Tiba ya homoni kwa wanawake waliokoma hedhi ni nini? hatari na faida zake

Kuanzia hali ya joto na ukungu wa akili hadi maumivu ya viungo na kukosa usingizi. Kuna dalili nyingi zinazoambatana na ukoma wa hedhi na kipindi cha mpito hadi hatua hii ya maisha ya uzazi ya mwanamke.

Lakini kwa wanawake ambao wanakabiliwa na baadhi ya dalili hizi na wanaona kuwa inasababisha kuzorota kwa ubora wa maisha yao, kuna chaguo la tiba ya uingizwaji wa homoni (pia inaitwa tiba ya homoni au tiba ya uingizwaji wa homoni).

Ikiwa unazingatia mbadala huu, hapa kuna mwongozo wa baadhi ya maswali ya msingi ili kukusaidia kuelewa ni mambo gani ya kuzingatia.

Tiba ya uingizwaji wa homoni ni nini?

Wakati hedhi inapokaribia kukoma, viwango vya estrojeni hubadilika-badilika na kupungua kwa baadhi ya wanawake.

Estrojeni zina kazi nyingi: husaidia kudhibiti mzunguko wa hedhi, huchangia kutengeneza mifupa yenye nguvu na huathiri joto la ngozi.

Viwango vya estrojeni vinapoyumba, dalili mbalimbali kama vile mwili kupata joto kali, kutokwa na jasho usiku, wasiwasi, na maumivu ya viungo vinaweza kutokea.

Tiba ya homoni huongeza viwango vya estrojeni katika mwili wa mwanamke na inaweza kusaidia kupunguza dalili hizi.

Wanawake wanaofanya tiba hii kwa kawaida haiwachukui milele, ili tu kupunguza dalili hizo katika kipindi cha mpito wa kukoma hedhi na wengi wanasema imefanya tofauti kubwa kwa ustawi wao.

Tiba ya uingizwaji wa homoni pia inaweza kuwa na faida zingine, kama vile kuzuia udhaifu wa mfupa na kuvunjika. Kwa wanawake walio chini ya miaka 60, inaweza pia kutoa ulinzi fulani dhidi ya ugonjwa wa moyo.

Huenda umesikia kuhusu manufaa mengine yanayoweza kutokea, kama vile kulinda afya ya ubongo na kuboresha ngozi na nywele, lakini hadi sasa ushahidi wa faida hizo ni mdogo.

Je, inasimamiwa vipi?

Matibabu huja katika maumbo na ukubwa tofautitofauti, kuanzia vidonge na hadi jeli na pete.

Kiambatanisho kikuu ni estrojeni, lakini moja ya aina za kawaida ni tiba ya mchanganyiko, ambayo estrojeni hutolewa pamoja na toleo la synthetic la progesterone ya homoni.

Kuongeza progesterone husaidia kulinda ukuta wa tumbo la uzazi, kwani estrojeni pekee inaweza wakati mwingine kuongeza hatari ya saratani ya mfuko wa uzazi.

Aina bora ya tiba hutofautiana kati ya mtu na mtu na inategemea dalili na mtindo wa maisha. Kwa ujumla, anza na kipimo cha chini kabisa.

Ni tiba gani iliyo bora kwangu?

Tiba nyingi za homoni huathiri mwili mzima. Lakini baadhi kama Gina 10, inapatikana kwenye maduka ya dawa nchini Uingereza hutumiwa katika uke tu, ili kupunguza dalili katika sehemu hiyo ya mwili.

Hii inapunguza kiwango cha estrojeni kufyonzwa na sehemu nyingine za mwili, lakini inamaanisha kuwa matibabu haya hayaondoi dalili zingine kama vile mwili kuwaka moto.

Inachukua muda gani kwa matibabu kuanza kufanya kazi?

Inaweza kuchukua hadi miezi mitatu kabla yakuhisi athari kamili na kipimo na aina ya tiba ya homoni inaweza kuhitaji kurekebishwa au kubadilishwa.

Wataalamu wengi wanapendekeza kuanza tiba ya uingizwaji wa homoni kwa dalili ya kwanza za kukoma hedhi.

Ushahidi ni mdogo linapokuja suala la kuanza baada ya miaka 60, ingawa baadhi ya wanawake hupata nafuu kutokana na dalili zinazoendelea.

Hakuna kikomo kwa muda wa kuitumia. Baadhi wanaunga mkono wazo la kuendelea na matibabu kwa miaka mingi, lakini Wakala wa Udhibiti wa Dawa na Bidhaa za Afya wa Uingereza unapendekeza itumike kwa kipimo cha chini kabisa na kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Kuna hatari gani?

Ingawa tiba hii imekuwa na habari vibaya hapo awali, faida zake zinadhaniwa kuzidi hatari zake.

Tafiti mbili zilizochapishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 zilisema kuwa na madhara zaidi kuliko faida. Hii ilipata matangazo mkubwa na matumizi yake yalipunguzwa.

Wengine huendelea kuwa waangalifu, licha ya uthibitisho unaoongezeka kwamba matibabu yanaweza kusaidia.

Aina fulani za matibabu yamehusishwa na hatari iliyoongezeka kidogo ya saratani. Mchanganyiko, kwa mfano, unaweza kuhusishwa na hatari ndogo ya kuongezeka kwa saratani ya matiti.

Kuna hatari ndogo ya kuganda kwa damu wakati wa kutumia dawa hii. Walakini, pia inategemea mambo mengine, kama vile sigara, uzito na umri.

Hatari ni ndogo ikiwa unatumia vipande vya kwenye ngozi au jeli badala ya vidonge.

Hatari ya kuganda kwa damu ni ndogo sana kuliko ile ya kuchukua vidonge vya kudhibiti uzazi au kupata mimba.

Madhara ni yapi?

Madhara mengi yanaonekana ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza matibabu. - Matiti kuuma - maumivu ya kichwa - kichefuchefu - Ugumu wa kusaga chakula - maumivu ya tumbo - kutokwa na damu ukeni

Ni kawaida kuongezeka uzito unapokaribia kukoma hedhi, lakini hakuna ushahidi kwamba tiba ya homoni ndiyo sababu.

Nani hapaswi kutumia matibabu haya?

Inaweza kuwa haifai katika kesi hizi: - Ikiwa umekuwa na saratani ya matiti, saratani ya mfuko wa uzazi - Shinikizo la damu lisilotibiwa - Ugonjwa wa ini - Au wewe ni mjamzito

Nini kingine cha kufanya?

Mazoezi ya mara kwa mara yanaweza kukusaidia kulala vizuri, kupunguza mwili kuwaka moto na kuboresha hisia zako.

Kula lishe bora, kupunguza unywaji wa kahawa, pombe, vyakula vyenye viungo, na kuacha kuvuta sigara kunaweza pia kusaidia kupunguza joto.

Mazoezi ya viungo, kupanda mlima, kutembea haraka haraka au kucheza tenisi pia huchangia kuimarisha mifupa.

Dawa zingine kama Tibolone, ambayo hufanya kazi kwa kuiga shughuli ya estrojeni na progesterone, au dawamfadhaiko fulani zinaweza kusaidia. Lakini pia zinaweza kuwa na madhara.

Huenda umesikia kuhusu homoni zinazofanana kibiolojia. Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza, kwa mfano, haipendekezi kwa sababu hazijadhibitiwa na usalama wake hauko wazi.