Tunachokijua kufikia sasa kuhusu benki iliyoporomoka ya SVB nchini Marekani

Hisa za benki barani Asia na Ulaya zilianguka licha ya kuhakikishiwa na rais wa Marekani kwamba mfumo wa kifedha wa Marekani uko salama kufuatia kuporomoka kwa benki mbili nchini Marekani.

Kuporomoka huku kunakuja baada ya mamlaka kuchukua hatua ili kulinda akiba za wateja wakati Benki ya Silicon Valley (SVB) yenye makao yake makuu nchini Marekani na Benki ya Signature zilipoporomoka.

Joe Biden aliahidi kufanya "chochote kinachohitajika" kulinda mfumo wa benki.

Lakini wawekezaji wanahofia wakopeshaji wengine bado wanaweza kuathiriwa na matokeo mabaya.

Siku ya Jumanne, hisa ya Benki ya Topix ya Japan ilishuka kwa zaidi ya asilimia 7, na kuiweka kwenye mkondo kwa siku yake mbaya zaidi katika zaidi ya miaka mitatu.

Hisa za Mitsubishi UFJ Financial Group, mkopeshaji mkubwa zaidi kwa mali nchini, zilipungua kwa asilimia 8.1 katika biashara ya katikati ya siku ya Asia.

Siku ya Jumatatu, Santander ya Uhispania na Commerzbank ya Ujerumani walishuhudia bei za hisa zao zikishuka kwa zaidi ya asilimia 10 kwa wakati mmoja.

Benki ndogo za Marekani zilipata hasara mbaya zaidi kuliko zile za Ulaya, licha ya kuwahakikishia wateja kwamba walikuwa na zaidi ya ukwasi wa kutosha kujikinga na majanga.

Kubadilikabadilika kumesababisha uvumi kuwa hazina ya serikali sasa itasitisha mipango yake ya kuendelea kuongeza viwango vya riba, iliyoundwa kudhibiti mfumuko wa bei.

Bw Biden alisema kuwa watu na wafanyabiashara ambao walikuwa wameweka pesa kwenye Benki ya Silicon Valley wataweza kupata pesa zao zote kuanzia Jumatatu, baada ya serikali kuingilia kati kulinda akiba zao kikamilifu.

Benki ya Silicon Valley iliangukaje?

Benki ya Silicon Valley - ambayo ilibobea katika kutoa mikopo kwa makampuni ya teknolojia - ilifungwa na wadhibiti wa Marekani ambao walitwaa mali yake siku ya Ijumaa. Ilikuwa ni kuanguka kubaya zaidi kwa benki ya Marekani tangu mgogoro wa kifedha mwaka 2008.

Imekuwa ikijaribu kutafuta pesa ili kuziba hasara kutokana na mauzo ya mali iliyoathiriwa na viwango vya juu vya riba. Habari kuhusu matatizo hayo ilisababisha wateja kukimbilia kuchukua fedha, na kusababisha mgogoro wa fedha.

Mamlaka siku ya Jumapili pia zilitwaa Benki ya Signature huko New York, ambayo ilikuwa na wateja wengi wanaohusika na crypto na ilionekana kuwa taasisi iliyo hatarini zaidi na janga sawa na hilo.

Bw Biden aliahidi kwamba kufidia akiba hizo hakutagharimu walipa kodi chochote, na badala yake kutafadhiliwa na ada wasimamizi wanatoza benki.

Kama sehemu ya jitihada za kurejesha imani, wasimamizi wa Marekani pia walizindua njia mpya ya benki kukopa fedha za dharura katika mgogoro.

Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba kushindwa, ambayo ilikuja baada ya kuanguka kwa benki nyingine ya Marekani, Silvergate Bank, wiki iliyopita, ni ishara ya matatizo katika makampuni mengine.

Paul Ashworth wa Capital Economics alisema mamlaka ya Marekani "ilichukua hatua kali kuzuia athari zaidi kutokea".

Mgogoro wa kisiasa

Kuanguka kwa SVB kumeibua upya mijadala - sawa na ile iliyoonekana kufuatia mgogoro wa kifedha wa mwaka 2008 - kuhusu ni kiasi gani serikali inapaswa kufanya kudhibiti na kulinda benki.

Mwenyekiti wa Hazina ya serikali ya Marekani, Jerome Powell, anasema kutakuwa na mapitio ya kina na ya uwazi ya anguko hilo.

Bw Biden alitoa wito kwa sheria kali zaidi na kusisitiza kuwa wawekezaji na viongozi wa benki hawatasalimika.

"Walijihatarisha... hivyo ndivyo ubepari unavyofanya kazi," alisema.

Seneta wa Republican Tim Scott, anayeonekana kama mgombeaji wa urais mnamo mwaka 2024, aliita uokoaji huo kuwa"shida".

Kwa mara nyingine tena watu wana wasiwasi kuhusu benki. Kwa mara nyingine tena kuna mjadala mkali kuhusu dhamana. Lakini hii sio 2008.

Kufuatia msukosuko wa fedha duniani, mkazo ulikuwa katika kufanya mageuzi katika benki zilizochukuliwa kuwa "kubwa sana kuanguka". Matatizo ya leo yanajikita kwenye benki za ukubwa wa kati na ndogo.

Benki zote mbili zilizoanguka - Benki ya Silicon Valley na Benki ya Signature - zilikuwa na kitu kimoja kwa pamoja: miundo yao ya biashara ilikuwa imejilimbikizia sana katika sekta moja na walikuwa na mali ambayo thamani yake ilikabiliwa na shinikizo kutoka kwa viwango vya juu vya riba.

Kwa kuwa benki nyingi zina mseto mzuri na zina pesa taslimu nyingi, dhana ni kwamba hatari kwa sekta nyingine ya benki ni ndogo. Hilo halitazuia wasimamizi kuangalia ni nini kilienda vibaya na ni sheria gani zinahitaji kubadilishwa.

Na shinikizo kwa benki ndogo na za kati haijaondoka. Kile kitatokea kwa uchumi wa Marekani na mapambano dhidi ya mfumuko wa bei bado havijaonekana.