Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Fine Water', maji ya bei ghali na ya kifahari yanayotumiwa sana na matajiri
Na Suneth Perera
BBC News
Je Umewahi kusikia kuhusu mgahawa ambao hutoa orodha ya maji ya kifahari badala ya divai nzuri, au harusi inayofurahisha wanandoa kwa maji ya kupendeza badala ya champagne au juisi ya matunda?
Maji katika tunayozungumzia hapa ni ghali kuliko kuliko yale ya kawaida ya madini au yale ya bomba, na chupa moja ya maji hayo inaweza kukugarimu mamia ya dola.
Yanaweza hata kutolewa kwa pamoja na chakula – kuanzia nyama hadi samaki – kama inavyokuwa kwa divai.
Vinywaji hivi vya bei kali vinajulikana kama maji mazuri (fine water)na hutoka kwa vyanzo vya asili kama vile miamba ya volkano, barafu inayoyeyuka kutoka theruji, au matone ya ukungu. Maji haya yanaweza hata kutolewa moja kwa moja kutoka kwenye mawingu.
Kila maji yatakuwa na sifa za mahali yanakotoka, na tofauti na maji ya kawaida ya chupa, hayachakatwa kabisa.
Sasa kuna mamia ya bidhaa nzuri za maji ulimwenguni kote, na kuna hata wataalam ambao wanaweza kukupa ushauri juu maji haya adimu.
Je, maji haya yana ladha?
Kama vile mvinyo unavyoonjwa, pia kuna watu maalum ambao kazi yao ni kuonja na kutathmini kila bidhaa ya maji haya na kutofautisha katika suala la madini, ladha, na mouthfeel.
"Maji sio maji tu. Kila maji katika dunia yetu ni tofauti na yana ladha," anasema Milin Patel, mshauri wa maji na muonjaji ambaye anaendesha duka la pop-up mjini London.
Anaendesha vikao vya kuonja kwa watu wanaopenda kuchunguza maji haya , ikiwa ni pamoja na aina za maji ya bomba na chupa.
Patel ameiambia BBC kuwa amedhamiria kuwaelimisha watu hasa kizazi kipya kuhusu aina mbalimbali za maji na ladha yake.
"Kumbuka shuleni, tulijifunza kuhusu mzunguko wa asili wa hmaji - uvukizi, mkazo, na mvua. Hata hivyo, tulikosa kipengele kimoja – remineralization [Urejeshaji wa madini mwilini ambao hutokea wakati madini muhimu—kama vile kalsiamu yanapoungana kwenye meno ili kujaza sehemu zilizo dhaifu za ufizi ]," alisema.
"Kwa hiyo, mara mvua inaponyesha ardhini, hufyonza na kisha kupenya kupitia miamba na udongo tofauti ili kutoa madini kama vile kalsiamu, magnesiamu, potasiamu, silica, n.k. Mchakato huu ndio unaotoa maji ladha yake ya madini," Patel aliongeza.
Maji kutoka vyanzo kama barafu au mvua, ambayo kwa kawaida haijapita ardhini, kwa kawaida huwa na kiwango cha chini cha vitu kama vile barafu zilizoyeyuka (TDS) ikilinganishwa na maji kutoka chemchemi na visima.
Patel ana mkusanyiko wa maji tofauti kutoka duniani kote, kuanzia maji ya bomba hadi maji mazuri ambayo hugharimu hadi £ 250 ($ 318) kwa chupa. Baada ya watu kuyaonja katika, hujaribu kuelezea jinsi kila maji yanavyoonja kivyake.
"Tunawapa watu fursa ya kuona maji sio tu kama ladha. Unapoanza kuchunguza na kunywa maji kwa uangalifu, unaweza kushangazwa na misamiati ya kuchangamsha ," Patel alielezea. "Tunapata misamiati hii mizuri kutoka kwa waonjaji wakisema - maji ni laini, yana ladha kama ya krimu, yana utamu , machungu, na wakati mwingine husema ni machachu."
"Na watu wengi mara nyingi husema - 'Oh, ladha hii hii inanikumbusha nilipokuwa mdogo', 'hii inanikumbusha likizo' au 'hii inanikumbusha nyumba ya babu yangu'," aliongeza.
Mashindano ya kuonja maji
Jumuiya ya Maji ya Mazuri (Fine Water) hufanya mkutano kila mwaka, ukiwajumuisha pamoja wazalishaji bora wa maji hayo kutoka duniani kote – kuanzia Bhutan hadi Ecuador - na mwenyeji wa mashindano ya kimataifa ya kuonja.
Wengi wa wale wanaohudhuria mkutano wa kila mwaka hutoka katika biashara zinazoendeshwa na familia zinazozalisha maji kutoka maeneo ya mbali.
"Kuonja maji kulichukuliwa kuwa wazo la ujinga sana mwanzoni," anasema mwanzilishi mwenza wa Jumuiya ya Fine Water na chui cha maji hayo, Dk Michael Mascha.
"Nilianza mchakato mzima miaka 20 iliyopita wakati nilipolazimika kuacha kunywa pombe," aliiambia BBC. "Wakati divai ilipoondolewa ghafla, niliangalia mezani, na ghafla kulikuwa na chupa nyingine ambayo sikuwa nimeiona hapo awali, ambayo ilikuwa ya maji. Nilidhani labda ninaweza kutumia udadisi wangu na kuitumia kwa kunywa maji badala ya divai," aliongeza.
