo vya polisi ulipaswa kuwasaidia waliopanga mapinduzi kutoa kauli kwamba hakuna nchi na kwamba hakuna mamlaka.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, aliunga mkono kauli ya Murkomen na kuwapongeza polisi kwa kile alichokitaja kuwa juhudi za kupongezwa.

"Tunawashukuru maafisa wetu shupavu waliofanya kazi nzuri jana kwa kuhakikisha nchi yetu inasalia salama licha ya changamoto nyingi zilizokuwepo," alisema Kanja.

IG alibainisha kuwa baadhi ya maafisa waliojeruhiwa walipata majeraha ya kutishia maisha na kuwahakikishia msaada wa serikali.

"Nawatakia maofisa hao zaidi ya 300 waliojeruhiwa uponaji wa haraka na kueleza jeshi la polisi litasimama pamoja nao kwani inathamini kazi wanayoifanya," alisema Kanja.

Kwa wahalifu waliojipenyeza kwenye maandamano, Mkuu wa polisi aliwaonya: "Tutawakamata na lazima tuwawajibishe kisheria."

Waliouawa ni akina nani?

David Mwangi mwenye umri wa miaka kumi na tisa, ambaye aliishi katika mtaa usio rasmi wa Mukuru Nairobi, alikuwa mmoja wa waliouawa kwa kupigwa risasi.

Mamake aliiambia BBC kwamba alikuwa mpita njia aliyekuwa ameenda shuleni kumchukua mdogo wake. Rachael Nyambura Mwangi aliyekuwa akibubujikwa na machozi alisema kwamba risasi ilimpata mwanawe kichwani.

"Nina uchungu sana," alisema.

"David alitarajia kwenda chuoni kuwa fundi mitambo. Alikuwa mtoto wangu wa kwanza na alikuwa msaidizi wangu. Nikihitaji kuchota maji au kupata kitu ningempelekea. Nauza viazi vitamu na kila nilipohitaji kupata hisa yangu nilikuwa nampelekea."