'Niliwasababishia makovu wanangu kwa kutumia mafuta ya kung'arisha ngozi'

Na Madina Maishanu
BBC Hausa
Fatima anaonekana kukasirika anapompakata mwanaye mwenye umri wa miaka miwili, ambaye ana madoa doa ya kuungua na ngozi iliyobadilika rangi usoni na miguuni mwake.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 alitumia vipodozi vya kung'arisha ngozi kwa watoto wake wote sita, chini ya shinikizo kutoka kwa familia yake, na sasa matokeo yake anayajutia sana.
Binti mmoja hufunika uso wake kila anapotoka nje, ili kuficha kuungua kwa ngozi yake.
Mwingine aliachwa na ngozi nyeusi kuliko hapo awali, na mduara wa rangi karibu na macho yake, Fatima anasema, wakati wa tatu akiwa na makovu meupe kwenye midomo na magoti yake. Mtoto wa miaka miwili bado ana majeraha ya kulia - ngozi yake imechukua muda mrefu kupona.
"Dada yangu alizaa watoto wenye ngozi nyeupe lakini watoto wangu wana ngozi nyeusi. Niligundua kuwa mama yangu anawapendelea watoto wa dada yangu kuliko wangu kwasababu ya rangi yao ya ngozi na iliniumiza sana hisia zangu," Fatima anasema.
Anasema alitumia krimu alizonunua kwenye duka la karibu, bila agizo la daktari.

Mwanzoni ilionekana kufanya kazi. Bibi yao aliwakumbatia watoto wa Fatima, ambao walikuwa na umri wa kati ya miaka miwili na 16 wakati huo. Lakini baadaye wakaanza kuungua na makovu yalianza kujitokeza wazi.
Vipodozi vya Kung'arisha ngozi au kuifanya iwe nyeupe pia hujulikana kama bleaching nchini Nigeria, na hutumiwa katika sehemu mbalimbali za dunia kwasababu za urembo, ingawa hizi mara nyingi vipodozi hivyo hutengenezwa majumbani.
Wanawake wa Nigeria hutumia bidhaa za kung'arisha na kuchubua ngozi zaidi kuliko nchi nyingine barani Afrika - 77% kati yao hutumia vipodozi hivi mara kwa mara, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Nchini Kongo-Brazzaville idadi ni 66%, nchini Senegal 50% na Ghana 39%.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Krimu zinaweza kuwa na corticosteroids au hydroquinone, ambayo inaweza kuwa na madhara ikiwa inatumiwa kwa kiasi kikubwa, na katika nchi nyingi zinapatikana tu kwa maagizo ya daktari. Viungo vingine wakati mwingine hutumiwa ni chuma chenye sumu, zebaki, na asidi ya kojic - bidhaa kutoka kwa utengenezaji wa kinywaji cha pombe cha Kijapani, sababu.
Dermatitis, chunusi na kubadilika rangi kwa ngozi ni matokeo yanayowezekana, lakini pia matatizo ya uchochezi, sumu ya zebaki na uharibifu wa figo. Ngozi inaweza kuwa nyembamba, na matokeo yake majeraha huchukua muda mrefu kupona, na kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa, WHO inasema.
Hali ni mbaya sana hivi kwamba Wakala wa Kitaifa wa Utawala na Udhibiti wa Chakula na Dawa wa Nigeria (Nafdac) ulitangaza hali ya hatari mnamo 2023.
Pia inazidi kuwa kawaida kwa wanawake kuwapausha watoto wao, kama Fatima.
Zainab Bashir Yau, mmiliki wa kituo cha mapodozi ya ngozi ngozi huko Abuja, anasema watu hufanya hivyo kwasababu ngozi nyepesi inahusishwa na utajiri na hadhi ya juu ya kijamii.
Anakadiria kuwa 80% ya wanawake ambao amekutana nao wamewapausha watoto wao, au wanapanga kufanya hivyo. Wengine walipaushwa wenyewe wakiwa watoto wachanga, anasema, kwa hivyo wanaendelea na mazoezi hayo.
Mojawapo ya njia za kawaida za kujua ikiwa mtu anatumia bidhaa za kung'arisha ngozi nchini Nigeria ni kwa weusi wa viwiko na vifundo vyao. Sehemu zingine za mikono au miguu ya watu huwa vyeupe lakini viwiko na vifundo huwa vyeusi
Hata hivyo, wavutaji sigara na watumiaji wa dawa za kulevya pia wakati mwingine huwa na mabaka meusi mikononi mwao, kutokana na moshi. Kwa hivyo watumiaji wa bidhaa za kung'arisha ngozi wakati mwingine hudhaniwa kimakosa kuwa wa kikundi hiki.