Maji mazuri hutoa kitu zaidi ya maji tu, anaamini: ni fursa kwa watu kuchunguza, kushiriki, na kufurahia kitu tofauti, na unaweza kufanya hivyo hata na watoto, kitu ambacho huwezi kukifanya kwa divai.
Kwa sasa kuna ongezeko la mahitaji ya maji safi, Dk Mascha anadai, na anaamini kuwa unasukumwa na mwenendo wa kutumia pombe kidogo na vinywaji laini vya kaboni, hasa miongoni mwa kizazi cha vijana ambacho ni muhimu kiafya.
Zaidi ya hayo, maji haya adimu, yanaweza kuuzwa na hadithi kuyahusu sawa na divai, jambo ambalo husaidia kuyafanya yawe yenye mvuto zaidi.
Maji na chakula
Baadhi ya migahawa katika nchi kama Uhispania na Marekani sasa inatoa menyu ambazo zinaunganisha aina maalum za maji mazuri wakiambatanisha vyakula vyao.
"Kwa sasa ninatengeneza orodha ya maji kwa ajili ya mgahawa wa nyota tatu wa Michelin nchini Marekani. Tunapanga kuwa na maji 12 hadi 15 yaliyohifadhiwa kwa uangalifu ambayo yanasaidia muonekano wa chakula , "anasema Dk Mascha.
"Unapokuwa na samaki, utahudumiwa maji tofauti na wakati unakula nyama. Unahitaji kuwa na madini ya chini ili kuepuka kuingilia kati madini yaliyomo katika samaki."
Dk Mascha pia anafanya kazi na nyumba za kifahari na miradi ya ghorofa ambayo itakuwa na 'vyumba vya uzoefu wa maji' badala ya divai.
Maji safi pia ni maarufu miongoni mwa tamaduni zinazoepuka pombe kwa sababu za kidini, Dk Mascha anabainisha, hasa katika harusi. Pia ni zawadi nzuri mbadala kuchukua nafasi ya champagne ya gharama kubwa, anadai.
Lakini hali hiyo, bila shaka, ina wakosoaji wake.
'Makosa ya kimaadili'
Kuna mamilioni ya watu duniani kote ambao wanahangaika kupata maji safi, na wengi hupinga wazo la kupata mapato ya bidhaa za msingi kwa njia hii.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mwaka 2022, watu bilioni 2.2 bado hawana maji safi ya kunywa, ikiwa ni pamoja na milioni 703 ambao wanaishi bila hata huduma ya msingi ya maji.
Wakosoaji wengine wanasema kuwa mtindo huu ni wizi tu; Maji ni maji tu na hakuna tofauti katika maji ya bomba ya kunywa, maji ya chupa na kinachojulikana kama maji mazuri (Fine Water) isipokuwa bei yake, wakati wanamazingira wanasema kuwa aina yoyote ya maji ya chupa yanaharibu sayari yetu kwani huishia kuwa takataka au katika taka za ardhi.
Carolyn Roberts, Profesa Mazingira katika Chuo cha Gresham, London, anaamini ni kinyume cha maadili kutumia mamia ya dola kwa chupa ya maji, wakati mamilioni ya watu wanahangaika kupata maji safi.
"Ni kama kuonyesha utajiri wako wakati unaenda nje kwa chakula cha jioni na watu. Ikiwa unasema, 'Naam, ninalipa chupa hii nzuri ya maji ambayo imesafirishwa kutoka Antarctica au mahali fulani huko Hawaii,' watu wanaweza kujisikia vizuri juu ya hilo. Hata hivyo, kwa kweli, hakuna faida kwa mtu yeyote. Yote ni kuhusu fedha," aliiambia BBC.
"Pia, muhimu zaidi, ni uharibifu wa mazingira. Iwe ni plastiki ambazo zinaharibika na kuwa vipande vipande, zinazohitaji mafuta kwa ajili ya uzalishaji, au glasi ambayo ni nzito sana na inahitaji kusafirishwa maelfu ya maili kutoka maeneo ya mbali, na kusababisha athari mbaya kwa uzalishaji wa kaboni, "alisema.
"Kwa hiyo, sio tu kuhusu fedha. Pia ni kuhusu uharibifu wa mazingira ambao haya yanayoitwa maji mazuri husababisha."
Lakini Dk Mascha anasema kuwa maji mazuri yanazalishwa sio tu kwa matajiri kwani kuna maji mazuri yenye ubora ambayo yanagharimu dola 2 tu.
"Kwa mtazamo endelevu, haina maana kuweka maji ya bomba yaliyosindikwa kwenye chupa ya plastiki. Unaendesha gari na kubeba chupa za plastiki nyumbani, kunywa, na kutupa chupa. Ni jambo la kusikitisha sana."
Badala ya kutumia maji ya chupa yaliyosindikwa, anapendekeza kutumia maji ya bomba kwa ajili ya maji.
"Mara nyingi tunasahau kuwa na maji ya bomba ya kunywa ni fursa ambayo watu wengi ulimwenguni hawana," alihitimisha.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi