Afcon 2023: Kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi kuandaa Afcon

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa serikali ya Ivory Coast dola bilioni 1 zimetumika kuandaa mashindano hayo, ambayo yataanza Jumamosi, baada ya kujenga viwanja vinne vipya na kukarabati vingine viwili.
Aidha, viwanja vya ndege, barabara, hospitali na hoteli zimejengwa au kuboreshwa katika miji mitano itakayoandaa mechi; Abidjan, Bouake, Korhogo, San Pedro na Yamoussoukro.
Ni ujenzi mkubwa wa maendeleo katika taifa hilo la Afrika Magharibi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002-2007 na 2010-11. Baadhi ya fedha za ujenzi zimetokana na mkopo wa dola za kimarekani bilioni 3.5 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Aprili mwaka jana.
Huku Ivory Coast ikiorodheshwa kama taifa la 138 kati ya 190 na IMF kwa ukubwa wa uchumi. Uchumi wake umekuwa kwa wastani wa 8% kwa mwaka tangu Rais Alassane Ouattara, mfanyakazi wa zamani wa IMF achukue madaraka 2010.
"Ivory Coast ni nchi maskini," Prao Yao Seraphin, profesa wa uchumi wa Ivory Coast, aliiambia BBC Sport Africa.
"Kutokana na hali hiyo, Rais Ouattara amelazimika kuchukua mikopo kufadhili mradi huu, hivyo tunapaswa kuhakikisha mikopo hiyo inanufaisha Ivory Coast. Nchi italazimika kutunza miundombinu."
Ivory Coast, ambayo wakati mmoja ilikuwa nyumbani kwa mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya tembo barani Afrika – itakuwa mwenyeji wa kombe la Afrika mwaka huu.
Maendeleo kwa siku zijazo

Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images
Baada ya kutumia zaidi ya dola bilioni 1 - huku baadhi ya ripoti za vyombo vya habari zikiripoti mara mbili ya kiasi hicho kama ya maandilizi - Ivory Coast inasema haijandaa mashindano hayo ili kupata pesa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Francois Amichia, anaendesha kamati ya maandalizi ya Kombe la Mataifa ya 2023, anasema "Ivory Coast ilipoamua kuandaa kombe hili, haikuwa kutafuta pesa bali kujipanga upya," anasema Amichia, ambaye pia ni mbunge na waziri wa zamani wa michezo.
"Ni fursa ya kujenga miundombinu ya michezo na lazima niwakumbushe hakuna miundombinu ya michezo iliyojengwa kwa miaka mingi - Kombe la Mataifa ya Afrika limeruhusu kuwa na viwanja vinne vipya na viwili vilivyokarabatiwa."
Kiasi cha dola za kimarekani milioni 79, milioni 84 na milioni 113 zimetumika kujenga viwanja vipya Yamoussoukro, Korhogo na Abidjan huku ukarabati wa uwanja wa Felix Houphouet-Boigny, Abidjan ukigharimu dola za kimarekani milioni 109.
Uwanja huo ulijengwa mwaka 1964, baadaye nchi hiyo ikawa mwenyeji Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1984, na uwanja wa Bouake ulijengwa kwa fainali hizo.
Vituo 24 vya mazoezi vimejengwa au kukarabatiwa katika miji mitano. Jengo moja moja la kifakhari la vyumba 32 limejengwa Bouake, San Pedro na Yamoussoukro na hoteli ya vyumba 48 huko Korhogo.
Hospitali za Korhogo na San Pedro zimeboreshwa na viwanja viwili vya ndege - pia vimefanyiwa ukarabati. Barabara kuu kutoka Abidjan - zote mbili za magharibi hadi pwani ya San Pedro, na kaskazini hadi Korhogo zimekarabatiwa.
"Tunajua Ivory Coast ilipitia kipindi kigumu, ambacho hakikuwa rahisi kiuchumi. Lakini Kombe hili limeruhusu Ivory Coast kujitayarisha na miundombinu ya kimichezo na isiyo ya kimichezo," anasema Amichia.
Kutumia vifaa

Chanzo cha picha, Reuters
Shirikisho la kandanda la Ivory Coast (FIF) limekuwa likipanga jinsi ya kushughulikia wasiwasi wa kama Profesa Seraphin juu ya mustakabali wa viwanja vipya vya gharama.
Waliandaa Ligi ya Mabingwa ya Afrika kwa Wanawake mwezi Novemba. Raia wa Ivory Coast wanataka kuwa kituo cha uandaaji wa michezo kikanda - hasa kwa kuwa nchi jirani viwanja vyao vya kitaifa havikidhi vigezo vya kuandaa michezo ya kimataifa.
"Tutahakikisha nchi yetu inakuwa kitovu cha Afrika Magharibi katika masuala ya soka na mashindano ya michezo," alisema rais wa FIF, Idriss Diallo.
"Tutatoa nafasi kwa nchi zote ambazo hazina miundombinu iliyoidhinishwa na Shirikisho la Soka Afrika na Fifa."
Rais Ouattara ana nia ya kuhakikisha ukanda huo una miundombinu bora ya michezo - kupitia mradi wa pamoja na Ufaransa wa kujenga viwanja 10 vidogo vya michezo kote Ivory Coast.
Fursa nzuri kwa biashara

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe - zaidi ya watu milioni moja walikimbia makazi yao, Ivory Coast imepanda kiuchumi.
Shukrani kwa uwekezaji mkubwa wa serikali na rasilimali ya kahawa na kakao. Ivory Coast ni muuzaji mkubwa wa bidhaa hizo duniani. Uchumi wake unaonekana kuwa wa tatu kwa ukubwa Afrika Magharibi - nyuma ya Ghana na Nigeria.
Mwaka 2013, Pato la Taifa la Ivory Coast na Ghana lilikuwa dola za kimarekani bilioni 43 na Ghana 63. Takwimu za IMF za 2022 zinaonyesha Pato la Taifa la Ivory Coast ni 70 bilioni na Ghana bilioni 73.
Katika mji mkuu wa kiuchumi wa Abidjan, mfanyabiashara wa chakula Akouba Angola aliyesoma Marekani wakati wa vita na kurudi 2017 anasema:
“Nilifikiri ulikuwa wakati mwafaka wa kurejea kwa sababu nchi ilikuwa na amani na kila kitu kilikuwa kikienda sawa. Miaka kumi iliyopita kufungua biashara ingekuwa hatari."
Amefungua migahawa mitano tangu 2021 - na sasa anatumai Kombe la Mataifa linaweza kuchochea zaidi uchumi wa Ivory Coast kukuwa.
"Kombe la Mataifa ni fursa nzuri sana kwa biashara, kwa sababu watu wengi wanaokuja kutoka nje watagundua tunachofanya nchini Ivory Coast."
Abidjan inachangia takriban 80% ya uchumi wa nchi. Kombe la Mataifa likiandaliwa - matumaini ni uchumi wa San Pedro, Yamoussoukro na Bouake na Korhogo kukuwa pia.

Chanzo cha picha, BBC Sport
Profesa Seraphin wa Chuo Kikuu cha Alassane Ouattara huko Bouake, anaamini manufaa ya Kombe la Mataifa yatakuwa ya muda mfupi na muda mrefu.
"Faida ya kwanza ya muda mfupi itaongeza mvuto wa Ivory Coast kwa wawekezaji binafsi, kwani macho ya dunia yatakuwa kwetu."
"Pia kutakuwa na biashara nyingi, ajira zitatolewa katika hoteli tunapokaribisha wageni na utalii ambao unawakilisha karibu 9% ya Pato la Taifa."
Seraphin anaamini viwanja vilivyoboreshwa vitawapa raia wa Ivory Coast shauku mpya ya kuhudhuria michezo, haswa kwa kuwa na migahawa na biashara.
"Watu wa Korhogo, Bouake, Yamoussoukro na San Pedro watafaidika na viwanja hivi pamoja na hospitali na vituo vya afya vilivyoboreshwa - na nchi itafaidika na ukarabati huu mkubwa."
Lakini Seraphin anaamini, usalama pamoja na kuondoa msongamano na mechi kwenda bila matatizo yoyote yatakuwa muhimu kwa mafanikio yoyote yale.

Chanzo cha picha, BACKPAGE PIX
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












