Kwanini Israel imeanzisha operesheni kubwa katika Ukingo wa Magharibi?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Ukingo wa Magharibi ulikumbwa na moja ya siku zenye vurugu zaidi katika kipindi cha hivi karibuni kutokana na operesheni ya vikosi vya Israel, na kusababisha vifo vya Wapalestina 10, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.

Vikosi vya usalama vya Israel vimesema vimeanza "operesheni ya kupambana na ugaidi" usiku kucha huko Jenin na Tulkarm, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na hadi sasa wamewaua "magaidi watano waliokuwa na silaha kutoka angani na ardhini."

Pia waliripoti kuwa wengine wanne waliuawa katika shambulio la anga wakati wa operesheni katika kambi ya wakimbizi ya al-Faraa karibu na Tubas.

Waandishi wa habari wa eneo hilo wanasema hawajaona operesheni kubwa kiasi hiki katika Ukingo wa Magharibi tangu siku za Intifada ya pili ya Wapalestina, uasi mkubwa dhidi ya uvamizi wa Israel ambao ulifanyika kati ya 2000 na 2005.

Kumekuwa na ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi tangu shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7 na vita vilivyofuata huko Gaza.

Ukingo wa Magharibi uko wapi huko?

Ukingo wa Magharibi upo magharibi mwa Mto Jordan na mashariki mwa Jerusalem. Kulingana na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina, takribani watu milioni 3.2 wanaishi katika eneo hilo. Wengi wao ni Wapalestina, ingawa pia kuna Wayahudi wanaoishi katika makazi yanayochukuliwa kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa.

Waanzilishi wa Israel ya sasa walikubaliana mwaka 1947 kwamba sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi inapaswa kuwa sehemu ya taifa la baadaye la Palestina. Hata hivyo, Israel iliacha mpango huu baada ya kushambuliwa na nchi jirani za Kiarabu.

Jordan ilichukua eneo hilo baada ya kusitishwa kwa mapigano mwaka 1950, lakini wanajeshi wa Israel walilitwaa katika Vita vya Siku Sita vya 1967 na likawa chini ya uvamizi wa kijeshi.

Katika miaka ya 1970 na 1980, Israel ilianzisha makazi ya Walowezi, na kuzua upinzani kutoka kwa wakaazi Waarabu na maandamano kutoka jumuiya ya kimataifa. Wapalestina walipanga uasi katika Ukingo wa Magharibi kutoka 1987 hadi 1993, na kutoka 2000 hadi 2005.

Jordan iliachana na madai yake kwa Ukingo wa Magharibi mwaka 1988. Kufuatia Makubaliano ya Oslo ya mwaka 1993. Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina inasimamia sehemu ya eneo hilo, na iliyobaki iko chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Israel.

Waisraeli na Wapalestina wanadai haki ya eneo hilo, lakini baada ya miongo kadhaa na majaribio yaliyoshindwa ya mazungumzo, mzozo bado haujatatuliwa.

Kwanini Israel hufanya operesheni?

Vikosi vya Israel huvamia mara kwa mara miji minne ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi: Jenin, Tulkarem, Nablus na Tubas, pamoja na kambi za wakimbizi zilizo karibu.

Katika operesheni hii, vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, barabara kuu za kuelekea Jenin zilifungwa na mapigano ya silaha yameripotiwa katika kambi ya wakimbizi ya mji huo. Msemaji wa jeshi la Israel alisema "vikosi vingi vimeingia katika mji huo.”

Duru za Wapalestina zinaonyesha wanajeshi wa Israel waliingia katika hospitali moja mjini Jenin alfajiri na kuziba njia ya kuingia katika hospitali nyingine mbili za Tulkarem.

Huko Nablus, jeshi lilishambulia kambi mbili za wakimbizi. Katika kambi ya Far'a, karibu na Tubas, watu walijeruhiwa kutokana na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Israel, na wanajeshi wa Israel waliripotiwa kuingia katika kituo cha matibabu cha Hilali Nyekundu.

Maafisa wa Israel waliripoti kwamba "magaidi tisa waliokuwa na silaha wameuawa.”

Katika kambi ya Nur Shams huko Tulkarem, wanajeshi wa Israel walizingira kambi hiyo na mkazi mmoja alisema kulikuwa na "makabiliano ya risasi."

Mkazi mwingine alisema wanajeshi walifunga barabara nje ya kambi ili kukagua vitambulisho vya kila mtu anayeondoka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz alisema Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) "limekuwa likifanya kazi kwa nguvu zote tangu jana usiku katika kambi za wakimbizi za Jenin na Tulkarem ili kusambaratisha miundo msingi ya kigaidi ya Iran."

Msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Nadav Shoshani amesema, wanajeshi huko Jenin na Tulkarm wamefanya "operesheni za kiintelijensia za kukabiliana na ugaidi ili kuzuia mashambulizi dhidi ya raia.”

Tangu shambulio la Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, Israel imekuwa ikifanya operesheni katika Ukingo wa Magharibi karibu kila siku.

Majibu ya Wapalestina

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi, imehimiza jumuiya ya kimataifa kusaidia kulinda hospitali za Jenin, Tulkarem na Tubas.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano asubuhi, wizara hiyo ilitoa wito wa usaidizi kutoka "jumuiya ya kimataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu" na kulishutumu jeshi la Israel kwa kuzuia magari ya wagonjwa, jambo ambalo "ni ukiukaji wa wazi wa sheria za ubinadamu.”

Mamlaka ya Palestina imeripoti, jeshi la Israel lilifunga barabara zinazoelekea katika hospitali ya Ibn Sina na kuizingira hospitali ya Khalil Suleiman na makao makuu ya shirika la Hilali Nyekundu na Friends of Patients Society.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, alikatiza safari yake kuelekea Saudi Arabia kufuatia hali ya Ukingo wa Magharibi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina.

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani kuongezeka kwa operesheni za kijeshi katika Ukingo wa Magharibi. Ofisi hiyo inasema operesheni hii inafanywa "katika namna ambayo inakiuka sheria za kimataifa na kuzidisha hali mbaya. Matumizi ya nguvu katika Ukingo wa Magharibi lazima yazingatie sheria za kibinadamu.”

Umoja wa Mataifa uliripoti wiki iliyopita, Wapalestina 128, wakiwemo watoto 26, waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukingo wa Magharibi tangu Oktoba 7.

Kwa jumla, Wapalestina 607 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, katika kipindi hicho. 11 kati yao walikufa kutokana na vurugu za walowezi wa Israel.

Katika Ukingo wa Magharibi kuna kambi kadhaa za wakimbizi zinazohifadhi maelfu ya Wapalestina ambao familia zao zilihamishwa kutoka katika makazi yao katika eneo ambalo sasa ni Israel.

“Kambi hizo zina viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa ajira, haswa miongoni mwa vijana. Huko Jenin, kumekuwa na makundi mengi mapya ya wanamgambo wa Kipalestina,” anaeleza mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia Paul Adams, “na operesheni zinazoendelea za Israel ni jaribio la kuyavunja.”

“Israel inaamini Iran imekuwa ikisaidia kuunda vikundi vipya vyenye silaha katika Ukingo wa Magharibi, kwa ufadhili na silaha, ili kuiweka kati Israel kwenye pande zote,” anasema Adams.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla