Vipodozi: Unajua hatari ya Kope bandia, wanja na rangi ya mdomo unayotumia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Lini ni mara ya mwisho ulikagua tarehe ya mwisho ya matumizi ya vipodozi vyako? Umewahi kufikiria kuwa vipodozi vilivyoisha muda wake vinaweza kuharibu ngozi yako, au hata kuhatarisha afya yako?
Je, wewe huosha brashi zako za mapambo mara ngapi? Umewahi kuazima ujiti wa kupakia wanja kutoka kwa rafiki au kujipaka rangi ya mdomo dukani?
Nakubali kwamba sikuwa mwangalifu sana kuhusu kusafisha vifaa vyangu vya kujipodoa au kuangalia tarehe za mwisho wa matumizi, na hivyo niliamua kuvipeleka Chuo Kikuu cha London Metropolitan nchini Uingereza ili kufanyiwa utafiti.
Dk. Maria Pilar Botesalvo, mhadhiri wa sayansi ya viumbe katika kitivo cha Sayansi ya Binadamu, alisimamia utafiti huo. Aliongoza timu iliyofanyia utafiti zaidi ya kope bandi 70 zilizokwisha muda wa matumizi, vijiti vya kupambia kope, penseli za kupakia rangi ya mdomo, rangi ya kupaka usoni, pamoja na brashi na sponji.
Bakteria

Tuligundua kuwa idadi ya bakteria katika sampuli za vipodozi nilivyopeleka ilikuwa ya juu sana.
"Vipodozi vyenye bakteria zaidi ni kope au penseli ya wanja," anasema Dk. Salo.
Bakteria hao ni pamoja na staphylococcus. Pia tulipata bakteria wa staphylococci katika sampuli nyingine za utafiti, brashi, sponji na ujiti wa kope.'
Bakteria wa staphylococcus wanaweza kusababisha aina nyingi za magonjwa. Ikiwemo kuvimba hadi maambukizi makubwa zaidi kama vile kiwambo cha sikio na maambukizo ya ngozi.
Hapa swali linatokea akilini mwangu; kwa nini sijapata madhara yoyote kati ya haya licha ya kutumia kope hizi za bandi mara nyingi?
"Ikiwa ngozi yako ni nzuri, maanake ina ulinzi mkali," anaelezea Dk Salo. Hakuna kinachoweza kukupata katika hali kama hiyo.'
'Lakini ikiwa ngozi yako imejeruhiwa mahali fulani, kuna mkwaruzo au una vidonda kwenye ngozi yako, hapa ndipo bakteria wanaweza kuingia na kusababisha uharibifu.
"Ikiwa mtu ana mfumo dhaifu wa kinga ya mwili, bakteria wanaweza kuleta matatizo pia.."
Kunawa mikono

Aina zote za bakteria zinaweza kuwa kwenye mikono, na ikiwa husafishi mikono, kuna hatari ya kuhamisha vijidudu kutoka katika mikono hadi katika vipodozi vya urembo.
Dk. Buti Salo baada ya utafiti wa baadhi ya bidhaa hizi, amesema "tulipata bakteria kama Enterobacteriaceae, ambayo kwa kawaida hupatikana kwenye utumbo."
Hii ni kutokana na usafi mdogo, na wadudu hawa wametoka kwenye kinyesi kupitia matone ya maji wakati wa kujisafisha au kusafisha choo.
Baadhi ya bakteria aina ya Enterobacteriaceae wanaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo, maambukizi ya njia ya hewa, maambukizi ya mifupa na moyo.
Fangasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Timu ya watafiti katika Chuo Kikuu cha Metropolitan pia imepata fangasi wanaoitwa Candida katika vipodozi. Ikiwa fangasi hawa wataingia kwenye ngozi, wanaweza kusababisha malengelenge na kuwashwa ukeni au mdomoni.
Utafiti uliofanywa kwa vipodozi 500 katika Chuo Kikuu cha Aston huko Birmingham, Uingereza - umegundua kuwa asilimia 79 hadi 90 ya vipodozi ambavyo watu hutumia vina aina fulani ya vijidudu, bakteria, au fangasi.
Dk. Amreen Bashir, mtafiti mkuu wa utafiti huo, alisema "ingawa kuna bakteria kwenye vipodozi, lakini si lazima wawe na hatari kubwa ya kuambukiza. Maambukizi yanahitaji njia ya maambukizi, kama vile mkwaruzo.
Usafi, ikiwa ni pamoja na kuosha na kuua vijidudu, kunaweza kupunguza hatari.
Muda wa kumaliza

Tarehe ya mwisho wa matumizi ni muhimu kwa sababu inaonyesha muda gani dawa katika bidhaa inaweza kuzuia ukuaji wa vijidudu. Bidhaa zilizo na kiwango cha juu cha maji zinaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata vidudu baada ya kufunguliwa, kwani hutoa mazingira rafiki kwa bakteria na fangasi kukua.
Bidhaa zina tarehe tofauti za mwisho wa matumizi na tarehe ya mwisho baada ya kufungua bidhaa ni kati ya miezi 3 hadi 12.
Dk. Amreen Bashir anasema, "ikiwa vipodozi havina tarehe ya mwisho wa matumizi, inashauriwa kuitupa baada ya miezi mitatu au mara tu unapofahamu kuwa imeingia vijidudu, kama vile ikianguka chini au kutumiwa na watu wengine, ili kupunguza hatari ya kuambukizwa."
"Ikiwa watumiaji hawana uhakika kama vipodozi vyao vimeisha muda wake, ni bora kununua bidhaa mpya badala ya kuendelea kuitumia," ameongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Dk. Buti Salvo anatoa vidokezo vichache vya kuzuia vipodozi kuingia vijidudu:
- Osha mikono yako kabla ya kupaka vipodozi.
- Usitumie vifaa vya kupaka vipodozi kwenye maduka kwa sababu hujui ikiwa watu waliotumia bidhaa hizo waliosha mikono yao au la.
- Safisha vifaa kama vile sponji na brashi mara kwa mara kwa maji ya moto na sabuni, na vikaushe vizuri.
- Mahali pabaya zaidi pa kuhifadhi vipodozi ni bafuni kwa sababu kuna unyevunyevu na giza.
- Funika vipodozi vyako na vifuniko. Hilo litatoa ulinzi dhidi ya vijidudu vilivyo hewani na kuzuia chembe za vumbi kujilimbikiza.
- Zingatia tarehe ya kumalizika muda wake.
- Na usiruhusu wengine watumie vipodozi vyako.