Fatima anasema ndivyo ilivyotokea kwa binti zake, wenye umri wa miaka 16 na 14.
"Walikabiliwa na ubaguzi kutoka kwa jamii - wote wanawanyooshea vidole na kuwaita waraibu wa dawa za kulevya. Hii imewaathiri sana," anasema.
Wote wawili wamepoteza uwezekano wa kupata wachumba kwasababu wanaume hawataki kuhusishwa na wanawake ambao wanaweza kudhaniwa kutumia dawa za kulevya.
Nilitembelea soko maarufu katika jimbo la Kano, ambapo watu wanaojiita wachanganyaji hutengeneza mafuta ya kung'arisha ngozi.
Soko lina safu nzima ya maduka ambapo maelfu ya krimu hizi zinauzwa. Baadhi ya aina zilizochanganywa awali zimepangwa kwenye rafu, lakini wateja wanaweza pia kuchagua viungo ghafi vya vipodozi hivyo na kuomba krimu ichanganywe mbele yao.
Niligundua kuwa mafuta mengi ya kublichi na lebo zinazosema zilikuwa za watoto wachanga, zilikuwa na vitu vilivyozuiwa.
Wauzaji wengine walikiri kutumia viambato vilivyozuiwa kama vile asidi ya kojic, hidrokinoni na antioxidant yenye nguvu, glutathione, ambavyo vinaweza kusababisha upele na madhara mengine.
Pia nilishuhudia wasichana wadogo wakijinunulia krimu za kuchubua ngozi na kwa wingi ili waweze kuziuza kwa wenzao.

Mwanamke mmoja, ambaye alikuwa amebadilika rangi, alisisitiza kwamba muuzaji aongeze hydroquinone kwenye krimu ambayo ilikuwa ikichanganywa kwa watoto wake, licha ya kwamba kiungo hiki kimezuiwa kwa watu wazima na ni marufuku kutumia kwa watoto.
"Ingawa mikono yangu imebadilika rangi, niko hapa kuwanunulia watoto wangu krimu ili waweze kuwa na ngozi nyepesi. Ninaamini mikono yangu iko hivi kwasababu tu nilitumia ile mbaya. Hakuna kitakachotokea kwa watoto wangu," alisema.
Muuzaji mmoja alisema wateja wake wengi walikuwa wakinunua krimu ili kuwafanya watoto wao "kung'aa", au kuonekana "weupe wenye ngozi laini".
Wengi walionekana kutojua kipimo kilichoidhinishwa.
Muuzaji mmoja alisema alitumia "kojic nyingi", ikiwa mtu alitaka ngozi nyepesi, na "kijiko kidogo" ikiwa anataka mabadiliko ya kidogo.
"Tunatumia vijiko kupima. Tunatumia kijiko kamili katika krimu za watu, ambayo ni kama 40% ya asidi ya kojic kwenye krimu ya mtu."
Kipimo kilichoidhinishwa cha asidi ya kojic katika krimu nchini Nigeria ni 1%, kulingana na Nafdac.
Niliona hata wauzaji wakiwapa wanawake sindano.

Dk Leonard Omokpariola, mkurugenzi wa Nafdac, alisema majaribio yanafanywa kuelimisha watu juu ya hatari. Pia alisema masoko sasa yanavamiwa, na juhudi zinafanyika kukamata viungo vya kung'arisha ngozi kwenye mipaka ya Nigeria wakati vikiingizwa nchini.
Lakini alisema wakati mwingine ilikuwa ngumu kwa maafisa wa kutekeleza sheria kutambua vitu hivi.
"Baadhi ya viungo hivyo vinasafirishwa tu kwenye vyombo visivyo na lebo, kwa hivyo usipovipeleka kwenye maabara kwa tathmini, huwezi kujua kilichomo ndani."
Fatima anasema matendo yake yatamsumbua milele, haswa ikiwa makovu ya watoto wake hayatafifia.
"Nilipomwambia mama yangu juu ya kile nilichofanya, kwasababu ya tabia yake, na aliposikia hatari za krimu na unyanyapaa gani wajukuu zake wanakabiliana nao, alihuzunika kwamba walilazimika kupitia hilo na kuomba msamaha," alisema.
Amedhamiria kuwasaidia wazazi wengine kuepuka kufanya kosa lile lile.
"Ingawa nimeacha... madhara bado yapo, ninawaomba wazazi wengine watumie hali yangu kama mfano."
* Jina la Fatima limebadilishwa ili kulinda utambulisho wa familia yake














