Je, Mtume Muhammad aliuteka vipi mji wa Makka na kueneza Uislamu kote duniani ?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Kuna matukio mengi katika historia ya Uislamu ambayo yametengeneza mwezi wa Ramadhani.

Tukio muhimu zaidi ndani yake ni Fatah-e-Makkah (Kutekwa kwa Makka). Baada ya hapo, eneo la Uarabuni lilipata fursa ya kuungana na Uislamu ha ukaenea nje ya eneo hilo.

Kabla ya kujua jinsi ushindi wa Makka ulivyokuwa na jukumu katika kuenea kwa Uislamu, ni muhimu kuelewa umuhimu wa Makka kabla ya Uislamu.

Historia ya Waarabu na Makka kabla ya Uislamu

.

Chanzo cha picha, SEERAT ALBUM, PSO

Makka ni mji wa kati wa Saudi Arabia na kitovu cha kidini na kiroho cha ulimwengu wa Kiislamu.

Mtaalamu maarufu wa mambo ya mashariki kutoka Uholanzi Dozey ameandika kwamba historia ya Makka huanza na wakati wa Mtume Dawood.

Imetajwa pia katika vitabu vya Taurati na Injili (Biblia) za Wayahudi.

Kisha Mtume Ibrahim (Ibrahim) alipokuja Palestina kutoka Misri, aliamrishwa kwenda Makka. Alifika Makka pamoja na mkewe Hajra na mwana wao Ismail.

Inasemekana kuwa aliweka msingi wa Kaaba huko Makka.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kaaba ilijengwa kwa msingi wa jengo la kale. Jengo hilo la zamani linasemekana kuwa moja ya miundo ya kwanza kujengwa kwenye ardhi.

Watu wenye mahitaji walikwenda katika eneo hilo karne nyingi na kutimiza matakwa yao.

Mtume brahim aliijenga upya Kaaba juu ya msingi wa jengo hilo.

Watu wa Bonde la Uarabuni walijiita al-Arab au wakazi wa Bara Arabu. Kwanini walijiita Waarabu haijulikani. Hata hivyo, wengi wao walikuwa wanahamahama jangwani kwa ina Bedouins.

Katika jamii ya kabla ya Uislamu, watu wa jamii ya Badu waligawanyika katika magenge au makabila kadhaa. Wote walikuwa na utawala na desturi tofauti.

Kulingana na kitabu cha Cambridge 'Historia ya Kiislamu', kabla ya Uislamu kulikuwa na falme ndogo na hakukuwa na eneo lililopangwa kisiasa au umoja.

Hata kabla ya kuzaliwa Mtume wa Uislamu, Muhammad, Makka ilikuwa imekuwa kituo kikuu cha biashara. Kwa mujibu wa kitabu cha Cambridge, Makka ilikuwa ikiimarika huku milki za Uajemi na Roma zikidhoofika kutokana na vita vya muda mrefu.

Umuhimu zaidi wa Makka pia ulitokana na Baitullah (Nyumba ya Allah, Kaaba). Misafara ya kibiashara ya kabila la Quraysh ilikuwa ikitoka Yemen hadi Syria na kuleta bidhaa maarufu kutoka nchi mbalimbali na kuziuza huko Makka. Maonyesho makubwa yalifanyika hapa kila mwaka. Mbali na mahitaji, watumwa pia waliuzwa.

Kulingana na kitabu cha Cambridge, umuhimu wa Makka uliongezeka kila mwaka wakati watu walikusanyika hapa wakati wa miezi mitakatifu.

Ukarimu wa watu wa Makka ulikuwa maarufu. Waliwakaribisha wageni wake kana kwamba ni wageni wa Baitullah. Hata wageni waliwaheshimu.

Matukio kabla ya Kutekwa kwa Makka na Hudaibiya

.

Chanzo cha picha, SEERAT ALBUM, PSO

Baada ya msafara kutoka Madina, watu wa Makkah walipigana vita vitatu dhidi ya Waislamu.

Kwa mujibu wa wanahistoria, kitovu cha vuguvugu la chuki dhidi ya Uislamu pia kilikuwa Makka, pamoja na watu wa udugu wa kabila la Quraish.

Katika hali hiyo, Dhulkadah moja (mwezi wa 11 wa kalenda ya Kiislamu) mwaka wa 6 Hijiria (628 AD), Mtume Muhammad pamoja na Maswahabah wake walivaa Ahram (nguo maalum) kwa ajili ya Ziyarat (kwenda kuona) Kaaba na Umrah.

Waarabu walikuwa na mila kwamba mtu akifika Makka akiwa amevaa Ahram, hazuiwi na desturi hiyo ilifuatwa kwa karne nyingi.

Hudaibiya, maili tisa kabla ya Makka, ni mahali ambapo Mtume Muhammad alituma ujumbe kwa udugu wa Kiquraish wa Makka kwamba 'Madhumuni yetu ya kuja hapa ni kuizuru nyumba ya mwenyezi Mungu. Hatukuja kupigana na mtu yeyote.'

Waliposikia ujumbe huu, watu wa Maquraishi walimtuma Urwa bin Mas'ud kwa Waislamu ili kujaribu kuwazuia wasifanye Umra. Hata hivyo, Urwa bin Masoud hakufanikiwa.

Uthman bin Affan (Khalifa wa tatu wa Uislamu) alitumwa kwenda kushauriana na matajiri wa Makka, lakini wakati uvumi ulipoenea kwamba alikuwa amefungwa kwanza na kisha kuuawa, mtume Muhammad alichukua hatua ya kulipiza kisasi pamoja na maswahaba zake, katika vita vilivyojulikana kama Bait-e-Rizwan.

Wakati udugu wa Kiquraish ulipojua kuhusu hatua hii, walituma ujumbe kwamba Uthman alikuwa salama na wakawaahidi Waislamu kwamba wanapaswa kurudi mwaka huu na mwaka ujao kufanya Ziara na Umra ya Kaba.

Watu wa Udugu wa Kiquraish waliahidi kwamba watu wataondoka Makka kwa muda wa siku tatu, ili kuzuia mgogoro wowote. Mapendekezo haya yaliandikwa kwa maandishi. Pia ilijumuisha baadhi ya masharti. Unajulikana kama Sulah-Hudaibiya au Mkataba wa Hudaibia.

Baadhi ya masharti ya mkataba huo kwa hakika yalikuwa dhidi ya Waislamu, lakini Qur'an iliuita mkataba huo Fatah-e-Mubeen (ushindi wa wazi).

Utekaji wa Makka

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Takriban mwaka mmoja baada ya mkataba wa Hudaibiya, baadhi ya matukio yalitokea, ambayo yaliufanya Udugu wa Kiquraishi kutangaza kusitishwa kwa mkataba huo.

Muhammad alipoondoka Madina na maswahaba zake siku ya kumi ya Ramadhani, Hijri nane (AD 630), walikuwa watu 7,000. Msafara huo uliungana na watu kutoka makabila mengine kadhaa wakati wa safari na idadi ya watu katika msafara huo ikafikia 10,000.

Waislamu hao walifika Makka na kupiga kambi eneo la maili kumi kutoka Makka. Wakati habari za kuwasili kwa watu hawa zilipowafikia watu wa kabila la Quraishi wa Makka, kiongozi wao Abu Sufyan alimwendea mtume Muhammad na akatangaza kuukubali Uislamu.

Waislamu waliingia Makka kutoka kila upande na hivyo wakafunga njia ya kutoroka kwa watu wa Makka.

Takriban watu 33-34 waliuawa wakati baadhi yao waliandamana. Mtume Muhammad aliwasili katika Kaaba siku ya Bis Ramzan (11 Januari, 630).

Akiwahutubia watu wa Makka, alisema, “Nyinyi nyote mmekuwa huru. Kuanzia leo hakuna mtu atakayekuuliza. Mwenyezi Mungu akusamehe wewe pia. Yeye ni Mwingi wa kurehemu.”

