Kwa nini Siku ya Wafanyakazi Duniani inaadhimishwa Mei 1?

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Natasa Andjelkovic
Role,BBC News Serbian
Katika nchi nyingi, Mei 1 inajulikana kama likizo ya msimu wa masika, lakini siku hizi inajulikana zaidi kama Siku ya Wafanyakazi (au Siku ya Wafanyakazi wa Kimataifa) kukumbuka mapambano ya kihistoria na maendeleo yaliyofanywa na wafanyakazi duniani kote.
Kila mwaka, maandamano huandaliwa duniani kote kudai mazingira bora ya kazi na nguvu ya muungano.
Awali, siku hii iliadhimishwa na mashirika mbalimbali ya kikomunisti na vikundi vya wafanyakazi.
Ingawa maandamano ya kwanza yalifanyika nchini Marekani, siku hiyo inaadhimishwa Jumatatu ya kwanza ya Septemba nchini humo.
Ilianzaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1886, vyama vya wafanyakazi vya Marekani vilianzisha mgomo wa watu wengi kudai kufanya kazi saa nane kwa siku , kwa kuzingatia wazo la mwanamageuzi wa kijamii wa Uingereza Robert Owen. Aliandaa lengo la siku ya kazi ya saa nane na kauli mbiu ‘’saa nane za kazi, saa nane za kucheza, saa nane za kupumzika."
Maandamano hayo makubwa yalifanyika mjini Chicago mnamo Mei 1 na kuhudhuriwa na wafanyakazi 40,000. Wakati huo, ilikuwa kawaida kufanya kazi nzito katika viwanda, bila kujali saa ngapi za kazi au siku za kupumzika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huo, Chicago ilikuwa kitovu cha tasnia cha Marekani na kituo cha kuandaa kazi.
Katika siku zilizofuatia, maandamano hayo ambayo hayakutazamwa vyema na duru za kiuchumi na kisiasa – yaliungwa mkono na maandamano mengine ya maelfu ya wafanyakazi wengine wasio na uwezo na watawala. Watawala wakati huo walikuwa watu ambao walipinga miungano mingine mbali na utawala na polisi.
Hali ya wasiwasi ilikuwa kubwa na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji yalisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Wakikasirishwa na ukatili wa polisi, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na washambuliaji waliandaa maandamano siku iliyofuata, Mei 4, katika uwanja maarufu wa Haymarket mjini Chicago.
Mshambuliaji ambaye bado hajajulikana alirusha bomu kwa polisi na kwa sababu ya mlipuko huo na hofu iliyojitokeza, maafisa saba wa polisi walifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Washambuliaji wasiopungua wanne pia waliuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.
Kufuatia kile kilichojulikana kama mauaji ya Haymarket Massacre au the Haymarket Affair, watu wanane walishtakiwa kwa mauaji na baadhi yao walihukumiwa kifo, ingawa hatia yao haikuthibitishwa kamwe.
Mwaka 1889, iliamuliwa kuadhimisha matukio haya mnamo Mei 1 katika Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Pili, mkutano wa vyama vya kisoshalisti na wafanyakazi na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka nchi 20.
Nchi mpya ziliidhinisha Mei 1
Makabiliano ya Chicago yalichochea kuibuka kwa vyama vingi vya mrengo wa kushoto katika miaka iliyofuata.
Katika Ulaya ya Kusini, Walovania na Wacroasia katika kile kilichokuwa wakati huo Dola ya Austro-Hungarian walikuwa wa kwanza kusherehekea Mei 1.
Hali ngumu ya kufanya kazi, mshahara mdogo na masaa marefu ya kufanya kazi haraka yalisababisha wafanyikazi nchini Serbia kuandaa mkutano wa Siku ya Mei 1 mnamo 1893.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, dhidi ya maendeleo ya haraka ya viwanda na chini ya ushawishi wa mapinduzi ya kikomunisti nchini Urusi, wafanyakazi walipigania haki zao za msingi duniani kote.
Nchini Ujerumani, Siku ya Wafanyakazi ikawa likizo rasmi mwaka 1933, baada ya chama cha Nazi kuingia madarakani.
Kwa kushangaza, chama hiki kilifuta vyama huru siku moja baada ya likizo kuanzishwa, karibu kuharibu harakati za kazi za Ujerumani (ingawa vyama vya wafanyakazi vilijengwa upya baada ya Vita vya Pili vya Dunia).
Mashariki na Magharibi

Chanzo cha picha, YUGOSLAVIA MUSEUM
Baada ya ushindi wa Muungano katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ramani ya dunia ilibadilika na mgawanyiko wa kisiasa na kiuchumi ukazidi kuwa mkubwa.
Siku ya Wafanyakazi imekuwa ikiadhimishwa kwa miongo kadhaa katika nchi za kisoshalisti kama vile Cuba, Muungano wa Sovieti na China, kama moja ya likizo muhimu zaidi.
Kwa kawaida ilikuwa na gwaride kubwa, kama lile lililofanyika kwenye Red Square huko Moscow, mbele ya viongozi wa juu wa chama na serikali. Pia lilikuwa ni ishara ya nguvu za kijeshi za Usovieti.
Viongozi wa Kikomunisti waliamini kwamba sikukuu hii mpya na sherehe ingehamasisha vyama vya wafanyakazi vya Ulaya na Marekani kuungana katika vita dhidi ya ubepari.
Vivyo hivyo ilikuwa kweli katika Jamhuri ya Shirikisho la Kisoshalisti ya Yugoslavia, ambapo Mei 1 ilitangazwa rasmi kuwa likizo ya umma mnamo 1945, iliyoadhimishwa na gwaride la kijeshi, pamoja na sherehe ya tuzo.
Gwaride la kijeshi, pamoja na kipimo kikubwa cha propaganda za serikali.
Kwingineko duniani, vyama vya wafanyakazi pia walifanya maandamano Mei 1 ili kudai mazingira bora ya kazi.
Haki za wafanyakazi bado ni muhimu wakati kukiwa na utabiri wa kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na umaskini wa kazi.
Licha ya kushuka kwa ukosefu wa ajira na ukuaji mzuri wa ajira, mishahara halisi ilishuka katika nchi nyingi za G20 wakati ongezeko la mshahara lilishindwa kuendana na mfumuko wa bei mwaka jana, linasema Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika ripoti yake ya utabiri wa 2024.
Mwaka jana, idadi ya wafanyakazi wanaoishi katika umaskini uliokithiri - hupata chini ya $ 2.15 kwa siku kwa kila mtu iliongezeka kwa karibu milioni moja duniani, linaeleza shirika la ILO.
Na idadi ya wafanyakazi wanaoishi katika umaskini wa wastani iliongezeka kwa karibu milioni 8.4 (yaani, wale wanaopata chini ya $ 3.65 kwa siku kwa kila mtu) ripoti hiyo inaongeza.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












