Ndoa ya kisiasa ya Raila na Ruto itabadili vipi siasa za Kenya?

Chanzo cha picha, Ikulu/Kenya
- Author, Na Laillah Mohammed
- Akiripoti kutoka, BBC News Swahili, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Raila Odinga, ambaye amekuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya kwa miaka mingi, sio mgeni katika mchezo wa karata za kisiasa za ndani na nje ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Katika zaidi ya miaka arobaini katika siasa, kiongozi huyo wa chama wa Orange Democratic Movement (ODM) amefanya maamuzi ya kisiasa yaliyowaacha wengi vinywa wazi, kwani wengi hawakutarajia, na kuwaacha raia wa kawaida na wadadisi wa kisiasa wakijaribu kutathmini maana ya maamuzi hayo na athari zake.
Ndoa ya kisiasa iliyobuniwa Ijumaa Machi 7, 2025 kati yake na Rais William Ruto, ambaye ni mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na vyama vyao viwili imezua maoni mseto.
"Huu ni usaliti kwa Wakenya," alisema kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka ambaye amekuwa mgombea mwenza wa Odinga katika chaguzi mbili (2013 na 2017), na pia alikuwa makamu wa rais wa taifa hilo (2008-2013).
Miongoni mwa raia, hisia zimegawanyika kuhusu iwapo hili litakuwa na manufaa kwao au la.
"Mimi nawaunga mkono kwa asilimia mia moja. Kwa sababu hawa watu wamezungumza kwa kinaga ubaga jinsi watakavyoendeleza Kenya", alisema William Onyango. Mkazi wa Nairobi.
Kwa upande wake, Amina Mohammed ambaye ni mkazi wa Kiamaiko mjini Nairobi amepinga.
"Sasa hata kama Ruto anashikana na Raila, sioni kitu cha maana hapo. Ila, sisi tunaumia kwa ndani, wamama na vijana tunaumia. Hakuna mtu ambaye anatusaidia katika mahangaiko yetu. Tunajenga Ruto atusaidie, atuangalie, atulinde, lakini vijana wakipigania haki yao, wanakabiliwa na risasi, na watoto wetu wanauawa", alisema Amina.
Ishara ya kwamba vyama vya ODM na UDA vilikuwa na mpango wa kuungana kisiasa ilionekana katika ikulu ndogo ya Mombasa, siku chache tu baada ya Ruto na Raila kurejea nyumbani kutoka Addis Ababa, Ethiopia ambapo Raila alishindwa katika kinyang'anyiro cha kuwania uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC, kiti alichokipata Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti.
Katika mkataba huu mpya na rais Ruto, Bw Raila amewapungia mkono viongozi aliokuwa nao katika muungano wa Azimio la Azimio la Umoja–One Kenya ambao alitumia kuwania kiti cha urais mwaka 2022.
Sasa amemrejelea Ruto ambaye mnamo 2007 alikuwa mojawapo ya viongozi wakuu wa ODM. Katika uchaguzi wa 2013, Ruto alimtema Raila na kujiunga na Uhuru Kenyatta kama mgombea mwenza, ambapo walitwaa ushindi.
Uchaguzi wa 2017 ulikumbwa na madai ya wiz iwa kura, na ulibatilishwa na mahakama ya upeo na kulazimika kufanyika tena, hatua ambayo Odinga alisusia kushiriki na kuitisha maandamano baada ya Kenyatta kutangazwa mshindi.
Kufuatia ghasia na maandamano ya 2018, ambapo Odinga 'alijiapisha' mjini Nairobi, kiongozi huyo aliingia katika makubaliano ya kisiasa na Rais Kenyatta maarufu kama 'handsheki'.
Hatua hii ilionekana kumtenga Ruto kama mwandani wa Kenyatta. Kwa kuhofia kurejelewa kwa hali kama hii, Rigathi Gachagua ambaye alikuwa naibu wa Ruto katika uchaguzi wa 2022, alisisitiza kwamba hawataruhusu 'serikali ya nusu mkate' kutokea katika serikali mpya chini ya muungano uliofahamika kama 'Kenya Kwanza'.
Miaka miwili baadaye, Rigathi aliondolewa uongozini, na kwa mara nyingine tena Odinga amejipata ndani ya serikali.
