Watafiti wagundua ishara ya maisha kwenye sayari ya mbali

edw

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Mchoro wa sayari ya K2-18

Darubini ya NASA ya James Webb inaweza kuwa imegundua ishara ya uhai kwenye sayari ya mbali. Imegundua atomi inayoitwa dimethyl sulfidi (DMS). Kwenye dunia, atomi hii huzalishwa na viumbe hai tu.

Watafiti wanasisitiza kwamba ugunduzi huu wa sayari ya umbali wa miaka 120 kwa spidi ya mwanga sio thabiti na takwimu zaidi zinahitajika ili kudhibitisha hilo.

Watafiti pia wamegundua methane na CO2 katika angahewa ya sayari hiyo. Kugunduliwa kwa gesi hizi kunaweza kumaanisha sayari, inayoitwa K2-18b, ina bahari ya maji.

Prof Nikku Madhusudhan, wa Chuo Kikuu cha Cambridge, ambaye aliongoza utafiti huo, aliambia BBC News kwamba timu yake ilishtuka ilipoona matokeo haya.

"Duniani, DMS inazalishwa tu na viumbe hai. Katika angahewa ya dunia gesi hii hutolewa na viumbe vya baharini," alisema.

Tahadhari

fg

Chanzo cha picha, ESA

Maelezo ya picha, Mchoro wa darubini ya James Webb Space

Ni mara ya kwanza wana anga kugundua gesi ya DMS katika sayari ya mbali. Lakini wanashughulikia matokeo kwa tahadhari. Wakikumbuka madai yaliyotolewa 2020 juu ya uwepo wa gesi ya phosphine, ambayo inaweza kuzalishwa na viumbe hai kwenye mawingu ya Venus. Lakini ilibainishwa mwaka mmoja baadaye kuwa si kweli.

Hata hivyo, Dkt. Robert Massey, mtafiti huru na naibu mkurugenzi wa Royal Astronomical Society huko London, anasema matokeo haya ya sasa yanafurahisha.

''Tunasonga polepole kuelekea mahali ambapo tutaweza kujibu swali la kama tuko peke yetu katika ulimwengu au la," anasema.

''Nina matumaini kwamba siku moja tutapata dalili za maisha. Pengine hivi punde, pengine katika miaka 10 au hata 50 tutakuwa na ushahidi wenye maelezo bora zaidi.''

Sayari iko umbali wa zaidi ya kilomita milioni 1.1, kwa hivyo kiwango cha mwanga kinachofikia darubini ni kidogo. Pamoja na DMS, pia wamegundua gesi ya methane na kaboni kwa kiwango kikubwa.

Darubini ya Nasa ya Hubble iligundua uwepo wa mvuke wa maji, ndiyo maana sayari hiyo, ambayo imepewa jina la K2-18b, ilikuwa mojawapo ya sayari ya kwanza kuchunguzwa na JWST. Lakini uwezekano wa uwepo wa bahari ni mkubwa.

Uwezo wa sayari kuhimili uhai unategemea halijoto, uwepo wa kaboni na pengine maji maji. Uchunguzi kutoka kwa JWST unapendekeza kwamba K2-18b ina hayo yote.

Uwepo wa sayari yenye dalili za uhai - haimaanishi kwamba kuna uhai. Kinachofanya sayari hii kuwa ya kuvutia zaidi ni kwamba haifanani na sayari ya dunia na ni karibu mara tisa ya ukubwa wa dunia.