Je unajua mikono yako ni 'hatari' kwa maisha?

G

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi

Umuhimu wa kunawa mikono na kuiweka katika hali ya usafi linaweza kuonekana ni jambo la kawaida, na kwa baadhi huenda likawa ni jambo la ‘aibu’ kumkumbusha mtu anawe mikono anapotoka kwenye matembezi yake.

 Lakini hii inaweza kuwa ni hatua muhimu tunayoichukua ili kuepuka kuugua wenyewe pamoja na kusambaza viini vya magonjwa hatari kwa wengine.

Ukweli ni kwamba magonjwa mengi na hali mbaya za kiafya husambazwa kwa njia ya mikono yetu kwa kutoinawa kwa sabuni na maji yanayotiririka.

Huenda usitambue ni kwa jinsi gani hasa mikono yako ni hatari kwa maisha yako, lakini ukweli ni kwamba mikono yako ni hatari isipotunzwa kwa usafi. Kwa siku tunayagusa mamia ya maeneo ambayo sio safi , ambayo yote ni makao ya vimelea wa magonjwa mbali mbali,

Karibu 80% ya magonjwa yanayosababishwa na viini husambazwa kwa njia ya mikono, linasema Mamlaka ya kuzuia na kudhibiti magonjwa nchini Marekani (CDC).

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kusalimiana kwa mikono ni njia mojawapo ya kuonesha ukarimu, lakini pia inaweza kuhatarisha afya ya maisha yako

Ni kwanini vimelea ni viumbe hatari sana?

Kiini ni kiumbe kidogo sana kinachoweza kusababisha magonjwa au ugonjwa. Vimelea wanaweza kuingia mikononi mwako baada ya kutumia choo, kubadilisha nepi (diaper), kukata au kushika nyama mbichi, au kugusa kitu chochote chenye vimelea.

Wakati haunawi mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka viini vya magonjwa kama vile virusi na bakteria huweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, na bila shaka usingependa kuugua.

G

Chanzo cha picha, Dr William sagilai

Maelezo ya picha, Daktari William Sigilai, anasisitizia umuhimu wa waandalizi wa chakula kudumisha usafi wa mikono yao ili kuepuka kusambaza viini vya magonjwa

Ukweli ni kwamba baadhi ya magonjwa yanayosambazwa kwa mikono michafu yanaweza kuwa mabaya zaidi.

Pili , wale wanaoumwa wanaweza kuathirika kifedha, kwa kulipa gharama za juu za matibabu.

 Pili ni kwamba ni kwamba watu wengi wanaougua, hupewa dawa za kukabiliana maambukizi,(antibiotics) ambazo mara nyingi sio muhimu.

‘’Kadri unavyotumia dawa za maambukizi ndivyo unavyojenga kinga dhidi yake na hivyo hazitafanya kazi ya kupambana na maambukizi utakayoyapata tena’’ Aliiambia BBC, Dkt Timona Obura wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan mjini Nairobi.

Magonjwa yanayosambazwa kupitia mikono.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulinaganana Dkt William Sigilai wa Hospitali ya rufaa ya Kenyatta mjini Nairobi kuna magonjwa mbali mbali yanayosambazwa kupitia mikono, yakiwa ni yale ya tumbo kama vile homa ya tumbo(Typhod), na kipindupindu yanayosababisha kuhara na kutapika

Mengine ni yale yanayoshambulia mfumo wa kupumua kama vile homa ya mafua ya kawaida, Influenza, Covid na kifua kikuu.

‘’Watu wanapaswa kunawa kwa maji safi na vitakasa mikono (sanitizer) hasa wanapotumia choo, kabla ya kupika chakula ili kuepuka viini vya magonjwa kusambaa kwa watu wengine’’.

 Unapopiga chafya au kukohoa na kuweka mkono wako kwenye kinywa na kisha unasalimiana na watu, au unashika kwenye maeneo mbali mbali bila kunawa viini vinasambaa kwa watu wengine utakao wasalimia au watakaogusa eneo uliloligusa… kudumisha usafi wa mikono ni muhimu’’ alisisitiza Dkt. Sigilai.

Licha ya hayo na magonjwa mengi yatokanayo na maambukizi ya macho na na ya ngozi pia husambazwa kwa mikono yetu.

Ni dhahiri kwamba janga la covid lililoikumba dunia limechangia pakubwa katika uhamasishaji wa usafi wa mikono, lakini Dkt Sigilai anasema bado magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya mikono yapo na ni hatari kwa maisha hasa pale mgonjwa anapochelewa kutibiwa.

Ukweli kuhusu viini hatari vinavyosambazwa kwa mikono yetu:

  • Kiini kimoja kinaweza kuzaa zaidi ya viini milioni 8 kwa siku moja
  • Karibu 80 ya magonjwa yanayosababishwa na viini husambazwa kwa njia ya mikono
  • Rimoti unayoitumia kutazama TV hubeba bakteria zaidi kuliko vifaa vingine vya nyumbani
  • Kuna viini zaidi kwenye simu yako ya mkononi, keyboard kuliko kiti cha choo (toilet seat).
  • Mtu mmoja kati ya watu watano hawanawi mikono yao na kati ya wale wanaonawa mikono yao, ni 30% pekee wanaotumia sabuni mara kwa mara .
  • Wakati unapo flash maji chooni, viini vinaweza kupaa futi 6 juu

Chanzo : Centers for Disease Control and Prevention( CDC)

Je ni njia ipi bora ya kunawa mikono yako? Tumia tu sabuni na maji!

  • Lowesha mikono yako, kisha ufunge maji, halafu upake sabuni mikono
  • Fikicha mikono yako pamoja mpaka povu jingi la sabuni
  • Safisha maeneo kuanzia kwenye vidole na chini ya kucha hadi juu ya kiganja na kisha nyuma ya kiganja
  • Sugua kwa walau sekunde 20.
  • Fungua tena maji na isuuze vizuri mikono yako
  • Kausha mikono yako na taulo safi au kitambaa na utumie kitambaa au taulo kufunga bomba la maji

 Chanzo: CDC

Sayansi isemavyo kuhusu faida za kunawa mikono vyema

Wakati unaponawa mikono yako, unaweza kuzuia ugonjwa 1 kati ya magonjwa 3 yanayohusiana na kutapika na 1 kati ya maambukizi 5 ya mfumo wa upumuaji kama vile mafua na homa, inasema Mamlaka ya kuzuia na kudhibiti magonjwa nchini Marekani (CDC).

Utafiti kuhusu usafi wa mikono uliofanywa na Shirika la afya ya umma nchini Marekani (AMHA) pia unaonyesha kuwa usafishaji wa bora wa mikono unaweza kupunguza magonjwa ya utumbo kwa 31% na kupunguza magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa 21%.

 Kunawa mikono ipasavyo kwa kutumia vitakasa mikono na sabuni kwa sekunde 40 kunaweza kuua viini vya maambukizi, ulionyesha utafiti wa AMHA.

Epuka maambukizi hatari yanayoweza kuua, kupoteza pesa kwa njia ya matibabu au kutumia dawa bila sababu, kumbuka kunawa mikono kila mara kwa sabuni na maji safi yanayotiririka.