Jinsi vijana wasio na kazi China wanavyojifanya wameajiriwa

Shui Zhou hulipa ili aende ofisini kila siku
Maelezo ya picha, Shui Zhou hulipa ili aende ofisini kila siku
    • Author, Sylvia Chang
    • Nafasi, BBC News Chinese, Hong Kong
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Hakuna mtu anayependa kufanya kazi bila kulipwa mshahara au, mbaya zaidi, kuhitaji kulipa ili upate kazi.

Ni jambo lisilo la kawaida.

Mtu kulipa ili aweze "kuonekana" kana kwamba anafanya kazi.

Lakini hiyo ndiyo hali halisi inayojitokeza kwa idadi inayoongezeka ya vijana wasio na ajira nchini China.

Katika mazingira ambako uchumi unadorora na nafasi za kazi ni adimu, vijana wengi waliohitimu vyuo wanajikuta wakiwa hawana kazi wala mwelekeo.

Badala ya kukaa nyumbani wakikabiliwa na shinikizo la kijamii na kifamilia, baadhi yao sasa wanachagua kutumia fedha zao kulipia huduma ya kuingia kwenye ofisi za kuigiza kazi maeneo yanayoitwa kwa mzaha "Makampuni ya kuigiza kazi."

Naweza kukaa ofisini kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane. Sio kwa sababu kuna kazi nyingi bali kwa sababu najihisi mtu wa maana nikiwa hapa.

Maneno haya ni ya Shui Zhou, kijana mwenye umri wa miaka 30 kutoka jiji la Dongguan, china.

Baada ya ndoto yake ya biashara ya chakula kufa mapema mwaka 2024, Zhou alijikuta hana pa kwenda kila siku.

Hakukuwa na kazi. Hakukuwa na matarajio. Kulikuwa na ukimya, shinikizo kutoka kwa familia, na hofu isiyoisha.

Kisha akagundua kitu kwenye mtandao wa kijamii Xiaohongshu: ofisi ya kuigiza kazi.

Ndiyo. Kulipa fedha ili ukae ofisini kana kwamba unafanya kazi.

"Nilianza kulipa yuan 30 sawia na dola 4.20 kwa siku.

Alipojiunga na kampuni hiyo ambayo ni kilomita 114 kutoka kaskazini mwa HongKong, alikutana na wenzake watano ambao pia wanashughuli hiyo.

''Nina furaha,'' anasema Bwana Zhou.

''Ni kama tunafanya kazi kama kikundi''.

Pia unaweza kusoma:

Huduma hizi zimeenea kwa kasi katika miji mikubwa kama Shenzhen, Shanghai, Nanjing, Wuhan, Chengdu na Kunming.

Ofisi hizi hujengwa kwa ufanisi mkubwa, zikifanana kabisa na maeneo halisi ya kazi, zenye kompyuta, intaneti, vyumba vya mikutano na hata sehemu za mapumziko na vinywaji.

Lakini tofauti ni kwamba hapa, hakuna mwajiri ni vijana waliokata tamaa wanaojaribu kuonyesha kuwa hawajapotea kabisa.

Wengine huutumia muda huo kutafuta kazi mtandaoni, kuandika miradi ya biashara, au hata kuanzisha shughuli zao binafsi.

Kwa ada ya kila siku kati ya yuan 30 na 50, huduma hii wakati mwingine hujumuisha chakula cha mchana na vinywaji.

Kwa wengi, huu si mzaha bali njia ya kujipa nidhamu, kutuliza hofu ya wazazi, au kudanganya vyuo kuwa wako kwenye mafunzo ya kazi.

wanaweza kuketi tu, au kutumia kompyuta iliyotolewa kusaka kazi
Maelezo ya picha, wanaweza kuketi tu, au kutumia kompyuta iliyotolewa kusaka kazi

Katikati ya kukata tamaa, vijana watafuta aana

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dkt. Christian Yao, mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Victoria, New Zealand, anaona kuwa hali hii inaakisi changamoto kubwa katika uchumi wa China.

"Hali ya kuigiza kufanya kazi sasa imeenea," asema.

"Mageuzi ya kiuchumi na kutokuwepo kwa uwiano kati ya elimu na ajira yamewafanya vijana kutafuta maeneo ya mpito ya kutafakari mustakabali wao."

Kwa Zhou, mazingira ya ofisi yamempa utulivu na mwelekeo wa kibinafsi.

Ameshakuwa hapo kwa zaidi ya miezi mitatu.

Wazazi wake, ambao hapo awali walihofia hali yake, sasa wanaridhika kuona picha zake akiwa katika 'kazi.'

Ingawa washiriki wana uhuru wa kufika na kuondoka wanavyotaka, Zhou huwasili kati ya saa mbili na tatu asubuhi, na mara nyingi huondoka usiku baada ya meneja kuondoka.

