Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kauli ya Serikali ya Tanzania kuhusu tozo yapokelewa kwa hisia mseto
Yusuph Mazimu, BBC Swahili
Serikali ya Tanzania leo imelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu masuala ya tozo ya miamala ya simu na benki ambazo ni moja ya tozo zinazopigiwa kelele kwa muda sasa.
Ingawa tozo ya miamala ya simu ilianza kupigiwa kelele tangu ilipoanza kutumika mwaka jana, tozo kwenye miamala ya benki, imeibua upya hisia za malalamiko kuhusu mzigo wa tozo kwa wananchi.
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akiambatana na mawaziri wengine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI. Mh. Innocent Bashungwa alieleza kwamba serikali imesikiliza maoni ya wananchi na itayafanyia kazi.
‘Tumepokea maoni mbalimbali na tumekutana na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa wafanyakazi, wataalam binafsi, tumefuatilia tafiti mbalimbali, ikiwemo twaweza’, alisema Nchemba.
Hata hivyo kumekua na maoni tofauti kuhusu kauli hii ya serikali. Hancy Machemba kwenye mtandao wake wa Twitter ameonyesha kutokukubaliana na ufafanuzi wa Waziri Nchemba.
Getrude Mollel yeye aliunga mkono maelezo ya Serikali ya Tanzania, akitaka kodi ziongezwe na kutanuliwa zaidi.
Mwananchi mwingine anayejiita Madenge (Rollymsouth) yeye amempinga Getrude kwa kuonyesha kuwa muhimu kuongeza idadi ya walipa kodi na si kuongeza wigo wa tozo.
Msingi wa malalamiko ya tozo
Malalamiko makubwa ya wananchi ni kuhusu viwango na kutozwa tozo mara mbili, kwa mfano ukiipata fedha ya mshahara unakatwa tozo na kodi zingine, lakini ukihamisha kwenda Benki unakatwa, na ukiutuma kwa mtu mwingine kupitia simu unakatwa tena.
Hili hata kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, ambaye pia ni mweyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amelisema wiki hii.
Kuhusu hilo Nchemba alisema ‘Serikali imesikia hoja hii, na ni hoja ya msingi kweli kweli, tumepokea na tunafanyia kazi na tutatoa majibu kwenye utekelezaji wake, tutakwenda kwenye utekelezaji wake muda sio mwingi tutakuwa tumetoa utaratibu wa utekelezaji wake’.
Nini chimbuko la tozo hizi zinazolalamikiwa?
Kuna tozo kadhaa zinatajwatajwa kwenye mitandao nchini Tanzania. Mfano tozo kwenye mita za umeme-Lipa Umeme Kadiri Unavyotumia (LUKU), tozo kwenye mafuta ya diseli, taa na petroli na pia kadi za simu.
Mijadala zaidi ni tozo kwenye visimbuzi na tozo kwenye miamala ya benki. Lakini chimbuko lake limetokea wapi hasa?
'Chimbuko la tozo ilikuwa ni kuunganisha nguvu kama watanzania ili tuweze kutekeleza baadhi ya mahitaji ya lazima, ambayo pengine yalikuwa yakikosa bajeti kutokana na bajeti inavyopangwa,' anasema Mwigulu Nchemba na kuongeza....
'tulianza kama mapendekezo, serikali ikapendekeza, wawakilishi wa wananchi wakaona kweli hili jambo lina mantiki, tulifanya kwa kuzingatia ulazima wa maeneo (mahitaji) hayo, 'Kwa mfano madarasa, nyumba za walimu, ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa miundo mbinu'.
Pamoja na miradi mikubwa kama bwawa la mwalimu Nyerere lenye bajeti ya zaidi ya trilioni 6 na reli ya kisasa bajeti dola bilioni 10 kama trilioni 23 anasema tozo hii ya kibenki simu ni kodi ya mshikamano
'hii si kodi ya biashara wala hii sio kodi ya faida ya biashara, hii ni 'solidarity fund' kwamba tuna watoto wetu kama tusivyochangishana ndoto yao itaishia hapa, alisema.
Kauli ya Serikali na matarajio ya wananchi
Kwa mujibu wa Utafiti wa shirika la Twaweza uliotolewa Agosti 25, 2022 kuhusu tozo unaonesha wengi kwamba watanzania wanaamini kuhusu umuhimu wa tozo, lakini hawazikubali.
Pengine kwa mawaziri wa serikali kujitokeza leo wakiongozwa na waziri wa fedha, Nchemba, wananchi pengine walitarajia kusikia kwamba tozo zimeofutwa ama kuondolewa. Hata wapo wanaojaribu kuendesha maoni yao mtandaoni kuuliza watu kwamba tozo zifutwe ama la.
Wangine wakiulizana kama maelezo na ufafanuzi wa Waziri umeeleweka ama umeongeza mkanganyiko zaidi.
Serikali inasema Kodi ya miamala ya simu na beki kwa mujibu wa Serikali si kodi mpya.
'kilichokuwa kinafanyika, mtu akifanya muamala kwa kutumia laptop, kiwango kile kile ambacho mwenzake wa simu amefanya, yeye alikuwa hakatwi, kwa sababu tu amefanya kwa laptop', tukaona busara na wananchi walishauri tupunguze kiwango ila tuongeze wigo, anasema Nchemba.
Hata kama si kodi mpya, kwa sababu kuna malalamiko, Nchemba anasema Serikali inakwenda kufanyia kazi malalamiko naitaleta majibu ya utaratibu na masuala mengine ya tozo, ingawa hajasema ni lini hasa majibu ya malalamiko ya wananchi yatatolewa.
"Tunatambua kuwa tozo, ni maumivu ya hapa na pale, tunatambua kuwa inavuruga 'purchasing power' (uwezo wa kununua bidhaa na huduma) ya mtu mmoja mmoja lakini tuna majukumu ambayo kama nchi na sisi wote kama wazazi tunawajibika kuyabeba kama jukumu letu," Waziri wa Fedha , Dk Mwigulu Nchemba