Kutoka jela hadi kuwa rais mwenye umri mdogo kuchaguliwa Afrika

Na Natasha Booty

BBC , News

th

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, "Sikuwahi kuzingatia kujiingiza katika siasa kamwe ," anasema mtoza ushuru huyo wa zamani na mume kwa wake wawili

Wachache walikuwa wamesikia kumhusu mwaka mmoja uliopita, na sasa anatazamiwa kuwa rais.

Kuinuka kwa njia ya ajabu kwa Bassirou Diomaye Faye kunafikia kipindi cha hali ya juu katika siasa za Senegal ambazo ziliwavutia watu wengi.

Miezi ya kukaa jela pamoja na mshirika na mwanasiasa mwenye ushawishi Ousmane Sonko iliisha ghafla, wawili hao wakiachiliwa wiki moja kabla ya uchaguzi wa urais.

Sasa 'Bw Safi', kama anavyoitwa kwa jina la utani, lazima aanze kufanyia kazi mageuzi makubwa aliyoahidi.

"Anayependa utaratibu" na "Asiye wa kujionyesha" ni maneno yanayotumiwa mara nyingi kuelezea mtoza ushuru huyo wa zamani ambaye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya mwaka 44 hapo jana Jumatatu.

Bw Faye anakumbuka kwa furaha maisha yake ya kijijini huko Ndiaganiao, ambapo anasema yeye hurudi kila Jumapili kufanya kazi ya shamba.

Upendo na heshima yake kwa maisha ya kijijini inalingana na kutokuwa na imani kubwa na wasomi wa Senegal na walio katika siasa za sasa.

"Hajawahi kuwa waziri na hakuwa kiongozi wa serikali hivyo wakosoaji wanahoji ukosefu wake wa uzoefu," mchambuzi Alioune Tine aliambia BBC.

"Lakini, kwa mtazamo wa Faye, watu wa ndani ambao wameendesha nchi tangu 1960 wameshindwa kwa kiasi kikubwa."

Kupambana na umaskini, ukosefu wa haki na ufisadi ni ajenda kuu ya Bw Faye. Walipokuwa wakifanya kazi katika Hazina ya kitaifa , yeye na Bw Sonko waliunda jopokazi la muungano ili kukabiliana na ufisadi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Makubaliano ya gesi, mafuta, uvuvi na ulinzi lazima yote yajadiliwe upya ili kuwahudumia vyema watu wa Senegal, anasema Bw Faye.

Anaanzisha enzi ya "uhuru" na "mpasuka" kinyume na zaidi ya hayo, aliwaambia wapiga kura, na hiyo ni kweli hasa kwa uhusiano na Ufaransa.

Rais mteule wa Senegal anasema kuwa ataondoa sarafu ya CFA franc ambayo inakosolewa sana, ambayo imeegemezwa kwenye euro na kuungwa mkono na mkoloni wa zamani Ufaransa.

Bw Faye anataka kubadilisha sarafu mpya ya Senegal, au eneo la Afrika Magharibi, ingawa hii haitakuwa rahisi.

"Itabidi ashughulikie uhalisia wa bajeti kwa kuanzia... Lakini naona kwamba ana matamanio mengi," Waziri Mkuu wa zamani Aminata Touré, ambaye alihudumu chini ya Rais anayeondoka Macky Sall, anaiambia BBC.

Kuimarisha uhuru wa mahakama na kuunda nafasi za kazi kwa vijana wengi wa Senegal pia ni vipaumbele muhimu kwa Bw Faye - ambayo "Rais Sall aliyapuuza sana na yakamrudi", Bi Touré anaongeza.

Yeye sio kigogo pekee wa kisiasa ambaye amemuunga mkono Faye mwenye umri wa miaka 44 - Rais wa zamani Abdoulaye Wade alifanya vivyo hivyo siku mbili tu kabla ya kura ya Jumapili.

Ni mabadiliko ya ajabu kwa Bw Faye ambaye alikaa gerezani miezi 11 iliyopita kwa mashtaka ya uasi, na miaka mingi zaidi kabla ya hapo chini ya kivuli cha mshirika wake.

