Jinsi Urusi inavyojaribu kuongeza ushawishi wake Afrika

sdxz

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Chiagozie Nwonwu, Fauziyya Tukur, Olaronke Alo & Maria Korenyuk
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wachezaji wa mpira wakisikiliza wimbo wa taifa wa Urusi kabla ya mechi. Karibu yao, wasanii wanachora picha ya Rais wa Urusi Vladimir Putin ukutani wakati wa tamasha la uchoraji.

Karibu Burkina Faso, mojawapo ya mataifa ya Afrika ambako Urusi inaongeza shughuli zake ili kupata ushawishi.

Ushahidi uliopatikana na BBC unaonyesha Urusi inavyotumia vyombo vya habari na tamaduni kuvutia waandishi wa habari wa Kiafrika, watu maarufu mitandaoni, na wanafunzi huku pia ikitumia habari za kupotosha kuongeza ushawishi wake Afrika.

Matukio haya yanasimamiwa na African Initiative, shirika jipya la vyombo vya habari la Urusi ambalo linajitambulisha kama "daraja la habari kati ya Urusi na Afrika." Lilianzishwa kutoka katika kikundi la mamluki cha Wagner na inaaminika lina uhusiano na mashirika ya usalama ya Urusi.

Lilisajili mwezi Septemba 2023, mwezi mmoja baada ya kiongozi wa Wagner, Yevgeny Prigozhin kufariki katika ajali ya ndege, African Initiative imewaleta wafanyakazi wa zamani kutoka Wagner iliyovunjwa.

Shughuli zake ziko hasa katika nchi tatu zinazosimamiwa na jeshi za Mali, Niger na Burkina Faso. Kufuatia mapinduzi, mataifa haya ya Afrika Magharibi yamejitenga na washirika wa Magharibi kama vile Ufaransa, yakikosoa kushindwa kupambana na vikundi vya jihadi na urithi wa kikoloni. Badala yake wameegemea Urusi.

Kando na shughuli za kitamaduni, African Initiative huendesha tovuti ya habari yenye habari kwa Kirusi, Kiingereza, Kifaransa, na Kiarabu, pamoja na chaneli ya video na chaneli tano za Telegram, mojawapo ikiwa na karibu watu 60,000.

Baadhi ya chaneli za Telegraph zinatokana na zile za zamani ambazo zilikuwa zimeundwa na vikundi vyenye uhusiano na Wagner. Walikuwa wa kwanza kuunga mkono chaneli ya kijeshi ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi ya Africa Corps, ambayo imechukua nafasi ya tawi la kijeshi la Wagner huko Afrika Magharibi.

Habari za kuunga mkono Urusi na habari za kupotosha, haswa kuhusu Marekani, zimeenea huko.

Habari kwenye tovuti ya African Initiative zinasema bila ushahidi kuwa Marekani inaitumia Afrika kama eneo la uzalishaji na majaribio ya silaha za kibiolojia.

Taarifa moja inaangazia madai ambayo hayajathibitishwa ya Kremlin kuhusu maabara za kibayolojia za Marekani kuhamishwa kutoka Ukraine hadi Afrika. Na wanasema maabara za kibayolojia za Marekani katika bara hilo zinaongezeka.

Taarifa hizo zinadai ni "chini ya kivuli cha utafiti na miradi ya kibinadamu, bara la Afrika linakuwa uwanja wa majaribio kwa Pentagon," na kupendekeza kuwa kuna majaribio ya kibiolojia ya siri yanaendelea.

Propaganda kupitia wanahabari

x

Chanzo cha picha, Russdiary

Maelezo ya picha, Mwandishi wa habari wa Ghana, Ivy Setordjie, alichapisha mfululizo wa ripoti ambapo anaitaja miji inayokaliwa na Urusi nchini Ukraine kama "maeneo ya migogoro nchini Urusi"
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Propaganda za Prigozhin zililenga hasa Ufaransa, lakini African Initiatives "unawalenga Wamarekani kwa kiwango kikubwa," anasema mtafiti Jedrzej Czerep, mkuu wa Kitengo cha Mashariki ya Kati na Afrika katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Poland.

Mwezi Juni, wanablogu na waandishi wa habari kutoka nchi nane walialikwa kwa "ziara ya waandishi wa habari" ya siku saba katika maeneo yanayokaliwa na Urusi ya Ukraine. Safari hiyo iliandaliwa na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi na maafisa wa Urusi walioekewa vikwazo na nchi za Magharibi, na waandishi hao walitembelea makao makuu ya African Initiative mjini Moscow.

"Afrika haikuwa ikipata habari nyingi [kuhusu vita]," Raymond Agbadi, mwanablogu na mwanasayansi kutoka Ghana ambaye alisoma nchini Urusi na aliyeshiriki katika "ziara ya waandishi wa Habari," aliiambia BBC. "Habari zozote tulizokuwa tukipata hazikuwa na ushawishi wa kutosha kwetu kuelewa vita hasa vinahusu nini."

Mtu mwenye ushawishi katika mitandao, Mmarekani Jackson Hinkle, mfuasi mkubwa wa Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye ameeneza madai mengi ya uongo kuhusu Ukraine, pia alikuwa kwenye ziara hiyo.

Baada ya kutembelea Moscow, waandishi wa habari walisafiri kilomita 1,250 (maili 780) hadi mji wa bandari wa Ukraine wa Mariupol katika mkoa wa Donetsk. Kisha wakaenda katika miji ya eneo la Zaporizhzhia - maeneo yote hayo yalitekwa na Urusi mapema katika uvamizi wake wa Ukraine.

Wakati wote wa ziara hiyo, waandishi hao waliandamana na maafisa wa Urusi na walisafiri pamoja na jeshi la Urusi kwa magari yaliyo na alama ya Z - ishara ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Mwezi Mei, African Initiative iliandaa "ziara ya wanahabari" wengine kuzuru Mariupol inayokaliwa na Urusi kwa ajili ya wanablogu kutoka Mali. Safari za wanahabari ni mbinu inayotumika sana kujaribu kubadili maoni kuhusu Urusi.

Katika habari zilizochapishwa tangu safari hiyo, waandishi wa habari wa Kiafrika wanaitaja miji ya Ukraine inayokaliwa na vikosi vya Urusi kama "maeneo ya migogoro nchini Urusi" na wananukuu propaganda za serikali ya Urusi na kuwasilisha mtazamo wa Kremlin kuhusu mipaka ya Ukraine.

Katika kipande kilichochapishwa kwenye JoyOnline, tovuti inayotumia Kiingereza inayoendeshwa na Multimedia Group, mwandishi wa habari wa Ghana Ivy Setordjie anaandika kuhusu eneo la Ukraine la Zaporizhzhia [ambalo mji mkuu wake uko chini ya udhibiti wa Ukraine], kuwa "liko kusini mwa Urusi."

Anaiambia BBC kuwa hakubaliani kwamba maeneo hayo yalitwaliwa kinyume cha sheria na Urusi, akithibitisha kwamba ripoti zake ni uamuzi wake mwenyewe na hazihusiani na nchi.

Ushawishi wa Urusi katika jamii

zx

Chanzo cha picha, mariupol-news.ru

Maelezo ya picha, Waandishi wa habari wa Afrika walichukuliwa katika ziara ya siku saba katika mikoa inayokaliwa ya Ukraine

Mbali na ziara za waandishi wa habari, African Initiative katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi, imeshiriki kikamilifu katika juhudi za kuzifikia jamii na kukuza ushawishi wa Urusi.

BBC imekuwa ikifuatilia chaneli za Telegram za African Initiative na kurasa za Facebook, ambapo video, picha, na ripoti za kazi zao mashinani zinawekwa.

Huko Burkina Faso, tulipata ripoti kuhusu shindano la mpira wa miguu ambapo wimbo wa taifa wa Urusi ulipigwa, shuleni wanafunzi wanafundishwa kuhusu Urusi, mashindano ya sanaa ya mapigano ya Soviet, warsha za huduma ya kwanza kwa raia na polisi na tamasha la uchoraji ambapo washiriki walimchora Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na kiongozi wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara, yote yakifadhiliwa na African Initiative.

Picha pia zinaonyesha wanachama wa African Initiative wakisambaza bidhaa za chakula kwa wenyeji na wakionyesha makala ya The Tourist iliyotolewa na Wagner, kuhusu kundi la wakufunzi wa Wagner katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo Wagner wamekuwa wakiisaidia serikali kupambana na waasi kwa miaka kadhaa.

"Wazo la awali na African Initiative lilikuwa ni kufuta chochote ambacho Prigozhin ilibuni na kuleta vitu vipya. Baadaye katika mchakato huo, ilionekana ni busara zaidi kutumia tena maudhui yote ambayo tayari yalikuwa,” "anasema mtafiti Czerep kutoka Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Poland.

Uhusiano na ujasusi wa Urusi

aszx

FSB, Shirika la Usalama ya Shirikisho ya Urusi, lina jukumu muhimu katika shirika jipya, anabainisha.

Mkuu na mhariri mkuu wa African Initiative ni Artyom Kureyev, anayetambuliwa na wataalamu wa Urusi kama wakala wa FSB. Kureyev anahusishwa na Valdai Club, kituo cha wataalamu chenye makao yake mjini Moscow kilicho karibu na Rais Putin.

Tovuti ya African Initiative inamuorodhesha Anna Zamaraeva, afisa wa habari wa zamani wa Wagner, kama naibu mhariri mkuu.

Viktor Lukovenko, mmoja wa wataalamu wa teknolojia wa Prigozhin alianzisha ofisi ya Burkina Faso ya African Initiative lakini aliacha nafasi hiyo katika miezi ya hivi karibuni.

Tuliwasiliana na African Initiative kwa maoni. Ofisi yake huko Moscow ilithibitisha kuwa imepokea maswali yetu lakini haikujibu. Pia tuliwasiliana na serikali ya Urusi lakini hatukupata jibu.

Mwezi Februari, katika kujibu ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, makala kwenye tovuti ya African Initiative ilisema bodi yake ya wahariri "inasisitiza kwamba madhumuni yake ni kueneza taarifa kuhusu Afrika nchini Urusi na kuifanya Urusi kuwa maarufu katika nchi za Afrika," ikitoa fursa mbalimbali kwa Waafrika kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na ukosoaji wao kwa nchi za Magharibi.”

Wakati huo huo, shirika hilo linaendelea kuimarisha shughuli zake katika Sahel. Wiki ya mwisho ya Agosti, takribani wanafunzi 100 nchini Burkina Faso walihudhuria warsha kuhusu fursa za mafunzo nchini Urusi.

"Nilijifunza kuhusu utamaduni wa Urusi na uhusiano kati ya serikali zetu," alisema kijana anayetabasamu aliyevalia fulana yenye nembo ya African Initiative kwenye video iliyorekodiwa baada ya majadiliano.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah