Kwanini uchomaji wa Quran umekithiri Sweden?

Mwanaume mwenye asili ya Iraq alichoma moto Quran hadharani mbele ya msikiti mkuu katika mji mkuu wa Uswidi, Stockholm katika siku tukufu ya Eid-ul-Azha. Salwan Momika alikuja Uswidi kama mhamiaji miaka mitano iliyopita na kuviambia vyombo vya habari kwamba sasa ana hati ya kusafiria ya Uswidi. Anadai kuwa yeye ni mtu asiyeamini Mungu.

Kauli yake: Qur'an inapingana na misingi ya demokrasia, uadilifu, haki za binadamu na haki za wanawake katika jamii ya Magharibi na kwa hivyo inapaswa kupigwa marufuku.

Lakini hakuwa wa kwanza kuinajisi Quran waziwazi nchini Uswidi. Matukio ya uchomaji pia yametokea Januari mwaka huu na mwaka 2020.

Mwezi Aprili mwaka jana, kikundi chenye itikadi kali za mrengo wa kulia kiitwacho Sturm Kurs kilichoma Quran huko Malmö, na kusababisha maandamano makubwa nchini kote. Stram Kurz kinajuulikana kwa kupinga uhamiaji na kupinga Uislamu, kundi hilo linaongozwa na mtu mwenye msimamo mkali anayeitwa Rasmus Paludan.

Kuongezeka mrengo wa kulia

Wasweden waliujui Uislamu kwa mara ya kwanza katika karne ya 16-17, wakati nchi hiyo ikipata nguvu za kijeshi.

Dola la Uswidi lilipotanuka, ndivyo mtazamo kuhusu dini ulivyoongezeka. Ingawa Wasweden hapo awali walikuwa Wakatoliki, nchi hiyo ikawa nchi ya Kiprotestant katika karne ya 16. Mnamo 1665, Wasweden waliharamisha dini za kijadi.

Wakati huo, Wakatoliki na Waislamu walionekana kuwa maadui wa "Ukristo wa kweli". Baada ya Vita vya pili vya dunia, uliberali uliongezeka nchini Uswidi pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Nchi ikiwa inaongozwa kwa sheria za kidunia.

Rais wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uswidi, Omar Mustafa anafikiri kwamba kuna mabadiliko makubwa katika mtazamo wa Wasweden. Anasema chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka. Na udhihirisho hauko tu kwenye mitandao, lakini ni katika maisha ya Waislamu.

Baada ya tukio la hivi karibuni la kuchomwa moto kwa Quran, alitoa maelezo juu ya matukio mbalimbali ya chuki kwa vyombo vya habari.

Ni pamoja na: kunyanyaswa kwa wanawake wa Kiislamu mitaani, kuchomwa moto nyumba za Waislamu na mashambulizi ya kinyemela kwenye misikiti.

Mwanahabari Tasneem Khalil ameishi nchini Sweden kwa muda mrefu. Ni mtu maarufu nchini humo. Anaamini siasa zinachangia kuibuka kwa itikadi kali za mrengo wa kulia kote Ulaya.

Anaeleza serikali ya sasa ya Uswidi iko madarakani kwa kuungwa mkono na chama kimoja kikuu cha Sweden Democrats kilichopata asilimia 20 ya kura katika uchaguzi uliopita. Walipata viti 72 katika bunge lenye viti 349.

Chama cha Demokrasia cha Uswidi awali kilikuwa chama cha mrengo mkali wa kulia ambacho kiliamini itikadi ya Nazi. Kwa kiwango kidogo, bado ni wabaguzi wa rangi, na wanaopinga wahamiaji.

"Matokeo yake, vyama vyenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia ambavyo hapo awali vilichukuliwa kama vikundi vya pembeni, sasa vimeibuka kuwa na nguvu mkubwa katika uwanja wa kisiasa," anasema.

Vyama hivi vya mrengo wa kulia vimeundwa ili kuvunja 'mwiko' au majadiliano yaliyokatazwa katika jamii ya Uswidi.

“Uhuru wa kujieleza katika katiba ya Sweden unatumiwa na vyama vya msimamo mkali wa mrengo wa kulia kuwashambulia walio wachache,” anasema, “na ndiyo maana tunaona matukio mengi zaidi kama vile, kuchomwa Quran."

"Waislamu sio sehemu kubwa sana ya watu hapa. Lakini ni rahisi kuwachokoza. Na kwa uchokozi huo Waislamu ulimwenguni kote hukasirika. Na matukio mbalimbali hutokea. Na hivyo ndivyo makundi ya mrengo wa kulia hufanya kwa njia iliyopangwa vizuri, ili kubadilisha mitazamo ya jamii ya Uswidi dhidi ya Waislamu. "

Chuki dhidi ya wahamiaji na Uislamu

Chuo Kikuu cha California kimefanya utafiti juu ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Uswidi.

Mmoja wa watafiti wake, Abdelkader Ng, anaeleza kwamba mitazamo ya Uswidi dhidi ya Waislamu ilianza kubadilika mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kura ya maoni ya 2014 inaonyesha 35% ya waliohojiwa walidhani Uislamu ni tishio kwa mtindo wa maisha wa Ulaya. Na 57% waliamini wakimbizi ni tishio kwa usalama wa taifa la Uswidi.

Judy Safin ameandika makala katika jarida la Berkeley Political Review kwamba chiki dhidi ya Uislamu zinaongezeka sio tu nchini Uswidi, bali duniani kote.

"Hasa Waislamu katika nchi kama Syria na Iraqi ambao wamekumbwa na vita na migogoro ya kifedha katika nchi zao. Chuki na hofu ya wageni inahusishwa na misimamo mikali ya utaifa katika nchi mbalimbali. Watu sasa wanakataa kuwasaidia 'wengine' kwa hofu ya kupoteza utambulisho wao wa kitamaduni, kazi na hata usalama."

Akilinganisha wakimbizi kutoka Ukraine na wale kutoka Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Urusi, ameandika, vyombo vya habari vya Sweden na viongozi wa kisiasa walisema mara kwa mara kwamba wakimbizi wa Ukraine "sio wakimbizi kutoka Syria, ni wakimbizi kutoka Ukraine ... ni Wakristo na ni wazungu."

Kwa hivyo, anaamini kuwa chuki dhidi ya wasio Wakristo na jamii za wachache zinaongezeka sana barani Ulaya.

Uhuru wa kujieleza dhidi ya uvumilivu

Mpango wa Salwan Momika wa kuchoma Quran haukuwa wa ghafla. Kwa muda mrefu aliomba ruhusa kwa mamlaka ya Uswidi ya kuandamana mbele ya msikiti. Lakini kwa vile polisi hawakutoa kibali, suala hilo lilienda mahakamani na kesi ikaendelea kwa muda wa miezi mitatu. Hatimaye mahakama ilimruhusu.

Kwa sababu ana haki ya kuandamana kwa mujibu wa katiba ya Uswidi. Serikali ya Uswidi ilishtushwa na majibu kutoka nchi za Kiislamu kwa tukio hili na hatimaye ikamkosoa Salwan Momika kama 'mtu wa mwenye chuki dhidi ya Uislamu.

Lakini baada ya tukio hili, mjadala mkubwa ulianza nchini Sweden kuhusu mipaka ya uhuru wa kujieleza. Polisi wa Uswidi sasa wanasema wamepokea maombi mapya ya maandamano kutoka kwa watu wanaotaka kuchoma Torati na Biblia, na sio Quran pekee.

Baadhi ya wachambuzi nchini Uswidi wanafikiri maandamano kama hayo yanapaswa kuchukuliwa kama vitendo vya chuki. Kwa sababu wanalenga watu maalumu, jambo ambalo limepigwa marufuku na sheria ya Uswidi.

Kwa upande mwingine, wengi ndani ya Uswidi wanasema kwamba ukosoaji wa dini, hata kama unaonekana kuwachukiza wale wanaoamini, unapaswa kuruhusiwa. Pia wanasema shinikizo la kurudisha sheria ya kukufuru, linapaswa kupingwa. Sheria hiyo ilifutwa miongo kadhaa.

Ndoto ya Uswidi kujiunga NATO

Wachambuzi wanaamini matumaini ya Uswidi kuwa mwanachama wa NATO yatapata pigo jingine baada ya Quran ya pili kuchomwa moto mjini Stockholm katika muda wa miezi sita.

Uswidi na Ufini zilituma maombi ya uanachama wa NATO mwaka jana, zikiacha sera yao ya muda mrefu ya kutoegemea upande wowote kijeshi kufuatia mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine.

Uanachama unahitaji idhini ya nchi zote wanachama wa NATO. Lakini Türkiye na Hungary bado hawajaunga mkono ombi la Uswidi.

Serikali ya Uturuki ya Erdogan imeishutumu mara kwa mara serikali ya Uswidi kwa kulihifadhi kundi la waasi la Kurdistan Workers' Party au PKK na makundi mengine ya upinzani ya Uturuki. Serikali ya Ankara inawachukulia kama magaidi.

Ikiwa serikali ya Uswidi haitachukua hatua dhidi yao, hawataunga mkono kujiunga na NATO. Maandamano makubwa yalifanyika mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm Januari mwaka jana na Qur'an Sharif pia iliteketezwa.

Maandamano hayo yaliandaliwa na kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia na chuki dhidi ya Uislamu, Rasmus Paludan.

Wakati huo huo, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema Jumatatu iliyopita kuwa nchi yake bado haiko tayari kuidhinisha uanachama wa Uswidi katika NATO.

"Shambulio la kutisha dhidi ya kitabu chetu kitakatifu, Quran, huko Stockholm lilitukera sisi sote," alisema.