'Bassirou ni mimi'

Bassirou Diomaye Faye alitangazwa mwezi Februari kama mgombea anayeitwa "Mpango B", akichukua nafasi ya kigogo wa upinzani Ousmane Sonko. "Ningesema hata ana uadilifu zaidi kuniliko," Bw Sonko alisema kwa majigambo.

Wanaume wote wawili walianzisha chama ambacho sasa kilivunjwa cha Pastef, wote ni watoza ushuru, na wanaume wote walijikuta wamefungwa mwaka jana kwa mashtaka ambayo walisema yalichochewa kisiasa.

Bw Sonko aliishia kuhukumiwa kwa makosa mawili, jambo lililomaanisha kwamba alizuiwa kushiriki uchaguzi, hivyo Bw Faye akaingilia kati.

"Bassirou ni mimi," Bw Sonko aliwaambia wafuasi hivi majuzi. "Ni pande mbili za sarafu moja," mwenzake wa Pastef Moustapha Sarré anakubali.

Hii imesababisha ukosoaji kwamba Bw Faye ni "rais kwa chaguo-msingi".

Si hivyo, asema mchambuzi Bw Tine. Lakini uhusiano wa wawili hao unaweza kuleta mtindo mpya wa uongozi.

"Labda wataanzisha mtindo wa kujitenga na mfumo wa urais wa kuwa na mkuu wa nchi mwenye mamlaka yote'

"Sonko bila shaka ni kiongozi asiyepingwa wa Pastef - Kilelezo haswa ... [Lakini] wawili hao wamekuwa na [nguvu] ya ushirikiano na kutegemeana."

Hapo zamani za kale, Bw Faye hakutaka kujihusisha na siasa. "Haijawahi kuniingia akilini," alisema mnamo 2019 wakati akikumbuka utoto wake.

Mmoja wa mashujaa wa Bw Faye ni mwanahistoria wa Senegal marehemu Cheikh Anta Diop - ambaye kazi yake inaonekana kama mtangulizi wa Afrocentrism-dhana ya kuipigania Afrika na itikadi zake. Wote wanaonekana kama wafuasi wa mrengo wa kushoto wa kuunga mkono sera zinazoigemea Afrika iliyoungana.

Matokeo ya mapema yalipokuja siku ya Jumatatu yakionyesha Bw Faye anatazamiwa kupata ushindi, watu katika mji mkuu, Dakar, walisherehekea kwa kupiga honi za gari na kuimba kwa sauti kubwa ya muziki.

Mwitikio kutoka kwa masoko ya kimataifa haukuvutia kwa kiasi hicho, huku dhamana za dola za Senegal zikishuka hadi kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miezi mitano. Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa wawekezaji wana wasiwasi kuwa uongozi wa Bw Faye huenda ukapuuza sera za nchi zinazofaa kibiashara.

Awali uchaguzi ulikuwa ufanyike mwezi uliopita lakini Bw Sall aliahirisha saa chache kabla ya kampeni kuanza, na kusababisha maandamano makubwa ya upinzani na mgogoro wa kidemokrasia.

Wagombea wengi walikuwa na muda mchache sana wa kujiandaa mara tu tarehe mpya ya uchaguzi ilipowekwa - lakini Bw Faye alikuwa na zaidi ya wiki moja tu baada ya kuachiliwa kutoka jela.

Licha ya kipindi kifupi cha kampeni, raia wa Senegal walikuwa wameshikilia kwamba watajitokeza na kutumia kura yao, Christopher Fomunyoh - wa Taasisi ya Kitaifa ya Kidemokrasia ya Mambo ya Kimataifa - aliiambia BBC Newsday .

"Senegal iko katika mchakato wa kuthibitisha kwamba demokrasia inaweza kujisahihisha na kuja kuwa na nguvu na uthabiti zaidi."

Na mtihani wa kweli kwa 'msafishaji' wa Senegal ndio umeanza.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Lizzy Masinga