"Tumejenga urafiki hapa. Tukiona mtu ana kazi kama kutuma maombi ya ajira tunamwachia afanye kazi. Lakini muda wa mapumziko tunacheka, tunacheza, na hata kula pamoja jioni."

Anasema maisha haya ya 'kazi ya bandia' yamemfanya ajihisi vizuri zaidi kuliko alipokuwa nyumbani peke yake.

Xiaowen Tang, msichana wa miaka 23 kutoka Shanghai, alikodisha meza katika ofisi ya kuigiza kazi kwa mwezi mzima.

Baada ya kuhitimu mwaka jana, chuo chake kilimwambia lazima awasilishe ushahidi wa kutarajali au kazi la sivyo hatapewa cheti cha stashahada.

"Nilipiga picha nikiwa kwenye kampuni hii ya kazi bandia, nikazituma chuoni kama uthibitisho. Ukweli ni kwamba, nilikuwa naandika riwaya za mtandaoni kupata hela ya vocha tu," anasema kwa kucheka.

Tang anasema ukweli mchungu: "Kama utaigiza, igiza mpaka mwisho."

Uongo Unaotafuta Heshima?

Katika mji huo huo wa Dongguan, mmiliki wa kampuni hiyo ya kuigiza kazi, anayefahamika kwa jina bandia Feiyu, anasema:

"Kile ninachouza siyo tu kiti cha kazi ni heshima. Ni hadhi ya kutokujiona kuwa mtu asiye na maana."

Feiyu mwenyewe alipitia ukosefu wa ajira baada ya biashara yake ya rejareja kufungwa wakati wa janga la Covid-19. Alikumbwa na msongo wa mawazo, akahisi hana nguvu ya kubadili hali yake.

Dkt. Biao Xiang, mkurugenzi wa Taasisi ya Max Planck ya Anthropolojia ya Kijamii nchini Ujerumani, anasema kwamba mtindo wa China wa kujifanya kufanya kazi unatokana na "hisia ya kuchanganyikiwa na kutokuwa na uwezo" kuhusu ukosefu wa nafasi za kazi.

"Kujifanya kufanya kazi ni ganda ambalo vijana hujitafutia wenyewe, na kujenga umbali kidogo kutoka kwa jamii ya kawaida na kujipa nafasi kidogo."

Katika mji huo huo wa Dongguan, mmiliki wa kampuni hiyo ya kuigiza kazi, anayefahamika kwa jina ambalo sio halisi Feiyu, anasema:

"Kile ninachouza siyo tu kiti cha kazi ni heshima. Ni hadhi ya kutokujiona kuwa mtu asiye na maana."

Feiyu mwenyewe alipitia ukosefu wa ajira baada ya biashara yake ya rejareja kufungwa wakati wa janga la Covid-19.

Alikumbwa na msongo wa mawazo, akahisi hana nguvu ya kubadili hali yake.

Lakini Aprili mwaka huu, alianza kutangaza kampuni yake ya "kuigiza kazi." Ndani ya mwezi mmoja, ofisi ilijaa.

Kwa sasa, mtu yeyote anayetaka kujiunga ni lazima aombe nafasi.

Anakadiria kuwa asilimia 40 ya wateja wake ni wahitimu wa hivi karibuni wanaokuja kupiga picha kama ushahidi wa mafunzo ya kazi.

Wengine huja kupunguza shinikizo kutoka kwa familia zao.

Asilimia 60 zilizobaki ni wafanyakazi huru wakiwemo waandishi wa kidijitali, wataalamu wa teknolojia, na hata watu wanaofanya kazi kwa makampuni ya mtandaoni kama "digital nomads."

Vijana hao wana umri kati ya 30 huku aliye mdogo zaidi miaka 25.

Feiyu, mmiliki wa Kampuni ya kuiga kazi anasema anawauzia watu "heshima"
Maelezo ya picha, Feiyu, mmiliki wa Kampuni ya kuiga kazi anasema anawauzia watu "heshima"

Feiyu anasema hana uhakika kama mradi huu utaleta faida ya kifedha, lakini kwake ni zaidi ya biashara ni jaribio la kijamii.

"Inatumia uongo ili kudumisha heshima, lakini inaruhusu baadhi ya watu kupata ukweli," anasema. "Ikiwa tutawasaidia tu watumiaji kurefusha ujuzi wao wa kuigiza tunahusika katika udanganyifu wa upole.

"Ni kwa kuwasaidia kubadilisha mahali pao pa kazi bandia kuwa mahali pa kuanzia ndipo jaribio hili la kijamii linaweza kutimiza ahadi yake."

Na kwa Zhou, hiyo ni hatua ya kwanza.

"Nikiwa hapa, najifunza kutumia zana za akili mnemba. Nimeona kampuni nyingi sasa zinaajiri wale wanaojua Midjourney, ChatGPT, au Copilot," anasema kwa matumaini.

"Nimeamua kutokuwa tu mtu wa kuigiza. Nimeanza kujenga maisha mapya."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid