Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watu mashuhuri waliotawala vichwa vya habari duniani 2023
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Mwaka 2023 ulianza na muendelezo wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine.
Vyombo vikuu vya habari kote duniani vikiangazia makabiliano yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Ukraine na juhudi zilizokuwa zikifanywa na Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa mtaifa ya magharibi, kuomba msaada wa kijeshi.
Muda ulivyosonga juhudi hizo inaonekana zilizaa matunda kwani mambo yalibadilika ghafla dhidi ya wanajeshi wa Urusi katika uwanja wa vita baada ya vikosi vya Ukraine kufanikiwa kukomboa maeneo yaliyokuwa yanakaliwa na Warusi mashariki mwa nchi hiyo.
Kujibu mashambulizi hayo Urusi iliimarisha kikosi chake kupitia jeshi la kukodi la Wagner ambalo lilipewa nafasi ya kuwasajili wapiganaji zaidi baadhi yao kutoka magerezani.
Hatua hiyo iliibua mvutano mkali kati ya majenerali wa jeshi hilo na kiongozi wa kundi la Wagner Yvgeny Prigozhin ambaye alilalamikia hujuma zinazofanywa na baadhi ya wakuu wa jeshi la Uruso dhidi ya wapiganaji wake kwa kutowapa silaha za kutosha.
Vuta ni kuvute hii iliendelea kwa miezi kadha hadi Bw Prigozhin alipofanya jambo ambalo halikutarajiwa- kutangaza uasi dhidi ya utawala wa Rais Vladmir Putin.
Katika makala haya maalum ya mwisho wa mwaka tunaangazia matukio makuu katika mzozo wa Urusi na Ukraine na hatimaye kutupia jicho mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati baina ya Israel na Palestina.
Yvgeny Prigozhin
Kifo cha aliyekuwa mshirika wa karibu na Rais wa Urusi, kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin kilizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Urusi mwaka 2023.
Hii ni kwa sababu kifo hicho kilitokea wiki kadhaa baada ya Prigozhin kuanzisha uasi dhidi ya utawala wa Putin katika tukio lililofichua migawanyiko ya kina ndani ya serikali ya Urusi kuhusiana na uvamizi wa Ukraine.
Licha ya Kremlin kuahidi kuwa kesi ya jinai dhidi ya Prigozhin itafutwa na wapiganaji wake kutochukuliwa hatua za kisheria kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza mgogoro huo kumekuwa na mashaka ikiwa ilimaanisha ilichosema. Swali lililokuwa vinywani mwa wengi likawa Je Putin anasamehe usaliti?
Wakati watu wakisubiri kuona uhusiano wa siku zijazo kati ya wawili hao utakavyo kuwa mkasa ambao haukutarajiwa ukatokea mnamo Agosti 23, wakati ndege ya kibinafsi iliyombeba Prigozhin na msaidizi wake Dmitry Utkin, ilipoanguka katika mkoa wa Tver karibu na Moscow.
Siku chache baadaye, mamlaka ya Urusi ilithibitisha vifo vyao baada ya vipimo vya DNA kufanywa.
Tafsiri mbali mbali na nadharia za kula njama ziliibuka baada ya ajali hiyo, lakini wapo wanaosema mlipuko ulitokea ndani ya ndege yenyewe. Wengine wakidai ilidunguliwa kutoka ardhini. Kila mmoja ana hoja zake. Lakini hakuna jibu la wazi lililopatikana kwa kile kilichotokea.
Putin
Rais wa Urusi Vladmir Putin tayari alikuwa vinywani mwa watu duniani tangu alipoanzisha uvamizi wa nchi yake dhidi ya Ukraine Februari 24, 2022.
Lakini kifo cha kutatanisha cha kiongozi wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin kiliekezea darubini moja kwa moja Rais Putin. Madai yakitolewa kwamba kuna mkono wake katika kifo hicho licha yakuwa kilitokana na ajali ya ndege kama ilivyothibitishwa na Urusi.
Kauli zilizotolewa na baadhi ya walinzi wa Moscow wakimwelezea Prigozhin kama ''maiti inayotembea'', tangu alipoongoza uasi dhidi ya Moscow mwishoni mwa Juni huenda zilichochea nadharia hiyo na swali la iwapo Prigozhin alifariki kutokana ana ajali ya ndege au aliuawa bado halijapata ufumbuzi.
Putin hata hiyo ameendelea kuiweka nchi yake kwenye mkondo wa vita na kuimarisha nguvu yake ya kiutawala. Amenunua vifaa vya kijeshi nje ya nchi na anasaidia kugeuza ulimwengu wa kusini dhidi ya Marekani.
Kimsingi, anadhoofisha imani ya nchi za Magharibi kwamba Ukraine inaweza—na lazima—itoke kwenye vita kama demokrasia inayostawi ya Ulaya.
Benjamin Netanyahu
Watu wengi nchini Israel humwita 'Bwana Usalama'. Benjamin Netanyahu ndiye waziri mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi Israel tangu taifa hilo kupata uhuru wake mwaka 1948. Aliingia madarakani takriban miongo mitatu iliyopita na tangu wakati huo lengo lake la kwanza limekuwa kulinda Israel.
Lakini mnamo Oktoba 7, Netanyahu alipata pigo kubwa wakati Hamas, kundi la wapiganaji la Palestina ambalo linatawala Ukanda wa Gaza, liliposhambulia miji ya karibu ya Israeli.
Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, zaidi ya watu 1,200 waliuawa huku wengine 240 wakichukuliwa mateka katika shambulio hilo la Hamas.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya watu elfu 11 wamefariki huko hadi sasa kutokana na operesheni ya Israeli huku watoto 4,000 pia wakijumuishwa katika idadi ya waliofariki. Vifo hivyo vimetokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Israel na mashambulizi ya ardhini.
Netanyahu anakabiliwa na labda mojawapo ya hali ngumu zaidi katika kazi yake ya muda mrefu. Sauti za maandamano dhidi ya Israel zinazidi kupata nguvu katika ngazi ya kimataifa.
Wakosoaji wanasema kuwa Israel imefanya mauaji ya halaiki na kwamba hatua zinazochukuliwa dhidi ya raia wa Palestina ni kubwa kuliko uharibifu ulioipata Israel.
Kando na 'Bwana Usalama', kuna majina mengine yanayotumiwa kwa Netanyahu katika siasa za Israel.
Bado anatumia jina lake la utani la utotoni 'BB' na ni maarufu sana miongoni mwa mashabiki wake.
Ni mwanasiasa pekee wa Israel ambaye amehudumu mara sita kama mkuu wa nchi. Ameshinda chaguzi nyingi. Ndio maana wafuasi wanamwita 'Badshah Bibi'.
Hamas
Hamas ni mojawapo ya makundi kadhaa ya wapiganaji wa Kipalestina ambayo yanadhibiti Ukanda wa Gaza, eneo ambalo mara kwa mara hulitumia kukabiliana na Israel, taifa ambalo halilitambui.
Kundi hili kwa miaka kadhaa limekuwa likiendeleza upinzani dhidi ya Israel lakini mwaka 2023 limegonga vichwa vya habari kwa kutekeleza shambulizi baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo la Kiyahudi mnamo tarehe 7, Oktoba.
Shambulio hilo limesababisha vifo vya Waisraeli 1,400 huku maelfu ya Wapalestina wakifariki katika shambulio la kulipiza kisasi la Israel.
Imehaririwa na Lizzy Masinga