Fahamu wachezaji 5 bora duniani ambao hawakuwahi kucheza kombe la dunia

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Kombe la dunia linaanza leo kwa mechi ya ufunguzi kati ya mwenyeji Qatar dhidi ya Ecuador. Ni mashindano yanayofanyika kila baadaya miaka minne na mwaka huu yatafanyika kwa siku 29 mpaka Disemba 18 kumsaka bingwa wa dunia.

Brazil, Argentina nabingwa mtetezi, Ufaransa zinapigiwa chapuo kushinda kombe hilo lenye hadhi ku bwa kabisa duniani kwenye soka la kimataifa.

Ni mashindano yanayoshirikisha wachezaji wengi nyota kama Pele, Maradona, Bobby Moore, Zinedine Zidane, Gary Lineker, Gerd Muller, Ronaldo de Lima, Lothar Matthaus , Franz Beckenbauer na Johan Cruyff.

Ni mashindano pia yanayoibua na kujenga majina ya wachezaji wengi kama Miroslav Klose wa Ujerumani, Davor Šuker ambaye fainali za mwaka 2018 zilimtambulisha vyema kisoka.

Zikiwa ni fainali za 22 tangu yaanzishwe mwaka 1930, wapo wachezaji wengi tu wakubwa duniani wenye majina na bora ambao hawakuwahi kucheza, kwa sababu mbalimbali, ikiwemo majeruhi, kuachwa ama timu zao kutofuzu.

Wengine kama Erling Haaland hawajacheza lakini bado wana nafas kwa kuwa wanaendelea kusakata kabumbu sasa, hawa ni miongoni ni nyota ambao, kombe la dunia ni historia kwao.

1.George Best - Ireland Kaskazini

George Best ni nembo ya Manchester United. Aliichezea kwa mafanikio makubwa. Alikuwa na uchawi miguuni mwake lakini hakuweza kulisaidia taifa lake la Ireland Kaskazini kufuzu Kombe la Dunia katika maisha yake ya soka.

Best ameitumikia taifa lake mara 37 na kufunga mabao tisa. Kutokucheza kombe la dunia, kungekamilisha historia nzuri ya soka ya gwiji hili la soka. Mwaka 1982, kidogo awe kwenye fainali lakini ilishindaka.

2. Alfredo Di Stefano - Hispania, Colombia na Argentina

Alfredo Di Stefano ni kama alikuwa na mkosi. Mmoja wa wachezaji bora wa soka kuwahi kutokea duniani. Alitajwa na Pele kama mchezaji wake bora kuwahi kutokea duniani.

Aliichezea Real Madrid kwa mafanikio makubwa na aliwakilisha katika mashindano ya kimataifa kwa nchi tatu tofauti - Hispania, Colombia na Argentina - lakini hakufanikiwa kucheza fainali hata moja za Kombe la Dunia.

Argentina haikushiriki Kombe la Dunia la 1950. Alipopata uraia wa Hispania, hakushiriki Kombe la Dunia la 1954 baada ya awali kuzichezea nchi za Argentina na Colombia.

Alicheza mechi chache za kufuzu lakini Hispania ilishindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 1958. Lakini ilipofuzu mwaka wa 1962, Di Stefano hakuweza kushiriki kwa sababu alikuwa ameumia.

3. George Weah - Liberia

Weah ndiye muafrika pekee kuwahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia. Alitwaa mwaka 1995. Anatajwa kama mchezaji bora kuwahi kutokea Afrika. Akitwa uchezaji bora Afrika mara 3 mwaka 1989, 1994 na 1995 huku mwaka 1996 akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa karne Afrika.

Pia ndiye mchezaji wa kwanza pia wa kulipwa kutoka Afrika kuwa Rais, akiwa rais wa Liberia tangu mwaka 2018.

Alikuwa katika ubora wa hali ya juu katika miaka ya 1990 akicheza kwa miaka 14 Ulaya kwenye vilabu vya Monaco, PSG, AC Milan, Chelsea na Manchester City.

Aliletwa Ulaya na Arsen Wenger, kocha wa zamani wa Arsenal, wakati huo akiifundisha Monaco. Pamoja na kuwa mpachika mabao bora kwenye klabu bingwa Ulaya msimu wa 1994/1995 na kutwa mataji mawili ya Seria A, na pia League 1 Ufaransa, hakuwa kucheza fainali za kombe la dunia, kwa kuwa timu yake ya Liberia hakuweza kufuzu hata mara moja wakati akicheza soka.

4. Ian Rush - Wales

Ian Rush kwa sasa anashikilia rekodi ya kupachika mabao mengi kwenye timu yake ya taifa, Wales, mabao 28.

Alikuwa gwiji hasa wa kupachika mabao akiicheze Liverpool kwa mafanikio makubwa, lakini na yeye hakuweza kuisaidia Wales kufuzu fainali za kombe la dunia.

Rush ni mmoja wa magwiji wengi wa Wales ambao hawakufanikiwa kucheza mashindano hayo kwa taifa hilo kutofuzu, akiwemo Ryan Giggs, winga wa zamani wa Manchester United.

Hata hivyo mashindano ya sasa, Wales imefuzu na kuwapa nafasi nyota wa sasa, Akiwemo nahodha Garath Bale na Aaron Ramsey kushiriki kwa mara ya kwanza. Wales imewahi kufuzu mara moja tu fainali hizo, mwaka 1958 zilizofanyika Sweden na sasa ni ya pili.

5. Eric Cantona - Ufaransa

Cantona hakuwa na shida ya kiwango wala majeruhi ila tabia yake ilimfanya asicheze kwa muda mrefu katika timu ya Ufaransa na hivyo kupunguza nafasi yake ya kucheza Kombe la Dunia.

Baada ya kuonyesha hasira dhidi ya uamuzi wa kocha mkuu wa wakati huo Henri Michel kumuondoa kwenye kikosi katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 1990, Cantona alipigwa marufuku kushiriki mechi za kimataifa.

Alifurahia kipindi kizuri chini ya Michel Platini na Gerard Houllier, lakini baada ya tukio lake la Crystal Palace alilompiga mshabiki baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu, alizidi kujichafulia.

Alihukumiwa wiki mbili jela, adhabu iliyopunguzwa mpaka kufanya shughuli za kijamii, lakini alifungiwa miezi 8 kutocheza soka.

Mwaka 1997 alitangaza kustaafu soka akiwa na miaka 30 na kujiingiza kwenye filamu, akalikosa Kombe la Dunia la 1998 lililotawaliwa na mfaransa mwenzie Zinedine Zidane.