Mkataba wa Hudaibiya, ambao ulielezewa kuwa ni ushindi wa wazi katika Surah (sura) Fatah ya Qur'ani, ulipatikana wakati huo.

Je, ushindi wa Makka uliwezeshaje kuenea kwa Uislamu?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Encyclopaedia ya Kiislamu inasema kwamba baada ya kutekwa kwa Makka, hofu ya Waquraishi ilitoweka katika akili za watu.

Maquraishi wenyewe walipojisalimisha kwa Uislamu, makundi makubwa na makabila ya Waarabu pia yalianza kuwa Waislamu.

Kwa mujibu wa kitabu cha Cambridge 'Historia ya Kiislamu', kutekwa kwa Makka na ushindi uliofuata katika Vita vya Hunain kulimaanisha kwamba hapakuwa na makabila yenye nguvu yaliyosalia kuwapinga Waislamu.

Hivyobasi Mtume Muhammad alipata heshima ya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi katika eneo hilo.

Kulingana na kitabu cha Cambridge, Waarabu waliheshimu mamlaka. Hivyo wakaanza kusilimu kwa makundi.

Kwa hiyo ushindi wa Makkah ulipatia eneo la Waarabu kiongozi ambaye uongozi wake ulikuwa wa kidini pekee. Wapiganaji wa Kiarabu sasa waliishi chini ya mwavuli wa kiongozi mmoja na dini moja.

Kwa mujibu wa kitabu 'Historia ya Kiislamu', jumuiya hiyo iliundwa ambayo wanachama wake walifurahia amani baada ya muda mrefu na kwa upande mwingine masultani wenye nguvu wa Uajemi na Rumi walidhoofika.

Kitabu hicho kinasema kwamba mfululizo wa ushindi ulianza kuzuia nguvu za wapiganaji wa Kiarabu kuvuruga amani ya Peninsula ya Arabia. Alisaidia kueneza Uislamu kwa jumuiya iliyopangwa ya Waarabu.

Kitabu cha Cambridge kinasema kwamba muda mrefu kabla ya kutekwa kwa Makka, mtume Muhammad aliona kwamba wakati ungefika ambapo kungekuwa na watu wachache sana wasio Waislamu waliosalia katika Rasi ya Arabia.

Kwa hivyo Uislamu utalazimika kuondoka kwenye rasi ya Arabia na kuelekea Iraq na Syria. Lazima alikisia kwamba ingehitaji mipango mingi na watu wenye uwezo wa kiutawala.

Kwa mujibu wa 'Historia ya Kiislamu', kulikuwa na watu wengi kama hao huko Makka ambao walikuwa na ujuzi na uzoefu wa kupanga misafara ya biashara ya masafa marefu.

Kwa mujibu wa kitabu cha Cambridge, majenerali na wasimamizi wengi waliofanikisha kuenea kwa taifa hilo jipya la Kiislamu walihusishwa na miji mitatu katika eneo la Hijaz. Inajumuisha Makka, Madina na Taaf.

Hivyo, baada ya kutekwa kwa Makka, wengi wa wale Waislamu wapya na vizazi vyao wakawa wanafikra, Mujahidina, na Maulamaa. Alieneza ujumbe wa Uislamu sehemu mbali mbali na akainua bendera ya Uislamu nchini Iraq, Iran, Syria na Afrika.

Baada ya kifo cha Mtume Muhammad, hadhi ya Makka kama mji mkuu ilidumishwa. Makka inakuwa kituo cha kidini, kiroho na kielimu kwa sababu ya Hijja.

Katika kipindi cha Banu Umayyad, kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu kilihama kutoka Madina hadi mji mkuu wa Syria, Damascus. Hata hivyo, hadhi kuu ya Makka na Madina ilidumishwa.

Watu walikuwa wakija kutoka sehemu mbali mbali ili kukata kiu ya kiroho na kielimu.

Hali kuu ya kiroho ya Makka bado haijabadilika hadi leo na kwamba kila Muislamu duniani anaswali akitazama Kaaba.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi