Je, Israel inatoa silaha kwa kundi la ISIS?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Upinzani wa Israel umeishutumu serikali kwa kulipatia silaha kundi lenye uhusiano na ISIS huko Gaza. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema, "Kuna ubaya gani katika hilo?"

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alithibitisha kuwa Israel inazipa silaha jamii za Gaza ambazo zinapinga Hamas.

Kauli yake imejiri baada ya vyombo vya habari vya Israel kuripoti, vikinukuu vyanzo vya Wizara ya Ulinzi, kwamba Netanyahu ameidhinisha ugavi wa silaha kwa kundi maalum kusini mwa Gaza.

Wanasiasa kadhaa wa Israel walimtuhumu Netanyahu kwa kutishia usalama wa nchi.

"Kuna ubaya gani?" Netanyahu alisema katika ujumbe wa video kwenye mitandao ya kijamii. "Inaokoa tu maisha ya wanajeshi wa Israel. Kuzungumza juu yake kwa uwazi kunanufaisha tu Hamas."

Waziri Mkuu huyo alikuwa akizungumzia ripoti kwamba Israel imetoa silaha kwa kundi linaloongozwa na Yassir Abu Shabab huko Gaza kwa amri yake binafsi.

Ingawa wengine wanalichukulia kundi hili kuwa la wanamgambo au wahalifu, linajionyesha kama kikosi cha upinzani kwa Hamas.

Kulingana na kundi hilo, lengo lao ni kulinda malori yanayoleta misaada Gaza. Lakini wakosoaji wanasema kundi hilo kwa hakika linaiba magari ya misaada.

Ingawa Benjamin Netanyahu hakuchukua taarifa hizi zilizovuja kwa uzito, zinaweza kusababisha mzozo mpya wa kisiasa.

Vyanzo vya Wizara ya Ulinzi ya Israel hapo awali vilithibitisha kwa waandishi wa habari wa ndani kwamba madai ya kiongozi wa upinzani Avigdor Lieberman yalikuwa ya kweli.

Lieberman, kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu, aliiambia Kan TV kwamba Netanyahu aliidhinisha kwa upande mmoja utoaji wa silaha kwa kundi la Abu Shabab.

"Serikali ya Israel inawapa silaha kundi la wahalifu na watu wenye jeuri wanaohusishwa na Islamic State (ISIS). Kulingana na taarifa yangu, uamuzi huu haukuidhinishwa na baraza la mawaziri," Lieberman alisema.

Kulingana na duru za Wizara ya Ulinzi, Israel iliuhami ukoo wa Abu Shabab kwa bunduki za kivita za Kalashnikov, ambazo baadhi yake zilinaswa kutoka kwa Hamas.

Jamii hii inafanya kazi huko Rafah, eneo lililo chini ya udhibiti wa kijeshi wa Israeli.

Hata hivyo, Yasser Abu Shabaab aliingia kwenye mitandao ya kijamii "kukanusha kabisa" kwamba kundi lake lilikuwa limepokea silaha kutoka kwa Israel.

"Silaha zetu ni rahisi, zimepitwa na wakati na zilikuja tu kwa msaada wa watu wetu," alisema.

Duru za Hamas zinasema kuwa shughuli za kundi la Abu Shabab zimekuwa tatizo. Kwa mujibu wa ripoti katika gazeti la Kiarabu, tawi la kijeshi la Hamas limeanza kuwaua watu wa ukoo huo.

Ofisi ya Netanyahu ilisema kuwa Israel "inafanya kazi ya kuishinda Hamas kupitia njia mbalimbali kulingana na mapendekezo ya wakuu wa vitengo vyote vya usalama."

Mpango huu ulikosolewa vikali na Yair Goland, kiongozi wa Democrats katika Knesset.

Aliandika katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii: "Netanyahu ni tishio kwa usalama wa taifa la Israel. Badala ya kufikia amani ... kuwarudisha wafungwa nyumbani na kuhakikisha usalama wa raia wa Israel, anaandaa 'bomu jipya' huko Gaza."

Imetafsiriwa na Seif Abdalla