Tahadhari, ni nani asiyepaswa kutumia kirutubisho hiki cha kujenga misuli?

Chanzo cha picha, Getty Images
Protini zipo katika mwili wa binadamu; kwenye misuli, mifupa, ngozi, nywele na katika tishu na viungo vyote. Kuna zaidi ya aina 10,000 za protini katika mwili.
Protini hukarabati tishu, kusafirisha vitu kupitia damu na kuzalisha homoni na kinga. Lakini moja ya kazi ya protini ambayo ni maarufu ni kuongeza uzito wa misuli.
Wakati wa mazoezi kama ya kuinua vyuma, majeraha madogo hutokea kwenye nyuzi za misuli. Ili kuzikarabati na kuziimarisha, mwili hutumia asidi ya amino inayotokana na protini, kuongeza ukuaji wa misuli na kukabiliana na hali hiyo.
Bila ulaji wa kutosha wa protini, mchakato wa kuongezea uzito wa misuli haukamiliki. Chanzo kikuu cha protini ni nyama, mayai, vyakula vya jamii ya kunde, kama vile maharagwe, dengu na njugu mawe, kwa uchache.
Unga wa protini

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini tangu miaka ya 1980, unga wa protini umekuwa maarufu katika kuongeza misuli. Ikiwa lengo ni kuongeza uzito wa misuli, mtu anahitajika kula kati ya gramu 1.4 na 2 za protini kwa kilo moja ya uzito, kulingana na pendekezo la Jumuiya ya Kimataifa ya Lishe na Michezo.
Ulaji huo unapaswa kuunganishwa na mazoezi ya mwili yanayolenga kupata misuli, kama vile mazoezi ya kuinua vitu vizito/vyuma. Kwa mtu mwenye uzito wa kilo 70, anatakiwa kula karibu gramu 119 za protini kwa siku.
Mfano, glasi moja ya maji au maziwa yenye unga wa protini, kwa kawaida ina takribani gramu 25 za protini, sawa na nyama ya ng'ombe ya gramu 125, au mayai manne, au minofu ya kuku ya gramu 100.
"Unga wa protini pia unaweza kutumika kwa wagonjwa walio na sarcopenia, ugonjwa ambao unasababisha kupoteza uzito wa misuli na nguvu kwa kasi, kawaida kwa wazee," anasema Daniela Gomes, mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Albert Sabin huko São Paulo, Brazli.
Mchakato wa asili wa kuanza kupoteza uzito wa misuli na nguvu huanza kutokea polepole, kuanzia mtu anapokuwa na umri wa miaka 30.
Baada ya kufikia umri wa miaka 50, mtu huanza kupoteza uzito wa misuli kwa kasi zaidi, inaweza kuwa ni 2% ya upotevu kila mwaka.
Unga wa protini kwa ujumla unapendekezwa kutumiwa baada ya mazoezi, kwani wakati huo ndio husaidia haraka kuponesha misuli na usanisi wa protini.
Kuna aina kadhaa za unga wa protini, na kabla ya kutumia, wataalamu wanashauri upate ushauri wa mtaalamu wa lishe ili kujua aina ya protini unayopaswa kutumia (ikiwa ni muhimu kwako kutumia) na kwa kiwango au kipimo gani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutumia protini nyingi ni hatari?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Mara nyingi husema hata maji mengi yanaweza kuwa na madhara," anasema Veridiana Vera de Rosso, mtaalamu katika taasisi ya afya ya jamii katika chuo kikuu cha Federal University huko São Paulo, Brazil.
"Kwa hiyo, nasisitiza umuhimu wa kuwa na mtaalamu wa afya ambaye anamwelekeza mtu anayehitaji, juu ya aina na kiasi cha kutumia kirutubisho hicho."
Kwa wagonjwa walio na ugonjwa sugu wa figo, ulaji mwingi wa protini unaweza kuzidisha tatizo la figo, na hivyo kuzidisha ukuaji wa ugonjwa.
Kikomo cha salama kinategemea hali ya ugonjwa huo, kwa hiyo ni muhimu zaidi kwa kundi hilo kwanza kufuatilia afya zao na kufuatilia matumizi ya protini yenyewe.
Hata hivyo, kwa watu wenye afya nzuri, protini ambayo haifyonzwi katika mwili kwa kawaida hutolewa, anaelezea Dr. Rosso.
"Kwa ujumla, gramu 30 za protini kwa kila mlo ndicho kikomo ambacho mwili unaweza kufyonza, ingawa hilo linaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu," anasema.
"Ikiwa italiwa nyingi katika mlo mmoja, baadhi ya protini hizi zitaondolewa katika mwili bila ya kutumiwa na mwili," anasema Rossa.
Kuboresha afya ni muhimu, ila kufanya maamuzi salama juu ya afya yako ni muhimu zaidi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












