Fatphobia: 'Kwani kuwa mnene ni dhambi katika nchi hii?'

Rayane Souza alikwepa kupanda mabasi ya jiji baada ya miaka mingi ya kuhangaika kupanda
Maelezo ya picha, Rayane Souza alikwepa kupanda mabasi ya jiji baada ya miaka mingi ya kuhangaika kupanda.

Rayane Souza alikuwa akipata shida kupanda basi huko Vitória, mji mkuu wa jimbo la Espírito Santo nchini Brazil, kilomita 480 kaskazini mwa Rio de Janeiro.

Akiwa na umri wa miaka 14, aliwahi kukwama kwenye basi, na kuhisi macho ya abiria wengine yalikuwa yakimtazama, aliapa kutotumia tena aina hii ya usafiri wa umma.

"Nimekuwa mnene maisha yangu yote. Nilizoea kusikia maoni yasiyofaa kuhusu uzito wangu," alisema.

Kisa chaBi Souza sio chaa kipekee. Mwanamke mwingine wa Brazil hivi majuzi alikwama kwenye kwenye basi kwa zaidi ya saa nne. Mwishowe, wazima moto waliitwa ili kumsaidia.

Abiria wachache walijaribu kumsaidia, lakini alisema wengine walichapisha picha zake za aibu kwenye mitandao ya kijamii.

Alipokuwa akisoma chuo kikuu, Bi Souza alifedheheshwa vivyo hivyo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukejeliwa na kunyanyaswa shuleni kuhusiana na uzito wake.

"Nilikuwa mwathirika wa uonevu, kutokana na unene wangu. Wanafunzi wote walitengeneza kundi la WhatsApp na wakachukua picha zangu nilizochapisha mitandaoni na kuanza kunifanyia mzaha."

Huo ulikuwa wakati mgumu sana kwa Bi Souza. Badala ya kujificha na kunyong'onyea, aliamua hatatishika.

Aliamua kuungana na na mhitimu mwenzake wa sheria Mariana Oliveira na kuanzisha kikundi cha kampeni. Waliipatia jina la Gorda na lei, kwa Kireno "Fat in the law".

Inalenga kuwashauri watu kuhusu haki zao za kisheria ikiwa wanabaguliwa kwa sababu ya uzito wao. Wanapokea karibu jumbe 70 kwa mwezi kutoka kwa watu wanaotaka fidia au kusimulia hadithi zao tu.

Kukubali maumbo tofauti ya mwili

Brazili huenda inajulikana kwa ''dhana potofu'' kwamba ina watu wenye miili mizuri na walio tayari kwenda ufukweni, lakini ukweli ni kwamba, kama ilivyo katika nchi zingine zilizoendelea, zaidi ya nusu ya watu wana uzito kupita kiasi, na robo yao wana unene wa kupindukia.

Mwanamke mnene

Wanaharakati wanasema jamii inapaswa kukubali hili. Wanasema Brazil ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kulazimisha kwa mafanikio kupitia mabadiliko ya sera ili kukidhi maumbo tofauti ya miili.

Kulingana na takwimu rasmi, kuna zaidi ya visa 1,400 zilizowasilishwa mbele ya tume maalum kuhusiana na jinsi watu nchini Brazil walivyo na hofu juu ya muonekano wa miili yao.

Hata ingawa woga wa unene sio uhalifu maalum, unaweza kutekelezwa chini ya kanuni zilizopo za kisheria kama vile kashfa, na unyanyasaji wa maadili, anaelezea Bi Oliveira, ambaye sasa ni mwanasheria wa haki za binadamu.

Anataja kesi moja ambapo mmiliki wa biashara aliweka sharti la kulipa bonasi kwa mmoja wa wafanyikazi wake endapo angelipunguza uzito. "Hata alimfanya aruke kwenye mizani," Bi Oliveira anasema.

Mariana Oliveira
Maelezo ya picha, Wakili wa haki za binadamu Mariana Oliveira amepokea visa kadhaa vya ubaguzi unaohusiana na unene.

Jaji aliamua mfanyakazi huyo alipwe fidia ya dola 1,900 za Kimarekani - mojawapo ya kiasi cha juu zaidi kilichosajiliwa nchini Brazili kinachohusisha kesi ya chuki dhidi ya unene, lakini bado ni kiasi kidogo ikilinganishwa na maamuzi mengine katika mfumo wa mahakama wa Brazil.

Mojawapo ya maeneo nchini Brazili ambapo mabadiliko ya sera yamefanywa ni katika jiji la Recife.

Mswada uliopitishwa na baraza lake mwaka jana unalazimu shule kuwa na madawati makubwa zaidi.

Diwani wa Recife Cida Pedrosa alikuwa mtoa hoja mkuu katika kutambulisha sheria mpya: "Visa vingi nilivyosikia ni vya watu kudhalilishwa kwa sababu hawakuweza kutoshea kwenye dawati la shule."

Sheria mpya iliyopitishwa na Bi Pedrosa inamaanisha kila shule ya Recife ina dawati kubwa katika kila darasa.

Cida Pedrosa

Chanzo cha picha, CIDA PEDROSA

Maelezo ya picha, Diwani wa jiji hilo Cida Pedrosa alisaidia kupitisha sheria mpya ya kuundwa kwa viti na madawati makubwa kwa watu wenye uzito mkubwa.

Bi Pedrosa anapinga pendekezo kwamba kufanya mabadiliko haya kunamaanisha kuachana na juhudi za kuwafanya Wabrazil wanene na wenye unene kupita kiasi wapunguze uzani.

"Hatukatai kwamba katika baadhi ya matukio, unene unaweza kuleta matatizo ya kiafya. Lakini pia tunapaswa kukubali miili ya aina yote na kuepusha dhana kwamba watu wanene ni wagonjwa."

Hakuna kampeni ya kitaifa nchini Brazil ya kuhimiza watu kupunguza uzito, na endapo hilo litatokea wataalamu wa afya watabuni jinsi ya kufikisha ujumbe bila kuwanyanyapaa watu wanene kupita kiasi.

Madaktari wengi wa Brazil wanaamini kuwa wagonjwa walio na uzito kupita kiasi wanapaswa kuambiwa moja kwa moja kwamba wanahitaji kupunguza uzito.