'Wanaume hawana hisia" na habari zingine potofu ambazo hatuelewi kuhusu "uanaume'

g

Chanzo cha picha, Getty/ SEGUN OGUNFEYITIMI

Muda wa kusoma: Dakika 8

Ni kawaida katika jamii zetu za Kiafrika kwa watoto kukua katika familia ambazo wazazi hawaonyeshi hisia zao waziwazi. Hisia ya hasira mara nyingi, ndiyo inayojitokeza hasa wanapoonyeshwa kukerwa na tabia fulani ya mtoto au mambo fulani katika jamii.

Mara nyingi "unapodadisi " mazungumzo ya faragha ya wanawake wenye umri mdogo leo kwenye mitandao kama vile Instagram na Tiktok , yanaweza kuleta wasiwasi: mwanaume mara nyingi huchukuliwa kama mtu asiyepaswa kuonyesha hisia zake kama vile kusikitika au kulia kwani jamii inamtegemea awe mtu jasiri asiyeonyesha mapungufu yakehata kama anaumia, au kuumizwa na anapoonyesha hisia zake basi huambiwa ana tatizo hapaswi kuwa hivyo, na mara nyingine huambiwa amuone daktari wa akili.

Ingawa inaweza kuonekana juu juu kuwa ni maoni haya ni kama mzaha kwenye mitandao ya kijamii, bila shaka yanaonyesha shida kubwa inayohusiana na mahusiano yao na hisia zao wenyewe, npamoja na wengine, katika uhusiano ambao unahitaji kiwango cha kujieleza kwa kuonyesha hisia zao.

Kuna imani iliyoenea, ambayo bado imekita mizizi katika utamaduni wetu, kwamba wanaume hawaonyeshi hisia zao, kwamba "hawana hisia." Wengi wanaamini kuwa ni "aibu" kwa mwanamume kulalamika juu ya wasiwasi wake, kuelezea udhaifu wake, au kuelezea hisia zake, kwasababu wanaume "hawalii." Lakini mawazo haya yanaweza kuwa hatari na kuwa na athari za muda mrefu kwa afya ya akili na kimwili ya wanaume.

Je, wanaume kweli wanakabiliwa na "ukosefu wa kihisia," au ni matokeo ya matarajio ya kijamii yaliyowekwa kwao?

Unaweza pia kusoma:

1- "Wanaume hawana hisia"

Moja ya maoni potofu ya kawaida katika jamii zetu ni kwamba wanaume "kawaida" hawana hisia , au hawawezi hisia za kina. Wazo hili linaloshikiliwa sana linachukuliwa kama ukweli wa kibaolojia, kana kwamba wanaume wana uwezo wa kujieleza au hata kuhisi.

Mwanasaikolojia Hadi Abi Al-Mona aliiambia BBC kuwa, "Mojawapo ya dhana potofu katika jamii zetu ni imani kwamba kuelezea hisia ni tabia ya '', kana kwamba hisia zinahusishwa na uanauke. Kinyume chake, kuzuia hisia au kuvumilia maumivu kimya huonekana kama ushahidi wa 'uanaume.'"

Uhusiano huu kati ya kuzuwiwa kwa mihemko na "uanaume" hauathiri si tu maisha ya kihisia ya wanaume, bali pia afya yao ya akili. Wengi wananyimwa fursa ya kuishi kwa usawa na amani ya ndani, kwa kuogopa kwamba udhaifu wao au usikivu utaeleweka vibaya.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwanasaikolojia Hadi Abi Al-Muna aliiambia BBC : "Mara nyingi inasemekana kwamba wanaume hawana hisia za kutosha, au kwamba hawawezi kuhisi kwa kina, na kwa hivyo hawaonyeshi hisia zao kwa njia sawa na wanawake. Inafikiriwa kuwa hii ni tabia ya asili, kitu ambacho wanaume huzaliwa nacho. Lakini ukweli ni kwamba wanadamu wote, wanaume na wanawake, ni sawa katika uwezo wao wa kuhisi na kina cha hisia zao."

Kwa hiyo nini kinaendelea? Kulingana na Abi Al-Mona, wanaume, hasa katika jamii zetu, "hujifunza tangu wakiwa wadogo kutoeleza hisia zao kwa maneno." Elimu hii haiondoi hisia, lakini badala yake huzika au kuzielekeza upya. Mwanasaikolojia anaeleza kuwa hisia hizi "hazipotei, bali hubadilika na kujidhihirisha kwa njia zingine, kama vile ukimya, hasira, au kuzamisha mambo kupita kiasi katika kazi."

Tulipomuuliza ikiwa kuwa na shughuli nyingi na kazi kulitoa utulivu wa muda, alijibu, "Kwa muda mfupi, ndio. Lakini kubadilisha hisia za msingi na hisia au vitendo vingine huzuia mtu huyo kutambua, kuchambua, kukiri, kuelewa, na kuelezea hisia zake—yaani, anaziepuka kabisa."

Abi Al-Mona anasisitiza kwamba kuepuka huku "sio suluhisho la muda mrefu, na haichangii kushughulikia hisia au kutatua tatizo la msingi."

h

Chanzo cha picha, Getty Images

2- "Kuzungumza hakutasuluhisha shida"

Hadi Abi Al-Mona anabainisha kuwa mojawapo ya mawazo ya kawaida anayosikia kutoka kwa wanaume wanaoepuka kutafuta tiba ni kwamba "kuzungumza juu ya tatizo haina thamani kwa sababu haisaidii kulitatua."

Lakini anaelezea kuwa kuzungumza kuhusu shida ndio hasa kiini cha tiba ya kisaikolojia. Anasema, "Tiba ya kisaikolojia inaruhusu mtu kuzungumza juu ya shida na hisia zake na kuelewa kinachoendelea kwake, hata ikiwa hatapata suluhisho la haraka. Hii inatoa ufahamu wa jinsi ya kukabiliana na kudhibiti hisia zao."

Anaonyesha jambo muhimu ambalo mara nyingi hupuuzwa: "Mtu anapotaja shida zake, humpa nguvu kidogo."

Kwa upande wake, mwanasaikolojia Gisele Saliba anaamini kwamba kusita kwa wanaume kutafuta tiba ya kisaikolojia kunahusishwa kwa karibu na ubaguzi ulioingizwa ndani yao tangu wakiwa na umri mdogo. Aliiambia BBC : "Wanaume wanaoamua kutafuta matibabu ya kisaikolojia mara nyingi husita sana, wakiamini kuwa ni ishara ya udhaifu au hupunguza uanaume wao."

Anaelezea, "Daima wanasisitiza kwamba hakuna mtu anayepaswa kujua kuhusu hilo. Hii ni kwasababu wamesikia tangu wakiwa na umri mdogo mambo kama, 'Wewe ni mwanamume, unapaswa kuwa na uwezo wa kufanya kila kitu peke yako, au kutatua kila kitu bila msaada.'"

Anaongeza: "Kuepuka kuelezea hisia ni kawaida sana kati ya wanaume, kwasababu wakiwa watoto waliambiwa kuwa kulia au kuonyesha mafadhaiko, hofu, au usumbufu haifai kwa wanaume na kwamba wanaume hawafanyi hivyo."

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa mpira wa miguu mara nyingi humdhihaki mchezaji wa timu pinzani anayelia kama "dhaifu" na "kihisia."

3- "Muda utasuluhisha kila kitu."

Mara nyingi tumesikia methali na nyimbo maarufu katika lugha nyingi zikisema, "Wakati hurekebisha kila kitu" au "Wakati hutufanya tusahau." Hata hivyo, utafiti umethibitisha mara kwa mara kwamba imani hii maarufu haina msingi wa kisayansi.

Hadi Abi Al-Mona anaeleza kuwa kupuuza tatizo au kujiepusha kulijadili hakuchangii utatuzi wake, bali husababisha kuongezeka kwake kwa muda. Anasema, "Kuepuka kuzungumza juu ya kitu hufanya shida kukua. Badala ya kutoweka, inakuwa ngumu zaidi."

Anatoa mfano wa kielelezo, akisema, "Meno yetu sio lazima yawe mashimo ili tuanze kuyasafisha. Ukweli ni kwamba, tunazisafisha ili yasipate mashimo, au shida inazidi kuwa mbaya baadaye."

Anasisitiza umuhimu wa kuingilia kati mapema, akisema, "Kadiri uingiliaji kati unavyotokea, ndivyo tatizo linavyokuwa kali, na kuna uwezekano mdogo wa kuenea katika nyanja zingine za maisha ya mtu huyo."

4- "Wanaume wanajisimamia bila msaada."

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Abi Al-Mona anasema kwamba moja ya sababu kuu za ni kwanini wanaume wanasita kutafuta msaada wa kisaikolojia ni kwamba hawajajifunza kuwa kuomba msaada ni kawaida.

Anaeleza kwamba mwanamume anapochukua hatua ya kuomba msaada, "anaaibishwa na kuonekana kuwa dhaifu," kwasababu jamii inahusisha dhana ya "uanaume" na uhuru kamili na kutohitaji mtu yeyote.

Anasema, "Dhana potofu ya mtu mwenye nguvu, ambaye anaweza kutatua kila kitu peke yake na ambaye hahitaji au kuomba msaada, bado inahusishwa kijamii na wazo la uanaume na nguvu. Kinyume chake, mwanamume anayeomba msaada au kueleza hisia zake anatazamwa kuwa sio mwanamume wa kutosha."

Viwango hivi vya uongo, kama Abi Al-Mona anavyoonyesha, vinazua maswali mengi kuhusu athari za matarajio yasiyo ya maana ya kijamii kwa afya ya akili ya wanaume na uwezo wao wa kuingiliana wao wenyewe na wengine kwa njia ya uaminifu na ya starehe.

Unaweza pia kusoma:

5- "Mtu aliyefanikiwa huwa thabiti kila wakati."

Hadi Abi Al-Mona anasisitiza kwamba mafanikio ya kweli hayapimwi kwa uthabiti wa nje au nguvu za nje, lakini badala ya uwezo wa kufikia usawa wa ndani unaomwezesha mtu kuelewa na kukabiliana na hisia na matatizo yake kwa njia nzuri.

Anaongeza kuwa ufahamu wa hisia na uwezo wa kuzidhibiti ndio humpa mtu uwezo bora wa maendeleo thabiti, wakati usumbufu wowote wa ndani ambao haujatibiwa katika kushughulikia mawazo na hisia unaweza kuzuia maendeleo yao ya kibinafsi sawa na ya kitaaluma

Kwa upande wake, mwanasaikolojia Gisele Saliba anasema kwamba baadhi ya watu wanaotafuta kujidhibiti kabisa na kujaribu kuwa na busara kila wakati wanaonyesha malezi kulingana na dhana ya potofu kwamba hisia ni hasi.

Anasema, "Kuna wale ambao wanaamini wanapaswa kuzingatia tu kazi na kuzuwia hisia zozote. Watu hawa mara nyingi hulelewa juu ya wazo kwamba hisia ni udhaifu, na kwamba kujishughulisha na hisia sio mantiki au haina maana.

Je, matarajio ya kijamii huongeza mateso ya wanaume?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Wataalam wa afya ya akili wanakubali kwamba ukuaji wa ugonjwa wowote wa kisaikolojia au ugonjwa wa akili hausababishwi na sababu moja pekee, bali matukio ya mambo makuu matatu: muundo wa kibaolojia, asili ya kisaikolojia, na hali ya kijamii inayozunguka mtu.

Katika muktadha huu, Gisele Saliba anasisitiza kwamba hisia zilizokandamizwa na udhibiti wa kijamii usio na mantiki uliowekwa kwa wanaume unaweza kuwafanya wawe katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya afya ya akili.

Anasema kuna "shinikizo nyingi zinazowekwa kwa wanaume na jamii, ikiwa ni pamoja na kwamba hawapaswi kueleza hisia zao, kuathiriwa, au kuzungumza juu yake."

Shinikizo hizi sio tu hubadilisha uzoefu wa kisaikolojia, lakini pia huathiri asili ya dalili ambazo wanaume hupata. Anaelezea, "Tunafikiri kwamba unyogovu, kwa mfano, unajidhihirisha kwa kila mtu kama huzuni na kujiondoa. Lakini kwa wanaume wengi, inajidhihirisha kama hasira ya mara kwa mara, kwa sababu kuelezea huzuni hairuhusiwi kwa wanaume."

Anaongeza kuwa viwango vya kujiua ni vya juu zaidi kati ya wanaume kuliko wanawake, akisema, "Kwa mtu kufikia hatua hii inamaanisha kuwa amefikia hali ngumu sana ya kisaikolojia."

Anaelezea nambari hizi kwa kusema, "Wanawake kawaida hawana shida kuzungumza juu ya shida na hisia zao, wakati wanaume mara nyingi huweka kila kitu kwao wenyewe na kukandamiza maumivu na hisia."

g

Chanzo cha picha, Getty Images

"Wewe ni mtu ambaye hawezi kulia

Mwanasaikolojia Gisele Saliba anabainisha kuwa viwango vya matumizi ya dawa za kulevya na uraibu wa pombe ni vya juu zaidi kati ya wanaume kuliko wanawake, na kwamba ugonjwa wa utu usio wa kijamii, unaojulikana na mifumo ya tabia ambayo inapuuza haki za wengine na kutegemea udanganyifu,upotofu, na uzembe, umeenea zaidi miongoni mwa wanaume.

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza, shida hii inahusishwa na sababu za kibaolojia na maumbile, pamoja na kiwewe cha utotoni, kama vile kufichuliwa kwa kupuuzwa, unyanyasaji wa kihisia.

Abi Al-Mona anatoa mfano wa rheumatism na fibromyalgia, ambapo matatizo ya kihisia, anasema, huchangia kuzidishwa kwa dalili. Anasema, "Kusonga kwa mwili, kama vile kutembea au kufanya mazoezi, huchangia sana kuboresha afya ya akili. Ukandamizaji na mafadhaiko, hata hivyo, unaweza kusababisha maumivu halisi ya kimwili, kama vile maumivu ya kichwa au shinikizo la damu."

Saliba anaonya dhidi ya kudharau mafadhaiko, akisema, "Katika miaka ya hivi karibuni, tumeona ongezeko la malalamiko ya kimwili ambayo hayana maelezo ya kibaiolojia. Katika visa hivi, tunasahau kuwa haimaanishi kuwa tuko sawa, lakini badala yake mafadhaiko au wasiwasi umesababisha shida halisi ya mwili.

Anaeleza kuwa, "Uchunguzi umeonyesha kuwa mfadhaiko unaweza kudhoofisha kinga, kuathiri afya ya moyo, kusababisha ukosefu wa usingizi, au hata matatizo ya kula, ambayo yote yanahusishwa na kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na hisia zetu kwa njia nzuri."

Saliba anahitimisha kwa ushauri kwa wazazi, hasa wale wanaolea watoto wa kiume: "Sentensi kama 'Wewe ni mwanamume, huwezi kulia' inatosha kumfanya mtoto ashindwe kukabiliana na hisia zake kwa maisha yake yote."

Anaongeza: "Badala ya kumfanya kuwa mtu mwenye nguvu, kama tunavyofikiria, tumepanda ndani yake shida kubwa ya kihisia na ukosefu wa faraja ya ndani."

Hatimaye anasisitiza: "Hatuwezi kumzuia mtu yeyote kuhisi. Tunachofanya ni kufanya kazi ya kuelewa na kushughulikia hisia hizi kuwa ngumu zaidi."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi