Hakuna siku ya kupumzika: Maisha magumu ya wafanyakazi wa nyumbani huko Qatar

g

Rekodi ya haki za binadamu inachunguzwa huku Kombe la Dunia likiendelea katika mji mkuu Doha. Mengi yameandikwa kuhusu jinsi walivyotendewa wafanyakazi wahamiaji waliojenga viwanja na hoteli , lakini ni vipi kuhusu wafanyakazi wa nyumbani wanaowafanyia kazi watawala wa Qatar? Mwandishi wa BBC wa masuala ya jinsia na utambulisho Megha Mohan amezungumza na wafanyakazi wa nyumbani wawili kuhusu maisha ya kufanya kazi saa nyingi bila kupewa siku za mapumziko

 "Ninafahamu uzoefu wangu sio uzoefu wa kawaida ," Althea (sio jina lake halisi) anaiambia BBC kwa njia ya simu kutoka kwenye eneo la chini la makazi ya familia ya kifalme ya Qatar ya Al Thani.

 Althea ni mchangamfu, na anapenda kujipamba, akiwa na nywele ndefu na hujipaka vipodozi usoni (make-up). Hajavaa sare wakati tunazungumza lakini anasema amevaa sketi ndefu na blauzi na viatu vya michezo vya Nike . Asingeweza kuvaa hizo nguo hizi nyumbani kwao Ufilipino. Ni vigumu kupata mshahara nyumbani ndio uliomleta hapa.

Althea anaishi katika nyumba moja kubwa na wafanyakazi wengine wa nyumbani kutoka Ufilipino , ambao walinisalimia na kujiunga na mazungumzo ya simu.

 Wanavyumba vyao vya kulala na jiko lao binafsi . Wafanyakazi wa nyumbani, au khadama, Althea hutazama TikTok na Facebook wakiomba chakula , na kuwaomba watu wawanusuru, hawana bahati.

 "Ninaona video hizo kwenye mtandao kila wakati, ndio maana ninahisi kuwa nina bahati sana ," anasema. "kwangu mimi kila siku nahisi kama hadithi ."

 Simu ya iPhone ya Althea ni zawadi aliyoipata kutoka kwa waajiri wake. Pia wamempatia nguo za kifahari, vipuli na viatu, na marupurupu zaidi ya pesa Qatari 500 (£115).

Kwa ujumla, amefanya kazi katika maeneo manne ya Ufalme, yote ya familia ya ufalme.

" Ni kasri nne za Cinderella ," anasema, akielezea vyumba vya majumba hayo kama vya kifahari na kuta zilizopakwa na kasri hizo zilizozingirwa na maua yenye harufu nzuri za kuvutia , na nyati zilizokatwa vyema. Kuna bustani zilizotengenezwa vizuri, vidimbwi vya uogelea, na viwanja vya tenisi.

Siku ya kazi katika makazi ya ufalme kwa ujumla huanza saa 12.30 asubuhi, wakati wahudumu wanapoandaa kifungua kinywa kwa ajili ya familia.

 Althea hula chakula mara baada ya familia kumaliza kula . Baada ya hapo husafisha vyumba na kuandaa maeneo kwa ajili ya chakula cha mchana.

"Ni kazi rahisi kwasababu pale tuko wengi," Althea anasema

 Wakishamaliza kula mlo wa mchana, wafanyakazi hupumzika katika makazi yao kati ya saa tisa alasiri na saa kumi na mbili jioni, halafu baada ya hapo huandaa chakula cha jioni.

 Baada ya chakula cha jioni Althea huwa amemaliza kazi, na anakuwa huru kuondoka iwapo anataka

Haki za wafanyakazi wa nyumbani

  • Nchini nyingi za ghuba hutumia mfumo wa "kafala" , ambao huwazuia wafanyakazi wa kigeni kubadilisha kazi au kuondoka nchini bila ruhusa ya muajiri , na unamruhusu muajiri kuzuilia paspoti za wafanyakazi
  • Qatar ilichukua hatua ya kubadilisha hili baada ya kushinda haki ya kupokea Kombe la Dunia la mwaka 2022 na kuchunguzwa kimataifa
  • Katika mwaka 2017 ilianzisha sheria ya wafanyakazi, ambayo kinadharia huweka ukomo wa saa 10 za kazi kwa siku , na hutoa muda wa mapumziko kila siku , siku moja ya mapumziko kila wiki na malipo ya likizo
  • Katika mwaka 2020 pia ilianzisha kima cha chini cha mshahara na kuwapatia wafanyakazi haki ya kubadilisha kazi au kuondoka nchini humo bila kuomba ruhusa
  • Hatahivyo Shirika la haki za binadamu, Amnesty International linasema sheria hizi hazifuatwi kila mara na watu hutumikishwa kazi kupita kiasi, kuna ukosefu wa mapumziko , na unyanyasaji unaendelea

Mary Grace Morales, muajiri aliyeko Manila anayewakutanisha wafanyakazi wa Ufilipino na watu muhimu (VIP) katika nchi za Ghuba , Emir wa Qatar ni mteja muhimu – hususan ni wakati msaada wa ziada ulipohitajika katika kuandaa Kombe la Dunia. Karibu vyumba vyote vya wageni vimechukuliwa na wageni muhimu (VIP) ambao wanahitaji huduma, anasema Bi Morales.

Wafanyakazi wa nyumbani huwa katika makundi matano katika Nyumba ya Al Thani: wafanyakazi wa usafi, wahudumu wa chakula, walezi (waliokuwa manesi zamani), wapishi na "manesi wa kike" kwa ajili ya kuwaendesha wanawake wa familia za ufalme.

