Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Muswada wa Fedha: Je Wabunge wa Kenya watamtii rais Ruto au kuheshimu maoni ya wananchi?
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
Licha ya zaidi ya mashirika 74 kati ya 84 yaliyoalikwa kutoa maoni mbele ya kamati ya bunge ya fedha na bajeti kuhusu muswada wa fedha wa mwaka wa 2023/2024 kupinga baadhi ya mapendekezo ya kuongeza kodi na tozo zinazopendekezwa na mswada huo,serikali ya rais William Ruto inashikilia kuwa lazima muswada huo upitishwe .
Rais hajakuwa tu akiwarai wabunge kuupitisha muswada huo ,ameonya kuwa atakuwa akingoja kwa hamu kuwaona wabunge watakaoukataa mswada huo usipitishwe siku ya Alhamisi .
‘Kila mjumbe ajulikane amepiga kura wapi.mimi nangojea mbunge anayepinga mswada unaolenga kuwapa vijana kazi.Nawangoja kupiga kura dhidi ya muswada huo unaoelnga kuleta ajira’ Rais ruto amesema mwishoni wiki katika kinachoonekana kama hatua inayolenga kuwashinikiza wabunge kuupitisha mswada huo licha ya pingamizi kuoka kwa wadau mbali mbali .
Naibu wake Rigathi Gachagua naye hajasaza maneno yake na ametishia kuwa wabunge wanaoupinga muswada huo wasiitishe fedha za kujenga barabara katika maeneo yao.
"Kuna uchochezi mwingi katika suala hili zima la Muswada wa Sheria ya Fedha. Nilikuwa Kitui(Mashariki mwa Kenya) juzi na mbunge wao alizungumza kuhusu kujitenga na watu wakapiga makofi. Halafu mara baada ya kuniambia wanahitaji barabara, anatarajia pesa za kujenga barabara zitatoka wapi?" Gachagua aliuliza.
Kulingana Gachagua , serikali inategemea mswada huo kuongeza mapato. Hivyo, wabunge wanapaswa kuunga mkono kikamilifu ikiwa wanatarajia kupata fedha za maendeleo.
"Baadhi yenu viongozi mnadanganya Wakenya, lakini fahamuni kwamba ikiwa mbunge wenu anapinga Mswada wa Fedha, hafai kuuliza barabara," alisema.
Ni hatua ambayo sasa inazua maswali kuhusu nia ya serikali hasa baada ya kuoneka wazi kuwa pendekezo la tozo ya nyumba kutoka kwa wafanyikazi nchini halijapokelewa vyema ilhali serikali inasisitiza lazima wafanyikazi watozwe asilimia tatu ya mishahara yao.
Wadadisi pia wanahoji kwa nini fedha zilitumiwa kuandaa vikao vya kukusanya maoni ya umma huku msimamo wa serikali ukiwa kwamba lazima mswada huo upitishwe bungeni.
Macho yote sasa yataangaziwa wabunge hasa wa muungano tawala wa Kenya Kwanza ambao serikali inawategemea kupitisha muswada huo huku wananchi ambao pato lao limebanwa na kuwa dogo ,wakitarajia kwamba wabunge wao ambao ndio waakilishi wao watawahurumia na kuukataa mswada huo.
Kinachoonekana kama vitisho kutokea upande wa serikali sasa kinawaweka wabunge wengi kati hali ya njia panda na itasubiriwa kuona kila mmoja wao atachukua uamuzi gani wakati wa kura kuhusu muswada huo wa fedha .Viongozi na wabunge wa upinzani tayari wameweka wazi msimamo wao wa kupinga mapendekezo katika mswada huo .
Makali ndani ya mapendekezo ya Muswada wa fedha
Wakenya watapatwa na mshtuko mkubwa iwapo mapendekezo katika Muswada wa Fedha wa 2023 yatapitishwa Bungeni jinsi Serikali inavyosisitiza.
Hazina ya Kitaifa imetoa mapendekezo ya kuchopoa malipo adimu ya wafanyikazi takriban milioni tatu wanaolipwa mishahara na kupunguza pakubwa mapato yao kando na kuongeza ushuru kwa mahitaji muhimu ambayo yanatarajiwa kuongeza gharama ya maisha.
Iwapo wabunge watapitisha mapendekezo hayo jinsi yalivyo, Wakenya wanaolipwa watashuhudia makato ya mapato yao yakipanda sana.
