Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ni nini na kwa nini inasikiliza kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel?
- Author, Aine Gallagher
- Nafasi, BBC News
Ni kesi ya mahakama ya karne.
Alhamisi hii, Januari 11 na Ijumaa, Januari 12, mawakili wanaowakilisha Afrika Kusini na Israel watafika mbele ya mahakamani ya kimataifa ya haki.
Je, Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Walestina huko Gaza?
Afrika Kusini inasema ndiyo ndiposa ikawasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague mnamo Desemba 29, 2023.
Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema nchi yake inaishi kwa "maadili" yasiyo na kifani katika kampeni yake ya Gaza, wakati msemaji wa serikali alifananisha kesi ya Afrika Kusini na "kashfa ya damu," shutuma za uongo. kwamba Wayahudi waliwaua Wakristo ili kutumia damu yao katika desturi za kale.
Yafuatayo ni maswali 11 yatakayokusaida kuelewa shtaka la mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini dhidi ya Israel.
1. Kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini inasema nini?
Waraka huo wa kurasa 84 uliowasilishwa na Afrika Kusini unasema kwamba hatua za Israel "ni za mauaji ya halaiki kwa sababu zinataka kusababisha uharibifu wa sehemu kubwa" ya Wapalestina huko Gaza.
Inashikilia kuwa vitendo vya mauaji ya halaiki ni pamoja na kuwaua Wapalestina, na kusababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili, na kuweka kimakusudi masharti yaliyokusudiwa "kuleta uharibifu wao wa kimwili kama kikundi." Inasisitiza zaidi kuwa matamshi ya maafisa wa Israel yanaeleza nia ya mauaji ya kimbari.
Juliette McIntyre, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Australia Kusini, aliambia BBC kwamba ombi la Afrika Kusini ni "la kina sana" na "imetungwa kwa uangalifu sana."
"Inatafuta kujibu hoja zote zinazowezekana za Israel... na kushughulikia madai yoyote ambayo mahakama inaweza kushughukia au kukosa mamlaka ya kufanya hivyo," alisema.
"Afrika Kusini inasema iliibua suala hilo na Israel katika majukwaa mengi tofauti kabla ya kuleta kesi hiyo," msomi huyo aliongeza.
2. Je, jibu la Israel limekuwa nini?
Msemaji wa serikali ya Israel Eylon Levy amesema Israel itatetea msimamo wake kuhusu kesi hiyo.
Pia alisema kuwa Hamas ndio inastahili kulaumiwa kwa kuanzisha vita vita hivyo.
3. Mauaji ya kimbari ni nini?
Chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya Umoja wa Mataifa wa 1948, ni kitendo kilichofanywa kwa nia ya kuangamiza kwa ujumla au sehemu kikundi cha kitaifa, kikabila, rangi au kidini, ambacho kinahusisha:
• Kuwaua washiriki wa kikundi
• Kusababisha madhara makubwa ya mwili au kiakili kwa washiriki wa kikundi
• Kuweka makusudi hali ya maisha ya kikundi inayokokotolewa kuleta uharibifu wake wa kimwili kwa ujumla au sehemu.
• Kuweka hatua zinazokusudiwa kuzuia uzazi ndani ya kikundi
• Kuhamisha watoto wa kikundi kwa kundi jingine
4. Nani anaweza kushtakiwa kwa mauaji ya halaiki?
Nchi au mtu anaweza kutuhumiwa kwa mauaji ya kimbari.
Michael Becker, profesa msaidizi wa sheria katika Chuo cha Trinity Dublin, anasema kuna tofauti kati ya kupata taifa linalokiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari na kupata mtu na hatia ya kufanya mauaji ya halaiki.
5. Je, ni nini jukumu la Mahakama ya Kimataifa ya Haki?
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ndiyo mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa ambayo huamua mizozo kati ya mataifa.
Wanachama wote wa UN ni wanachama wa ICJ moja kwa moja.