Historia ya mikataba ya Bw Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images
Raila sio mgeni kwa ushirikiano wa aina hii wa kisiasa. Baada ya ghasia za wenyewe kwa wenyewe za mwaka 2008, alibuni serikali mseto na Rais Mwai Kibaki, ambapo Bw Odinga aliteuliwa kama Waziri Mkuu.
Kabla ya Kibaki, aliwahi pia kujipata katika ndoa ya kisiasa na Rais Daniel Toroitich arap Moi mnamo 2001, kabla ya kujiondoa haraka na kubuni muungano wa NARC uliomzuia Uhuru Kenyatta kumrithi Moi katika uchaguzi mkuu wa 2002
Muungano wa Ruto na Raila unamaanisha nini?

Chanzo cha picha, Ikulu/Kenya
Wakili Alutalala Mukhwana anasema kwamba ili kurejesha imani ya Wakenya katika uongozi wa taifa, ni sharti viongozi hao wawili wayape kipaumbele mapendekezo ya ripoti ya kamati ya kitaifa ya mazungumzo NADCO ambayo ilitolewa baada ya maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2022.
"Ripoti hiyo ilipendekeza kuwepo kwa nafasi ya Waziri Mkuu, na nafasi rasmi ya kiongozi wa upinzani. Kwa hivyo kwa ujumla, serikali itabadilika. Na msimamo wa viongozi hawa wawili ni kwamba sharti yaliyokuwa yamependekezwa katika ripoti hiyo yatekelezwe," Mukhwana aliiambia BBC.
Katika katiba mpya ya 2010, ofisi za Waziri Mkuu na kiongozi wa upinzani bungeni ziliondolewa, na sasa mgombea wa urais hawanii kiti cha Ubunge pia. Hii ilileta taswira ya 'winner-takes-it-all' yaani mshindi anapata vyote na kuwaacha walioshindana naye bila chochote na kulazimika kusalia kwa kibaridi kikali kwa miaka mitano.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, siasa za upinzani zimekufa Kenya?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya Wakenya wanahisi kwamba katika kuungana mkono na rais Ruto, Bw Odinga ambaye wengi walimtarajia awajibikie jukumu la kuhakikisha uadilifu serikalini sasa amevuka sakafu na kujiunga na serikali, na kuwaacha wananchi bila ya mtetezi.
Mchambuzi wa kisiasa Javas Bigambo hata hivyo anapinga wazo hili, akisisitiza kwamba katiba ya Kenya inampa kila raia uwezo wa kuiwajibisha serikali.
"Zaidi ya hayo kunao viongozi wengine wa kisiasa ambao wanaweza kuzungumza kwa niaba ya wakenya na kuwatetea, bungeni au hata nje ya bungee," Bigambo aliiambia BBC.
Bigambo anasema kwa sasa cha muhimu ni kuona ikiwa masuala kumi kuu yaliyoorodheshwa katika makubaliaono kati ya ODM na UDA yataafikiwa.
"Suala la kwanza kuitaka ripoti ya NADCO kutekelezwa kikamilifu – yaani kubuniwa kwa afisi hizo mbili za kisiasa - itahitaji kura ya maoni kuandaliwa. Kwa sasa sidhani kama Bw. Ruto ana uwezo wa kuandaa kura hiyo kwa sababu mbali mbali muhimu" aliongeza.
Masuala mengine katika mkataba huo wa makubaliano ni deni la taifa, huku pande zote zikipendekeza ukaguzi wa kina kutathmini lina ukubwa kiasi gani na ni fedha ngapi ambazo zimetumika hadi sasa. Lingine ni kusitishwa kwa uharibifu wa fedha, na kukomeshwa kwa ufisadi.
Katika mitandao ya kijamii, vijana nchini Kenya almaarufu Gen Z wamehakikisha sauti yao inasikika wakiishinikiza serikali kuwajibikia uongozi bora na kupinga ufisadi.
Kilele cha ghadhabu yao ilikuwa maandamano na kuvamia majengo ya bunge la taifa mnamo Juni 25, 2024, wakiwataka wabunge kutopitisha mswada wa fedha ambao walihisi unawakandamiza kiuchumi.
Hanifa Adan ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa maandamano ya vijana Kenya, aliandika katika ukurasa wake wa X mapema wiki hii kwamba "vijana hawatopunguza kasi yao hasa ikizingatiwa kwamba uongozi wa taifa unazidi kuonyesha kiburi kwa matamshi na vitendo vyao."
Imehaririwa na Peter Mwangangi