Kodi ya ujenzi wa nyumba inayopendekezwa ya asilimia tatu itapunguza kiasi cha fedha wanazopeleka nyumbani wafanyikazi baada ya makato menghine ya lazima .
Hili ni sawa na makato mengine kama vile viwango vipya Hazina ya malipo ya uzeeni (NSSF) na utekelezaji wa viwango vipya vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Hospitali (NHIF).
Ahadi zilizogeuka kuwa karaha
Utawala wa Kenya Kwanza uliahidi kabla ya kuingia madarakani kwamba utapunguza uharibifu wa fedha serikalini kwa kupunguza bajeti hiyo.
Serikali imetetea ushuru wa nyumba kuwa ni akiba, ambayo pamoja na kupunguza mapato ya mtu binafsi kwa muda mfupi, kuna faida kwa muda mrefu.
Pia inasema kwamba mtu binafsi ataweza kujiondoa kwenye mpango huo ikiwa hatahitimu kupata nyumba za bei nafuu.
Hazina ya kitaifa imependekeza ongezeko la Kodi ya Thamani ya bidhaa (VAT) kwenye bidhaa za petroli hadi kiwango cha kawaida cha asilimia 16 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia nane.
Wauzaji wa mafuta wameonya kuwa ongezeko la VAT inayotozwa kwa bidhaa za petroli huenda likasababisha lita moja ya petroli kuuzwa hadi zaidi ya Sh200.
Vyama mbalimbali vya wafanyakazi vimepinga mapendekezo katika Muswada wa Fedha na kutishia hatua kubwa. Watumishi wa umma walisema iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, itashuhudia makato yao ya mishahara yanaongezeka hadi zaidi ya asilimia 50 ya malipo yao.
Baadhi ya wafanyikazi wa umma mnamo Mei 29 waliandamana katika barabara za Nairobi, wakiandamana hadi Bungeni ambapo kupitia maafisa wa vyama vyao waliliomba Bunge kukataa baadhi ya mapendekezo katika Mswada huo.
Watumishi wa umma pia walionya kwamba watagoma iwapo Muswada huo utapitishwa.
Kwa nini serikali haishauriki?
Licha ya kuelewa haja ya serikali kutafuta mapato Zaidi kupitia kodi ,wadadsi wamehoji upuuzaji ambaao umetoka kwa upande war ais na maafisa wake wakuu kuhusu baadhi ya mapendekezo katika mswada huo.
Kikubwa kinachowasumbua wengi fikra sio tu kwamba hapajakuwa na maelezo ya kutosha kuhusu jinsi mpango wa ujenzi wa nyumba utakavyotekelezwa bali pia wakati huu sio mwafaka kwa serikali kulazimisha watu kusalimisha sehemu ya mapato yao.
Hali ya gharama ya juu ya Maisha imewaathiri watu wengi wakiwemo wafanyikazi na pendekezo la waakilishi wao lilikuwa kwa serikali kuboresha hali ya miundo msingi na mazingira mengine ili kufufua hali ya uchumi kwanza kabla ya kutoa mapendekezo kama haya.
Pia kuna tisho la wawekezaji walioko nchini kuondoka na wale wanaotaka kuja kuipeuka Kenya kwa sababu kutakuwa na ongezeko la gharama Zaidi kwao kuhudumu kenya.Kila mwajiri anatakiwa kuongeza asilimia tatu kwa kila mchango wa mfanyikazi ambaye anatozwa ada ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Waajiri wengi ,kuna uwezekano watalazimika kuwafuta kazi baadhi ya wafanyikazi wao ili kupunguza gharama .Hatua hiyo itaonyima serikali ushuru unaokatwa katika mapato(PAYE) hatua ambayo itakuwa kinyume na lengo la serikali la kuongeza makusanyo ya kodi .
Baadhi ya wadau pua wameishauri serikali kuutekeleza mpango wa nyumba za bei nafuu kwa hiari ya wanaozitaka nyumba hizo -ila rais na maafisa wake wameligeuza kuwa suala la ‘ubinafsi’ upande wa wafanyikazi wakisema wanaolipwa mishahara hawataki kuwasaidia wasio na ajira wapate kazi ili wajitegemee. Kinachongojewa na wengi ni hatua ya wabunge siku ya Alhamisi wakati wa mjadala na baadaye kura kuhusu mswada huo .