Wimbi la pili la milipuko ya vifaa vya mawasiliano Lebanon laua 20 na kujeruhi 450

Milipuko iliripotiwa kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na mji wa Sidoni, pamoja na vitongoji vya kusini mwa Beirut na Bonde la Bekaa.

Chanzo cha picha, AFP

Muda wa kusoma: Dakika 5

Takribani watu 20 wameuawa na zaidi ya 450 kujeruhiwa na wimbi la pili la milipuko kutoka kwenye vifaa vya mawasiliano visivyo na waya nchini Lebanon, wizara ya afya ya nchi hiyo inasema.

Simu za upepo zinazotumiwa kwa mawasiliano na kundi lenye silaha la Hezbollah zimelipuka katika viunga vya kusini mwa mji mkuu Beirut, Bonde la Bekaa, na kusini mwa Lebanon, maeneo yanayoonekana kama ngome zake.

Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea wakati wa mazishi ya baadhi ya watu 12 ambao wizara hiyo ilisema waliuawa wakati wafuasi wa Hezbollah walipolipuka siku ya Jumanne. Hezbollah iliilaumu Israel kwa shambulio hilo. Israel haijasema chochote.

Mashambulizi hayo yametokea wakati Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant akitangaza "awamu mpya ya vita" na kuwa kitengo cha jeshi la Israel kilitumwa tena kaskazini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionya kuhusu "hatari kubwa ya kuongezeka kwa kasi" na kutoa wito kwa pande zote "kujizuia".

"Kwa hakika mantiki ya kufanya vifaa hivi vyote kulipuka ni kufanya hivyo kama shambulio la awali kabla ya operesheni kubwa ya kijeshi," aliwaambia waandishi wa habari.

Tayari kulikuwa na hofu ya kuongezeka kwa mzozo wa pande zote baada ya miezi 11 ya mapigano ya kuvuka mpaka yaliyochochewa na vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

Saa chache baada ya milipuko ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwarejesha makumi kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutoka kaskazini mwa nchi "salama kwenye makazi yao".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant wakati huo huo alisema Israel "inafungua awamu mpya katika vita" na kwamba "nguvu za rasilimali zinahamia eneo la kaskazini.

Kikosi cha jeshi kilichokuwa hivi karibuni huko Gaza kimetumwa tena kaskazini, jeshi la Israel limethibitisha.

Hezbollah inasema inaiunga mkono Hamas, ambayo pia inaungwa mkono na Iran na kupigwa marufuku kama shirika la kigaidi na Israel na nchi nyingi za Magharibi na itasimamisha tu mashambulizi yake ya kuvuka mpaka mara tu mapigano ya Gaza yatakapomalizika.

Ofisi ya vyombo vya habari ya Hezbollah siku ya Jumatano ilitangaza kifo cha wapiganaji wake 13, akiwemo mvulana wa miaka 16, tangu kutokea kwa wimbi la pili la milipuko.

Pia ilisema kundi hilo lililenga wanajeshi wa Israel karibu na mpaka na katika eneo la Milima ya Golan linalokaliwa na Israel wakati wa mchana, wakirusha makombora katika maeneo ya mizinga ya Israel.

Jeshi la Israel lilisema takribani makombora 30 yalivuka kutoka Lebanon siku ya Jumatano, na kusababisha moto lakini hakukuwa na majeruhi.

Ilisema ndege za Israel zilishambulia wapiganaji wa Hezbollah kusini mwa Lebanon.

Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea wakati wa mazishi ya watu 12 waliouawa

Chanzo cha picha, Reuters

Milipuko mikubwa ya Jumatano inawakilisha fedheha nyingine kwa Hezbollah na dalili kwamba mtandao wake wote wa mawasiliano unaweza kuwa umepenyezwa na Israel.

Walebanon wengi wameshtushwa na kukasirishwa na kile kilichotokea Jumanne, wakati maelfu ya vifaa vya mawasiliano vilipolipuka kwa wakati mmoja, baada ya watu kupokea ujumbe ambao waliamini kuwa umetoka kwa kundi hilo.

Watu 12 , ikiwa ni pamoja na msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka 11 waliuawa na wengine 2,800 walijeruhiwa na milipuko hiyo, kulingana na waziri wa afya wa Lebanon.

Timu ya BBC ilikuwa kwenye mazishi ya wanne kati ya waliouawa katika kitongoji cha Beirut kusini mwa Dahiya siku ya Jumatano waliposikia mlipuko mkubwa mwendo wa saa 17:00 kwa saa za huko (14:00 GMT).

Kulikuwa na fujo na mkanganyiko miongoni mwa waombolezaji, na ndipo taarifa zikaanza kuingia za milipuko inayotokea katika maeneo mengine ya nchi pia.

Video moja ya mtandao wa kijamii ambayo haijathibitishwa ilionesha mtu akianguka chini baada ya mlipuko mdogo wakati wa kile kilichoonekana kuwa maandamano ya Hezbollah yaliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Lebanon limesema zaidi ya magari 30 ya kubebea wagonjwa yalikuwa katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu, pamoja na kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa.

Wizara ya afya ilisema milipuko hiyo mibaya "ililenga mazungumzo". Chanzo kilicho karibu na Hezbollah pia kililiambia shirika la habari la AFP kwamba maongezi yaliyotumiwa na wanachama wake yamelipuka.

Shirika la Habari la Taifa la Lebanon (NNA) lilisema mtu mmoja aliuawa wakati simu ya upepo ilipolipuka ndani ya duka la kuuza vifaa vya mkononi huko Chaat, kaskazini mwa Bonde la Bekaa.

Ilitambua kifaa hicho kama redio ya VHF ya ICOM-V82 inayoshikiliwa kwa mkono, ambayo ni muundo ambao hautumiwi kwa sasa unaotengenezwa na kampuni ya kutengeneza vifaa vya kielektroniki yenye makao yake nchini Japan ICOM.

NNA ilisema ICOM-V82 nyingine ililipuka kwenye nyumba nje kidogo ya mji wa karibu wa Baalbek. Picha za video zilionesha uharibifu uliosababishwa na moto kwenye meza na ukuta, pamoja na sehemu zilizoharibika za kile kilichoonekana kuwa redio ya upepo yenye lebo ya "ICOM".

Simu ya upepo yenye nembo ya ICOM iliharibiwa na mlipuko katika nyumba moja nje kidogo ya Baalbek.

Chanzo cha picha, Getty Images

Shirika la habari la Reuters lilinukuu chanzo cha usalama cha Lebanon kikisema simu hizo za upepo zilinunuliwa na Hezbollah miezi mitano iliyopita, karibu wakati uleule wa kununuliwa kwa vifa vya mawasiliano .

Tovuti ya habari ya Axios ilinukuu vyanzo viwili vikisema kwamba idara za kijasusi za Israel zilinasa maelfu ya watoa taarifa kabla ya kuziwasilisha kwa Hezbollah kama sehemu ya mfumo wa mawasiliano wa dharura wa wakati wa vita wa kundi hilo.

BBC iliomba ICOM ya Uingereza kutoa maoni juu ya ripoti hizo, lakini ilielekeza maombi yote ya vyombo vya habari kwa ofisi ya waandishi wa habari ya kampuni hiyo nchini Japan. BBC imewasiliana na ICOM Japan.

Vyanzo vya Marekani na Lebanon vililiambia gazeti la New York Times na Reuters kwamba Israel ilitega kiasi kidogo cha vilipuzi ndani ya vifaa vya mawasiliano vilivyolipuka siku ya Jumanne.

Daktari wa macho katika hospitali moja mjini Beirut aliiambia BBC kwamba takribani asilimia 60 ya watu aliowaona wamepoteza angalau jicho moja, huku wengi wao wakiwa wamepoteza mkono.

"Pengine hii ndiyo siku mbaya zaidi ya maisha yangu kama daktari. Ninaamini idadi ya waliojeruhiwa na aina ya uharibifu ambao umefanywa ni wa kutamausha," Dk Elias Warrak alisema.

"Kwa bahati mbaya, hatukuweza kuokoa macho mengi, na kwa bahati mbaya uharibifu hauko kwenye macho tu, baadhi yao yana uharibifu katika ubongo pamoja na uharibifu wowote wa uso."