"Wanawake wanaopelekwa kufanya kazi katika familia ya ufalme ya Qatari waa umri wa kuanzia miaka 24 na 35 na ni warembo sana ," anasema Bi Morales.

Alisita kidogo kuangalia kwenye skrini, nikimtazama kutoka makao makuu ya BBC mjini London. "Warembo zaidi kuliko wewe," ananiambia, huku akitabasamu.

G
Maelezo ya picha, Mary Grace Morales anasema wafanyakazi wa uflme wa Qatari lazima wawe wameelimika na "warembo sana"
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Lazima wawe vijana kwasababu familia ya ufalme Qatari inahitaji watu wenye nguvu sana na afya nzuri ambao wanaweza kumudu mazingira yenye shughuli nyingi ya kasri.

"Na wanaoomba kazi lazima wawe na sura nzuri – warembo sana sana," alisisitiza.

Kufanya kazi kama msaidizi binafsi katika familia ya ufalme ni lazima uwe umehitimu mafunzo ya chuo kikuu na uwe unazungumza lugha ya kiingereza, Bi Morales ananiambia , huku wafanyakazi wa usafi wakiwa ni lazima wawe wamemaliza masomo ya shule ya sekondari

Anasema amewapeleka mamia ya wafanyakazi kwenye kasri ya kifalme kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita . Huwa wanarefusha mikataba yao.

Mmoja wao ni Gladys (sio jina lake halisi ), ambaye anamfanyia kazi mmoja wa watu muhimu (VIP)katika familia ya ufalme ya Qatar.

Katika mazungumzo mafupi ya mtandao na BBC, wakati muajiri wake alkiwa amelala, anasema hufanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni kila siku .

Hufanya usafi, husaidia kuandaa chakula, na kuwalea watoto. Hula mabaki, na anasema hajawahi kupata siku hata moja ya kupumzika tangu aajiriwe miezi 18 iliyopita.

"Madam ni mtu mbaya," Gladys anasema kuhusu muajiri wake. "Huwa ananifokea kila siku ."

 Gladys hawezi kuipata paspoti yake , lakini anahisi mwenye bahati, kwasababu ana simu yake. Hataki kuondoka au kuomba ubalozi wa Ufilipino nchini Qatar umsaidie kwasababu ana umri wa miaka zaidi ya 40 na anafikiria kuwa hawezi kupata kazi bora kwa sasa.

Hupata mshahara wa 1,500 pesa za Qatari kwa siku (chini kidogo ya £350) na hutuma pesa zote nyumbani.

Sababu nyingine inayomfanya Gladys ahisi kuwa mwenye bahati ni kwamba hateswi kimwili. Anasema anawafahamu wafanyakazi wengine kadhaa wa nyumbani nchini Qatar ambao hupigwa.

G

Joanna Concepcion wa shirika la wahamiaji la kimataifa - Migrante International, ambalo huwasaidia wafanyakazi Wafilipino wanaofanya kazi katika mataifa ya kigeni, anasema ana matumaini kuwa ushahidi wa Althea wa kufanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani wa familia ya ufalme ni wa kweli, lakini anaongeza : "Ni vigumu kuweza kujua hilo wakati bado yuko Qatar na akifanya katika familia yenye mamlaka ya aina hiyo."

 Baadhi ya wafanyakazi wamelalamika baada ya kuondoka nchini humo, mwaka 2019 wafanyakazi watatu Muingereza na Wamarekani wawili – mlinzi , mkufunzi binafsi na mwalimu wa kibinafsi – walimshitaki dada yake emir wa Qatar, Sheikha al Mayassa bint Hamad bin Khalifa.

 Al Thani na mume wake, wanadai kwamba wamekuwa wakilazimishwa kufanya kazi masaa mengi bila malipo ya ziada. Familia hiyo ilikanusha madai hayo na wakadai kinga ya kidiplomasia kwani wawili hao walikuwa wakifanya kazi New York.

Bi Concepcion anasema wafanyakazi wa nyumbani wanaofanya kazi katika nchi za ng’ambo wakati mwingine huwa kimya kuhusu hali mbaya za kazi kwasababu ya vipaumbele vyao ili waendelee kupata pesa kwa ajili ya familia zao.

 Lakini wakati wale wa mataifa ya Ghuba wanapohisi kuwa na ujasiri wa kutosha wa kuongea , anasema, wakati mwingine hutaja unyanyasaji mbaya waliofanyiwa. Mwnamke mmoja alisema muajiri wake alikuwa akimsukuma ndani ya choo na kumnyima chakula a maji alipokuwa na njaa.

"Kuripoti, kutatua kesi za unyanyasaji na mateso, ukosefu wa usalama na afya na ukosefu wa makazi bora ya kuishi huwa ni changamoto ," anasema mkurugeni wa Shirika la Wafanyakazi la Kimataifa (ILO) wa mataifa ya kiarabu , Ruba Jaradat.

 ILO inasema inashirikiana na Qatar kutekeleza sheria mpya ya kazi, ingawa hili limesalia kuwa ‘’changamoto".

Althea, Katika mazingira yake ya ufalme, anasema ni mwenye furaha licha ya kutopewqa siku moja ya mapumziko kwa wiki.

Anapokwenda kulala humtumia ujumbe mmoja wa ndugu zake au wazazi wake nchini Ufilipino. Mara kwa mara huwa anakumbuka sana nyumbani kwao.

Hatahivyo, bado yeye ni chanzo cha pato kwa familia yake.

"Nisingeisaidia familia yangu bila kazi ," anasema.

BBC iliitaka familia ya ufalme ya Qatari na ubalozi wa Qatari mjini London kutoa maoni yake, lakini haikupata jibu.