Taifa lazima lipeleke kesi kwa ICJ, ambayo inaundwa na majaji 15 waliochaguliwa kwa muhula wa miaka tisa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama.
Sehemu ya mamlaka ya mahakama ni kusikiliza mizozo inayohusiana na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948.
Mkataba huo ulipitishwa baada ya Wayahudi milioni sita kuuawa na Wanazi huko Uropa wakati wa Vita vya Kidunia vya pili, kati ya 1939 na 1945.
Israel, Afrika Kusini, Myanmar, Urusi na Marekani ni baadhi ya nchi 153 zilizoidhinisha.
6. Kuna tofauti gani kati ya ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu?
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilianzishwa mwaka 2002 na pia iko mjini The Hague.
Ni mahakama ya mwisho ambayo hufanya kazi tu wakati mahakama ya kitaifa haifanyi hivyo. Marekani, Urusi na Israel si wanachama.
ICC inashughulikia kesi za jinai na inaweza kumtia hatiani mtu kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki. Kila mmoja ana ufafanuzi tofauti katika sheria.
7. Nani amehukumiwa kwa mauaji ya kimbari?
Mtu wa kwanza kupatikana na hatia ya mauaji ya halaiki alikuwa Mnyarwanda Jean-Paul Akayesu, mwaka 1998.
Akayesu, ambaye alikuwa meya wa jiji la Taba, alishtakiwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kwa kuhusika kwake katika mauaji ya halaiki ya Watutsi mwaka 1994, ambayo yalisababisha vifo vya watu 800,000.
Mnamo mwaka wa 2017, wakati huo huo, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Yugoslavia ya zamani (ICTY) ilimtia hatiani kamanda wa zamani wa Serb wa Bosnia Ratko Mladic kwa mauaji ya halaiki ya 1995 ya Srebrenica, ambapo wanajeshi wake waliwaua wanaume na wavulana 8,000 Waislamu. .
Lakini Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilikataa madai ya Bosnia kwamba Serbia, au Yugoslavia ya zamani, ilifanya mauaji ya kimbari moja kwa moja huko Srebrenica.
Badala yake, mahakama ilihitimisha kwamba Serbia haikuzuia mauaji hayo ya kimbari.
Michael Becker, ambaye alifanya kazi kama karani wa sheria katika ICJ, anasema mahakama inaweka kizuizi cha juu sana cha kuanzisha "nia ya mauaji ya kimbari" ya serikali.
Ni nini kinafanyika Gaza?
Mzozo huo ulizuka tarehe 7 Oktoba 2023 wakati wapiganaji wa Hamas walipozuka Gaza na kuua Waisraeli 1,200, pia wakiwachukua mateka zaidi ya 200 kurudi nao.
Tangu wakati huo, Israel imefanya mashambulizi ya anga, ilifanya uvamizi wa ardhini na kuwaamuru Wapalestina kuhamia kusini mwa Ukanda wa Gaza. Pia imezuia utoaji wa chakula na mafuta.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema zaidi ya watu 22,000 wameuawa kufikia sasa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Israel, Uingereza, Marekani na mataifa mengine yenye nguvu za Magharibi yanairothesha Hamas kama kundi la kigaidi.
Nini kitatokea tarehe 11 na 12 Januari 2024?
Afrika Kusini pia imewasilisha kesi ikiitaka ICJ kuchukua hatua ya dharura. Inataka mahakama iamuru Israel kusitisha harakati hatua zote za kijeshi mjini Gaza. Huu ni utaratibu wa haraka ambao husikilizwa kwanza.
"Hii haitasababisha kupatikana kwa mauaji ya kimbari katika hatua hii," anasema Bi McIntyre. "Kuna kiwango cha chini sana cha uthibitisho. Swali linaloulizwa ni kama kuna uwezekano wa madhara yasiyoweza kutenduliwa."
Afrika Kusini inahoji kwamba kuna "hatari inayowezekana ya kutokea kwa mauaji ya halaiki", anaongeza Bi McIntyre, ambapo wakati ni muhimu.
Ukraine ilitoa ombi sawa na hilo baada ya kuvamiwa na Urusi tarehe 24 Februari 2022, na ICJ ikaamuru Urusi kusitisha operesheni yake ya kijeshi wiki chache baadaye. Moscow ilipuuza amri hiyo.
Bi McIntyre anatarajia ICJ kutoa uamuzi wake mwishoni mwa Januari.
"Uamuzi kama huo ungeweka shinikizo kwa Israel," anasema Bi McIntyre, lakini anaongeza kuwa hautakuwa wa mwisho, na ICJ haina njia ya kuutekeleza.
"Mahakama inaweza baadaye huenda ikaamua hakukuwa na mauaji ya halaiki inapoangalia uhalali au kiini cha kesi."
Bw Becker anasema hukumu ya muda ya ICJ dhidi ya Urusi ilikuwa "ya kushangaza" kwa kufikia hatua ya kuiamuru Urusi kusitisha kampeni yake.
"Nina mashaka zaidi kwamba mahakama itaiambia Israel kuacha," anasema, akipendekeza mahakama inaweza kuiomba Israel "kuzuia" kampeni yake ya kijeshi.
"Inachoweza kumaanisha ni kwamba Israel lazima ifuate majukumu ya kisheria ya kimataifa ambayo tayari ina," anaongeza.
Vipi kuhusu kesi nyingine za mauaji ya halaiki katika ICJ?
Bi McIntyre anasema ulinganisho halali zaidi ni kesi ya mauaji ya kimbari ya Gambia dhidi ya Myanmar.
Wapalestina wa Gaza na watu wa Rohingya hawawezi kufikia ICJ kwa vile wao si mataifa, hivyo nchi nyingine zinafanya hivyo kwa niaba yao.
Gambia, kwa niaba ya nchi za Kiislamu, iliishutumu Myanmar kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Rohingya baada ya hadi milioni moja kulazimika kukimbilia Bangladesh mwaka 2017.
Mwishoni mwa mwaka wa 2023, Uingereza, Denmark, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi, pamoja na Canada, ziliomba kujiunga na kesi hiyo, ikimaanisha kuwa wanaweza kutoa hoja za kisheria.
"Ni ishara kwa ulimwengu na mahakama kwamba wanaunga mkono hatua inayochukuliwa," asema Bi McIntyre.
Nchi za Magharibi zilichukua hatua kama hiyo kuunga mkono Ukraine katika ICJ.
Lakini Bi McIntyre anahisi Magharibi itasuluhisha kesi hii.
"Hatutaona mataifa ya Magharibi yakiingilia kati kusaidia Afrika Kusini," anasema.
"Swali ni kama tutaona uingiliaji kati kutoka kwa mataifa ya Kiarabu."
Ni lini tunaweza kutarajia hukumu ya mwisho?
Gambia iliwasilisha kesi yake mnamo Novemba 2019 lakini kesi hiyo bado haijasikilizwa. Inaweza kuchukua miaka kadhaa hadi uamuzi wa mwisho utolewe.
Iwapo ICJ itabaini kuwa Israel ilifanya mauaji ya halaiki mjini Gaza, Bi McIntyre anasema baadaye inaweza kutumika kama ushahidi katika mashtaka ya jinai katika ICC.
Wataalamu hao wawili wa sheria wanakubaliana kwamba hukumu hiyo dhidi ya Israel itaweka shinikizo kwa nchi nyingine hususan wafuasi wa Israel kutathmini upya uhusiano wao na Tel Aviv.
Hata hivyo, Marekani tayari imejitokeza kupinga vikali kesi ya Afrika Kusini dhid ya Israel, huku msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House John Kirby akisema "haifai" na " haina msingi wowote wa ukweli".
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah