"Nampenda mpenzi wa Mamangu ndio maana nilimuua Mama"

Chanzo cha picha, Getty Image
“Mpenzi wa mama yangu ni mkubwa kwangu mara mbili kiumri. Lakini, nilimpenda. Nilimpenda. Siku moja mama yangu alitufuma. Ndiyo sababu niliamua kumuua mama yangu. Alikuwa kikwazo kwa mapenzi yetu."
Haya ni maneno ya Tina (jina lake tumelibadilisha) baada ya kunaswa na polisi. Tina sasa yuko katika kizuizi cha watoto. Tunaficha jina lake ili utambulisho wake usijuulikane. BBC ilizungumza naye kwa usaidizi wa mshauri.
Polisi wa Mudra Sagari, India walimkamata Tina na mpenzi wake Yogesh Jothia. Wote wawili wanatuhumiwa kumuua Geetha mwenye umri wa miaka 38 (jina limebadilishwa pia). Geetha aliuawa na mwili wake ukatupwa baharini karibu na kijiji cha Hamir More huko Kutch.
Katika kesi hii binti wa Geetha, Tina, pamoja na Yogesh Jothia na mtu mwingine aitwaye Naren Jogi walikamatwa.
Wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo, polisi waligundua kuwa Geetha alikuwa na uhusiano wa nje ya ndoa na Yogesh Jothia. Lakini, binti yake Tina pia alikuwa na uhusiano na Yogesh.
Geetha alipogundua kuhusu uhusiano wa Tina na Yogesh, wawili hao walipanga njama ya kumuua Geetha. Lakini, wote wawili walikamatwa na polisi kupitia mazungumzo ya simu.
Geetha ni nani?

Chanzo cha picha, KACHCHH MITRA
Geetha alizaliwa na kukulia Ahmedabad. Mwanamke anayeishi karibu na nyumba ya Geetha aliiambia BBC kuhusu marehemu. Alizaliwa katika familia maskini - wahunzi. Alilazimika kufanya kazi tangu utotoni kwa sababu ya umaskini.
‘’Geetha aliolewa na Kishore Vekaria, mkandarasi. Wana watoto wanne - wavulana watatu na msichana mmoja. Baada ya watoto kuzaliwa, waliachana. Baadaye, Geetha alikwenda kwa dadake anayeishi Kutch,'' anasimulia mwanamke huyo.
Alipofika Kutch, Geetha akapendana na mwanaume kwa jina la Jitendra Bhatt. Baadaye walifunga ndoa. Geetha alikuwa amewachukua watoto wake wawili kati ya wanne. Mmoja ni mvulana wa miaka sita na mwingine ni msichana wa miaka minane.
Geetha na Jitendra waliamua kuwalea watoto hawa wawili pamoja. Walifunga ndoa miaka tisa iliyopita. Lakini maisha yao yalibadilika bila kutarajia.
Jitendra Bhatt anazungumza na BBC kuhusu siku za uchungu za maisha yake.
"Tulipokuwa tukifanya kazi ya kupaka rangi huko Madapar, tulikutana na Yogesh Jothia. Yogesh na mke wangu walikuwa wakikutana kwa siri nilipokwenda kazini. Tina pia alinificha jambo hilo,” anaeleza Jitendra.
Kuuawa kwa Geetha

Chanzo cha picha, Getty Image
Mapenzi ya Geetha na Yogesh yalipoanza, pia Tina akawa na uhusiano na mwanaume huyohuyo. Yogesh alikuwa na mahusiano na mama na binti. Kulikuwa na vita kati ya Geetha na Tina juu ya suala hili.
Niliporudi nyumbani kutoka kazini Julai 10, Tina aliniambia kwamba Geetha amekwenda katika mji wa Anjar. Baada ya siku 20 hakurudi nyumbani na simu yake haipatikani.
Nilifungua kesi ya kutoweka kwake katika kituo cha polisi cha Madapar. Siku moja picha ya maiti iliyopatikana karibu na fukwe huko Mundra ilitumwa katika kituo cha polisi cha Madapar.
Ndio tukajua kuwa Geetha amefariki. Jitendra anasema mwili wa Geetha ulitambuliwa kwa nguo zake.
“Nilimtambua Geetha nilipoona nguo nyeusi aliyokuwa amevaa. Nilipoona cheni, mkufu na kidani shingoni mwake, nilimtambua kuwa ni Geetha,” anasema Jitendra.
Simu ilivyofichua wauaji

Chanzo cha picha, Getty Image
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maelezo ya kesi hii yalifichuliwa na Inspekta Jadeja wa Kituo cha Polisi cha Mundra.
"Julai 13, maiti ya mwanamke ambaye hakutambuliwa ilipatikana karibu na kijiji cha Hamir Mora. Juhudi zetu za kuutambua mwili huo hazikufaulu. Baadaye tulituma picha za maiti katika vituo vyote vya polisi vya Kutch. Baada ya siku 17 tulipata taarifa juu ya maiti huyo,” anasema Jadeja.
"Taarifa kupitia mnara wa simu ilifichua kuwa simu ilipigwa kwa mtu anayeitwa Naren Jogi kutoka eneo hili saa 3:18 usiku," Jadeja anasimulia.
"Yogesh alikuja hapa na gari la Wagon-R kutoka Madapar. Kisha alinipigia simu usiku wakati gari likiwa limekwama kwenye mchanga. Nikaja na nilipokuwa nikimsaidia, niliona msichana mdogo kwenye gari lake,” Naren Jogi aliambia polisi.
Polisi walipokusanya maelezo ya simu za Naren Jogi, iligundua kwamba Yogesh Jothia alimpigia simu Julai 10.
Yogesh alimleta mpenzi wake Geetha na bintiye Tina kwenye eneo hili kwa matembezi. Geetha na Yogesh walipigana, wakati Gethaa alipomwambia Yogesh aachane na Tina.
''Kisha wakahamia mahali palipojificha kidogo. Hapo Geetha aliuawa na kutupwa baharini na wakaondoka. Hata hivyo, gari lao lilikwama kwenye mchanga. Walinipigia simu usiku. Nikaenda na nikawasaidia kulitoa gari. Kutoka hapo tulimwacha Tina mahali na sisi kwenda Madapar,'' alieleza Naren.
Simu ya Yogesh kwa Naren usiku iliwapa polisi fununu juu ya mauaji hayo. Kwa msaada wa Naren, washtakiwa walikamatwa. Muda mfupi baada ya Tina na Yogesh kukamatwa, walikiri mauaji hayo.
PSI Jadeja alisema, "Yogesh alisema kwenye taarifa kwamba Geetha alikuwa akimshinikiza Tina kumaliza uhusiano na naye. Kwa pamoja walipanga kumpeleka Geetha mahali pasipokuwa na watu umbali wa masaa manne na kumuua.''
BBC ilijaribu kuwasiliana na kakake Geetha, anayeishi Ahmedabad. Lakini alikataa kuzungumza juu yake.












