Je, Manchester United ilifanya makosa kumsajili tena Ronaldo?
Na Abdalla Seif Dzungu

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota wa Manchester United Cristiano Ronaldo amegonga vichwa vya hav=bari kwa mara nyingine kwa kudai kwamba klabu hiyo imemsaliti.
Mshambuliaji huyo hakukomea hapo tu, amesema pia 'hamuheshimu' meneja wa United, Ten Hag kwa kuwa kocha huyo amekataa kumuheshimu.
Katika mahojiano na mwanaspoti Pius Morgan kupitia TalkTv , mreno huyo aliongeza kwamba anadhani hatakiwi klabuni tangu msimu uliopita na kwamba anafanyiwa kila hila ili aondoke.
BBC Swahili imekuwa ikifuatilia matukio yanayomkumba CR7 tangu ajiunge tena na Mashetani hao wekundu na Mwanahabari wetu Seif Abdalla anachanganua
Ukubwa wa Ronaldo na Jina lake

Chanzo cha picha, Real Madrid
Jina Cristiano Ronaldo linapotajwa mahali popote pale katika ulimwengu wa soka , kitu cha kwanza kinachokuja akilini kwako ni kwamba yeye ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka. Akiwa kundi moja na kina Lionel Messi, Diego Maradona na Pele.
Ameshinda karibu kila kitu katika maisha yake. Amefanikiwa kutwaa mataji 32 katika maisha yake ya soka, yakiwemo matano ya ligi ya mabingwa Ulaya. Anashikilia rekodi ya kucheza michezo mingi zaidi ya ligi ya mabingwa Ulaya (183) na kupachika mabao mengi zaidi (140) katika ligi hiyo.
Ni mmoja wa wachezaji wachache duniani waliocheza michezo zaidi ya 1,100 ya soka la kulipwa, akiwa na klabu za Sporting Lisbon alipoanzia, Manchester United na Real Madrid.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or) ana mabao zaidi ya 800 kwenye maisha yake ya soka akiwa miaka na 37 kufikia sasa ndiye mchezaji mwenye umaarufu mkubwa zaidi duniani katika mtandao wa Instagram atakayeshiriki katika kombe la dunia nchini Qatar akiiwakilisha Ureno.
Hatahivyo mchezaji huyo katika siku za hivi karibuni amekuwa akigonga vichwa vya habari tangu alipojiunga tena na klabu yake ya zamani ya Manchester United akitokea Juventus msimu uliopita.
Aliichezea United chini ya Kocha Sir Alex Ferguson kwa misimu sita (2003–2009) na kuipa taji la ligi ya mabingwa Ulaya na mataji matatu ya ligi kuu England.
Kwa United Ronaldo ni mfalme, ni mshindi, ni kiongozi na kioo cha kila kitu. Japo uwezo wake wa sasa haufanani na miaka mitatu iliyopita ama hata miaka akiicheza United, ufalme wake unasalia kutokana na alichoshinda binafsi na mchango wake kwa klabu.
Lakini vichwa vya habari vimeibua mjadala mkubwa na havionyeshi kufurahisha ndani ya klabu ya Manchester united ambayo imeanza kujiinua katika wimbi la matokeo mabaya ya ligi ya England tangu kuwasili kwa Mkufunzi raia wa Uholanzi Eric Ten Hag.
Mzozo wa Ronaldo na United umeanzia wapi?
Matatizo ya Cristiano Ronaldo katika klabu Manchester United yalianza baada ya klabu hiyo kushindwa kufuzu katika kombe la klabu bingwa Ulaya msimu uliopita .
Msimu ambao mchezaji huyo mwenye haiba kubwa duniani alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo akifanikiwa kufunga mabao 24 katika michezo 38 aliyoitumikia timu hiyo.
Wakati huo Ronaldo aliomba kuruhusiwa na klabu hiyo kuhamia klabu nyingine inayoshiriki ligi ya mabingwa ili kupata nafasi ya kucheza klabu bingwa Ulaya iliyomjenga na kumpa hadhi.
Hatahivyo licha ya mikutano kadhaa na baadhi ya maafisa wa klabu hiyo, jibu alilopata ni kwamba hakukuwepo na timu iliokuwa ikimtaka isipokuwa timu moja nchini Saudia ambayo pia haikukubali sharti la kuendelea kulipa asilimia kubwa ya mshahara wake mkubwa.
Kusugulishwa 'benchi'

Chanzo cha picha, Getty Images
Cristiano Ronaldo anajiamini licha ya umri wake mkubwa anaona ana nguvu na uwezo wa kuendelea kushirikishwa katika kila mechi na mkufunzi Ten Hag.
Kwa upande mwingine, Erik ten Hag anajaribu kuunda kikosi ambacho kinaweza kutawala mpira, kukaba kuanzia mbele kwa mtindo wa kisasa, mbinu ambayo miongoni mwa mashabiki wengi wa soka wanaona haiendani na matarajio ya Ronaldo.
Lakini kitendo cha hivi majuzi cha Ronaldo kuondoka uwajani wakati ambapo kocha Ten Hag alikuwa anajiandaa kumuingiza ndicho dhidi ya Tottenham kilipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la mustakabali wake.
Kitendo hicho kilizua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki 'kindakindaki' wa timu hiyo pamoja na wachezaji wa zamani huku wengi wakihoji tabia yake.
Mchezaji wa kwanza kumshtumu Cristiano Ronaldo ni mchezaji mwenzake wa zamani wakiwa United, Wayne Rooney.
Mshambuliaji huyo wa zamani anayefundisha D.C United ya ligi kuu ya Marekani, alimshutumu Cristiano Ronaldo kwa kuwa ‘msumbufu’ katika klabu hiyo kutokana na tabia yake ‘isiyokubalika’ katika miezi ya hivi karibuni.
“Mambo ambayo amefanya tangu mwanzo wa msimu hayakubaliki kwa Manchester United. Nimemuona Roy Keane akimtetea. Roy asingekubali hilo. Roy hatakubali hilo hata kidogo," Rooney alieleza wakati akifanya mahojiano na chombo cha habari cha talkSPORT.
"Ni kero ambayo Manchester United haihitaji kwa sasa, alisisitiza Rooney.
"Kwa Cristiano, weka kichwa chako chini na ufanye kazi na uwe tayari kucheza wakati meneja anakuhitaji. Akifanya hivyo, atakuwa ni mchezaji mwenye thamani. Asipofanya hivyo, atakuwa kizuizi kisichohitajika, Rooney aliambia TalkSport.
Hatahivyo Ronaldo amemjibu Rooney katika mahojiano yake akisema kwamba anamuonea wivu na kwamba licha ya umri wake bado yuko na afya njema ya kuendelea kusakata soka la kiwango cha juu.
Je Man United ilifanya makosa kumsajili tena Ronaldo?
Kurejea kwa Ronaldo katika klabu ya Mashetani Wekundu kulionekana kama kama ushindi mkubwa ndani na nje ya klabu hiyo.
Hata hivyo, kulikuwa na hofu pia kutoka kwa watu nje ya Klabu kwamba amerejea tu kwa sababu United walikuwa wamepania kumzuia kujiunga na Manchester City.
Na kwa mujibu wa gazeti la The Mirror, uongozi wa Old Trafford ulikuwa tayari umeanza kukubali kwamba kwa hakika ilikuwa ‘kosa la maamuzi’ katika uamuzi uliofanywa kwa sababu zisizo sahihi.
Waliamini kuwa mshindi huyo mara tano wa taji la Ballon d’Or angewafanya wawe washindani wakubwa wa mataji ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, kumsajili bila mpango kumeiwacha klabu hiyo katika mtafaruku.
Huku wakisalia katika nafasi ya timu tano bora katika jedwali la ligi ya England, hakuna siri kwamba msimu huu haujaimarika licha ya kuwasili kwa Erik ten Hag.
Na kufuatia mahojiano yake na Pius Morgan wa TalkTv kuna uwezekano mkubwa United haitamzuia iwapo anataka kuondoka baada ya kombe la dunia hapo Januari.
Ndoa ya 'tende' ya Ronaldo na United imefikia ukomo?

Chanzo cha picha, BBC Sport
"Sina shaka kwamba Ronaldo hatoichezea tena Manchester United," mlinda mlango wa zamani wa Uingereza Rob Green alisema kupitia BBC Radio 5 Live.
"Ni talaka mbaya lakini Ten Hag alikuwa na subra muda mrefu. Ronaldo amejiharibia ."
United sasa imemaliza mechi yake ya mwisho dhidi ya Fullham ugenini mwishoni mwa wiki kabla ya kombe la dunia kwa ushindi wa magoli 2-1.
Lakini kufuatia madai yake kwamba klabu hiyo imemsaliti na kwamba hana hamuheshimu tena na kocha wake Ten hag , ni dhahiri tosha kwamba kilichosalia 'ndoa' imefikia ukomo na ni wakati mchezaji huyo kuiaga Old Trafford.
Kulikuwa na watu huko United wakati wa msimu wa joto waliohisi kwamba chumba cha kubadilishia jezi cha United kingekuwa bora bila Ronaldo.
Matamshi ya mchezaji hayo yanaonyesha ushahidi wa hilo.
Baada ya kombe la dunia ni bora pande zote mbili kuona iwapo wanaweza kusonga mbele bila ya mmoja wao, hata ikimmmnisha kwamba kwamba United italamika kumlipa mshahara wake uliosalia ama mchezaji huyo kuondoka bila kuchukua chochote.












