Safari ndefu ya kupata haki Afrika Kusini juu ya madhila ya ubaguzi wa rangi

Chanzo cha picha, Kwa hisani ya Fort Calata Found
Kumbukumbu ya awali ya Lukhanyo Calata ni mazishi ya baba yake. Anakumbuka baridi kali iliyokuwepo na majonzi ya mama yake. Ilikuwa msimu wa baridi mwaka 1985 katika kijiji kidogo cha Carckdock mashariki mwa Cape.
Anakumbuka akihisi kama ardhi inapasuka kutokana na kishindo cha kuimba na kucheza kwa maelfu ya waombolezaji.
Walifika kutoka kila kona ya nchi kutoa heshima zao za mwisho kwa baba yake Lukhanyo,Fort Calata na wanaume wengine watatu ambao walijulikana kama 'Cradock Four'. Licha ya kuwa mojawapo ya uhalifu mbaya zaidi kukumbukwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi,wanaoshukiwa kuhusika nao hawajawahi kufikishwa mahakamani licha ya kuwa hawakupewa msamaha na tume ya taifa ya ukweli na maridhiano (TRC).
Lakini sasa,shinikizo linashika kasi la kufungua upya uchunguzi kuhusu uhalifu huu na mamia ya uhalifu mwingine uliotendwa wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi. Mauaji ya 'Cradock Four' mnamo mwaka 1985 yalizua ghadhabu kote Afrika Kusini.
Oliver Tambo, Rais wa chama cha African National Congress ANC ambacho wakati huo kilikuwa kimepigwa marufuku alihutubia umati uliokuwa umehudhueia mazishi hayo kupitia ujumbe alioutuma akiwa uhamishoni.
Siku hiyo, Rais PW Botha alitangaza hali ya hatari mashariki mwa Cape na kurefusha amri hiyo mwaka uliofuatia. Hatua hiyo iliipa Polisi na vikosi vingine vya usalama ngumu kubwa za kukandamiza shughuli za kisiasa za kutaka kukomeshwa kwa utawala wa wazungu walio wachache Afrika Kusini.
United Democratic Front (UDF) ambacho kilikuwa kikiandaa harakati za vijijini za muungano wa mamia ya asasi zilizokuwa zikipinga ubaguzi wa rangi, mmoja wa wanaharakati hao wanne,Matthew Goniwe mara kadhaa angesafiri hadi mji wa Port Elizabeth kuhudhuria mikutano. Katika mojawapo ya mikutano hiyo,aliandamana na Fort Calata, Sparrow Mkhonto na Sicelo Mhlauli.

Chanzo cha picha, The Washington Post
Viongozi hao wanne waliokuwa na ushawishi katika jamii walijulikana na polisi kwa kuendeleza harakati zao za kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi. Walipokuwa wakirejea Cradock,safari ya umbali wa kilomita 200 usiku huo,walisimamishwa katika kizuizi cha polisi barabarani.
Miili yao iliyokuwa imeungua baadae ilipatikana katika maeneo tofauti. Mwanzoni,serikali ilikanusha kuhusika na mauaji yao na jopo la uchunguzi mwaka 1987 lilisema wanaume hao wanne waliuawa na watu wasiojulikana.
Lakini uchunguzi wa pili ulianzishwa kuelekea mwishoni mwa utawala wa wazungu mwaka 1993 baada ya gazeti moja kuripoti kuwa ujumbe wa siri wa kijeshi ulikuwa umetumwa ukitaka kile kilichosemakana 'kuondolewa kabisa kutoka kwa jamii' kwa bwana Goniwe binamu yake Mbulelo Goniwe na Bwana Calata. Ilifikia uamuzi kuwa maafisa wa usalama walihusika katika mauaji yao lakini haikujtaja majina ya hasa ni kani waliohusika.
Bado haki haijapatikana
Lukhanyo Calata alikuwa na umri wa miaka mitatu wakati baba yake alipouawa. Miaka thelathini na nane baadae,familia za Cradock Four bado zinasubiri waliohusika na mauaji hayo kuwajibishwa. Kisa hicho ni miongoni mwa maelfu ya vitendo vya uhalifu vilivyosikizwa na TRC kujaribu kutuliza hali Afrika Kusini kufuatia kufikia kikomo kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Rais Nelson Mandela alimuomba Askofu Mkuu Desmond Tutu kuongoza tume hiyo iliyolenga kuliponesha taifa hilo kupitia maridhiano na msamaha ili kuepusha kuzuka kwa ghasia za kulipiza visasi baada ya miongo ya ukatili dhidi ya watu weusi nchini humo.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ilileta pamoja washukiwa,mashahidi na waathiri wa vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanywa wakati wa utawala wa wazungu kutoa ushahidi mbele ya umma. TRC ilitoa msamaha kwa wale waliokiri kwa dhati makosa yao,ambapo angalau ingewapa jamaa za wahanga faraja ya kujua kilichowasibu wapendwa wao.
Maafisa Sita wa polisi kati ya saba waliokiri kuhusika na mauaji ya Cradock Four walinyimwa msamaha kwa misingi kuwa hawakufichua kila kitu. Kesi hiyo ni miongoni mwa nyingine takriban mia tatu ambazo TRC ziliwasilisha kwa waendesha mashitaka mnamo 2023 kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kufungua mashitaka.
Lakini kwa jamaa ambao wamesubiri kwa miongo kadhaa kwa haki kupatikana,kilichofuata ni kusubiri zaidi kwani karibu kila ya hizo kesi bado hazijashughulikiwa. Haijabainika wazi ni kwanini maafisa wanajikokota katika kushughulikia kesi hizo.
Kilichotoa mwanga ya kwanini huenda kuna kucheleweshwa huko kulikuja mwaka 2015 wakati dada ya Nokuthula Simelane,mwanaharakati mchanga aliyepotea 1983, alipowasilisha kesi mahakamani ya kutaka uchunguzi rasmi kuhusu kupotea kwako.
Maafisa wa zamani wa ofisi ya waendesha mashitaka walijitokeza na kudai kuwa serikali ilizuia uchunguzi na kufunguliwa mashitaka kwa kesi zilizowasilishwa na TRC ikiwemo ile ya Bi Simelane.
Walidai kuwa kulikuwa na wasiwasi kuwa ucgunguzi wa baadhi ya kesi huenda ungewahusisha baadhi ya viongozi wa chama tawala cha ANC na ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. BBC ilitafuta maonii ya Serikali ya Afrika Kusini kuhusiana na madai hayo lakini haikupata jibu.
Hakujakuwa na uchunguzi rasmi kuhusu madai ya muingilio wa kisiasa na sababu hasa ya kuhusishwa na madai hayo. Hata hivyo,taarifa hizo zinaonekana kama kuwasafishia nia mawakili wa waathiriwa ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakifuatilia hitimisho za kesi hizo bila ya mafanikio.Bwana Calata anasema hatimaye ni bayana kile ambacho wamekijua kimedhihirika.

Chanzo cha picha, Familia ya Nokuthula Simelane
Bi Simelane alikuwa mwanachama wa uMkhonto we Sizwe,tawi la kijeshi la ANC,alipotekwa katika eneo la maegesho ya gari mjini Johannesburg Septemba ya 1983 na kuteswa kwa majuma kadhaa. Hayo ni kulingana na ushahidi uliotolewa na maafisa wa polisi waliohudumu wakati wa utawala wa wazungu.Mwili wake haukuwahi kupatikana.
Maafisa wawili kati ya wanne wa polisi waliotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Simelane wameshafariki dunia. Kesi zinasowakabili wawili waliosalia inaahirishwa mara kwa mara.Maafisa watatu kati ya hao wanne waliokuwa wameomba kupewa msamaha na tume ya TRC,kwa kumtesa bi Simelane ombi lao halikuridhiwa na hakuna kati yao aliyeomba msamaha kwa mauaji yake.
'Pigo kubwa'
Kufunguliwa upya kwa uchunguzi mwaka 2017 wa kifo cha mwanaharakati Ahmed Timol aliyefia mikononi mwa polisi 1971. Afisa wa polisi alishitakiwa kwa mauaji ya Timol mwaka uliofuatia lakini alifariki dunia kabla ya kufikishwa kizimbani.
Ilikuwa mwanzo mpya anasema Katarzyna Zdunczyk, meneja wa mipango wa TRC katika shirika lisilo la serikali,wakfu wa Haki za binadamu.
Mapema mwaka huu,familia za waathiriwa zilipokea vyema taarifa kuwa mamlaka ya kitaifa ya kuendesha mashitaka NPA imemteua aliyekuwa kamishna wa TRC Dumisa Ntsebeza kutathmini utendakazi wake katika kushughulikia kesi hizo.
Lakini bi Zdunczyk anaamini kuwa uchunguzi huo hautaweza kuchunguza kikamilifu muingilio wa kisiasa na kusema kinachohitajika ni tume huru kuundwa kuchunguza madai hayo. Wengi wa waliohusika na ukiukaji wa haki za binadamu na mashahidi wakuu wameshafiriki dunia,uwezekano wa kusuluhisha kesi hizo unaonekana kuwa mdogo.
Lakini Bwana Calata anasema ataendelea kufuatilia kesi ya baba yake. Bi Nkadimeng anasema familia yake inachotaka ni hatimaye kuweza kufunga ukurasa huu mchungu. Baba yake na ndugu yake walifariki dunia bila ya kushuhudia Simelane akipatikana na kuzikwa lakini anatumai mama yake ataweza kufanya hivyo.














