Mzozo wa DRC: Congo yaishtaki Rwanda katika Mahakama ya Afrika

Muda wa kusoma: Dakika 4

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC imewasilisha kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kwa madai ya ukiukwaji wa haki.

Tuhuma za Congo dhidi ya Rwanda zinahusiana na mzozo uliokumba eneo la mashariki mwa nchi hiyo tangu 2021, ambako vikosi vyake vimekuwa vikabiliana na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda- imepinga hili.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani mwaka 2023 lakini itaanza kusikilizwa rasmi hapo kesho Jumatano na Alhamisi ambapo hoja za pande hizo mbili kuhusu mamlaka ya mahakama hiyo na uwezo wake wa kusikiliza ombi iliyowasilishwa na DRC itasikilizwa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC, kukutana jijini Dar es Salaam Tanzania, kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha Tanzania, Congo inadai kuwa mzozo huo umesababisha mauaji, uvamizi wa maeneo yake, na watu 520,000 kulazimika kuyahama makazi yao, kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu na uharibifu wa shule na hivyo kusababisha watoto 20,000 kukosa elimu.

DRC aidha inalalamikia uharibifu wa miundombinu mbinu yake vile vifaa vya kusambaza umeme, uporaji na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na vituo vya afya.

Pia inadai kuwa Rwanda inawahifadhi watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa, na ambao mahakama zake zimetoa hati za kimataifa za kukamatwa kwao.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekwama vitani, wanamgambo wa kundi la M23 wamekuwa vitani dhidi ya jeshi la kitaifa na kudhibiti sehemu muhimu zote kwa mkoa wa mashariki.

Katika kipindi cha wiki chache tu, idadi kubwa ya watu wameuawa na vita vilevile vimechangia vita vya maneno kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na jirani yake, Rwanda.

Je, tulifikaje hapa?

Mwishoni mwa mwezi Januari 2025 Rais Felix Tshisekedi alilazimika kukatiza ziara yake mjini Davos Uswizi baada ya mapigano makali kuzuka katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo waasi wa M23 na jeshi walidaiwa kufyatuliana risasi.

Wakati huo wote wakazi walisambaza video za wapiganaji wa M23 wakishika doria katika maeneo muhimu ya mji wa Goma.

Na wakati ambapo maelfu ya raia walionekana kutorokea miji jirani, waasi walitangaza kuudhibiti mji wa Goma madai ambayo awali yalipingwa na mamlaka ya DR Congo.

Serikali ya DRC ililisisitiza kuwa bado vikosi vyake vinadhibiti maeneo ya kimkakati ikiwemo uwanja wa ndege.

Rwanda inasemaje?

DR Congo inaishtumu nchi jirani ya Rwanda kwa madai ya kutangaza vita na kutuma wanajeshi wake mpakani kuunga mkono wapiganaji wa M23.

Rwanda haikatai kuunga mkono M23 lakini inashutumu mamlaka ya Congo kwa kuunga mkono wanamgambo wanaojaribu kuipindua serikali ya Kigali.

Rwanda inadai mamlaka ya Congo ilikuwa ikifanya kazi na baadhi ya wale waliohusika na mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994, ambao walitorokea mpakani kuelekea DR Congo.

Kundi la M23 limechukua udhibiti wa maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye utajiri wa madini tangu 2021.

Kufuatia utekaji huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umewashutumu waasi wa M23 kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa na DRC na Rwanda mwezi Julai mwaka jana.

Mkuu wa ujumbe huo Bintou Keita alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mashambulizi na kuelezea kukamatwa kwa mji wa mashariki wa Masisi kama hatua ya kutisha.

Awali waasi hao waliwaamuru wanajeshi kusalimisha silaha zao na kuweka muda wa mwisho wa saa 48 ambao ulikamilika mapema Jumatatu.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walisema kuwa baadhi ya wanajeshi wa Congo walisalimisha silaha zao pamoja nao kabla ya muda uliowekwa.

Je, suluhu ya mzozo huu inaweza kupatikana?

Juhudi za upatanishi wa kikanda juu ya utatuzi wa mzozo wa DRC, M23 na Rwanda kupitia mazungumzo ya Nairobi na ya Luanda yaliyoongozwa na Rais wa Angola João Lourenço na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na kutumwa kwa vikosi vya Afrika Mashariki, na vile vya SADC zimeshindwa kupata suluhu ya amani kufikia sasa katika eneo hilo la mashariki mwa DRC.

Kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kinachofahamika kama MONUSCO ambacho kimekuwa DRC kwa miaka takriban 30 pia kimeshindwa kumaliza mzozo wa Mashariki mwa DRC.

Pande zote pia zimekuwa zikilaumiana kwa kukiuka makubaliano ya amani, ambayo yangeweza kuleta suluhu la mzozo huo.

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia Dkt. Nicodemus Minde anasema suluhu la mzozo wa DRC litapatikana kwa njia ya kisiasa na kidiplomasia na sio kwa hatua za kijeshi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa.

Jambo la kwanza ''Kunapaswa kuwa na muktadha wa kufahamu ni nini kinachoendelea, Rwanda, DRC – Kwa wasuluhishaji ni muhimu kuangalia chimbuko kihistoria zaidi na kufahamu chimbuko la mzozo. Tukifahamu historia ya vita na malumbano itakuwa ni njia nzuri'', anasema Dkt. Minde.

Kulingana naye suluhu ya sasa ni kuwakutanisha mahasimu na kuwaleta katika meza ya mazungumzo. Hata hivyo anasema mzozo huu hauna suluhisho moja tu.

''Mzozo huu unahitaji suluhisho la usitishaji mapigano, suluhisho la muda mfupi la utekelezaji wa michakato ya amani inayoendelea kwa mfano mchakato wa Luanda uliokwama kutokana na Rwanda kutokubaliana nao, na mchakato wa Nairobi uliosusiwa na Rais wa DRC Felix Tschidekedi''.

Imeandaliwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Athuman Mtulya