Afcon 2023: Nahodha wa Morocco, Romain Saiss na matarajio yao baada ya mafanikio Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Mark Lomas
- Nafasi, BBC
Wakati Morocco watakaposhuka dimbani dhidi ya Tanzania mechi yao ya ufunguzi ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 Januari 17, itakuwa ni miezi 13 tangu wamalize mbio za kihistoria za Kombe la Dunia la 2022 baada ya kushindwa kupata nafasi ya tatu walipofungwa na Croatia.
Lakini imeweka historia ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia. Timu hiyo inawinda taji la kwanza la bara tangu 1976, ni miaka 48 imepita.
Nahodha wa Morocco, Romain Saiss anasema, "kwa kweli kuna kitu kimebadilika. Ni wazi itakuwa vigumu kufika nusu fainali ya kila mashindano, lakini tunatakiwa kubaki katika kiwango kizuri na kusaidia soka la Morocco kuendelea kukua. Na sihisi kama ni shinikizo, bali ni jukumu. Tumeonja ladha na sasa tunataka zaidi."
Kikosi cha Walid Regragui kiko nafasi ya 13 katika viwango vya ubora duniani, lakini mlinzi wa zamani wa Wolves, Saiss anasisitiza hadhi yao ya kuwa timu bora Afrika haiwafanyi kuwa ndio washindi wa taji la Afcon mwezi Februari."
Morocco, pia itacheza na DR Congo na Zambia katika Kundi F. Hawajafika fainali tangu 2004, walipofungwa 2-1 na Tunisia.
"Nafikiri Ivory Coast watakuwa na presha kwa sababu wanacheza nyumbani. Kuna timu nyingi hatari na zenye uzoefu mkubwa pia, kama Senegal, Cameroon, Algeria na Misri.
“Unaweza kuona Afrika kila mchezo ni mgumu, lolote linaweza kutokea, yatakuwa ni mashindano magumu na tunatakiwa kuwa tayari kiakili ili kufika mbali iwezekanavyo. Nadhani haya yatakuwa moja ya [mashindano] magumu katika historia."
Mashindano Hayatabiriki

Chanzo cha picha, Getty Images
Morocco, katika kumbukumbu za hivi karibuni, imekuwa miongoni mwa timu isiyofanya vizuri katika Afcon.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Walishindwa kutinga hatua ya makundi katika michuano mitano kati ya 2006 na 2013, na katika mashindano matatu yaliyopita wametolewa mara mbili katika robo fainali na Misri na mara moja katika 16 bora na Benin.
Saiss alicheza katika kila mechi kati ya hizo tatu za hatua ya mtoano na anasisitiza yeye na kikosi chake wamejiandaa vyema wakati huu ingawa mashindano hayo hayatabiriki.
Timu ya Zambia walipata ushindi wa Afcon mwaka 2012, na kuonyesha kwamba mshindi anaweza kutoka katika timu yoyote.
"Tunajua kila mtu anatusubiri na anataka kutushinda, lakini tunaweza kuwa na mafanikio makubwa," anasema Saiss mwenye umri wa miaka 33 - kwa sasa anachezea klabu ya Saudi Pro League, Al-Shabab. .
"Haijalishi timu. Kwetu muhimu ni kuwa makini kwa kila mchezo na sio kufikiria hatua inayofuata. Litakuwa kosa kubwa tukifanya hivyo. Lengo kuu kwa sasa ni kufuzu makundi."
"Tunahitaji kuwa tayari kuteseka kwa sababu itakuwa kazi ngumu. Kwenye Kombe la Dunia tulifika mbali kwa sababu kila mtu alijitolea mwili wake kutinga nusu fainali."
Kusonga mbele Morocco hadi hatua ya nne bora nchini Qatar kulisaidiwa kwa kiasi kikubwa na safu yao ya nyuma, huku Saiss akipanga safu yake ya ulinzi na kuweka rekodi ya kutofungwa mabao mengi na Croatia, Ubelgiji, Uhispania na Ureno.
Kipa Bono (sasa yuko Saudi Arabia, na Al Hilal), beki wa kulia Achraf Hakimi (Paris St-Germain), beki wa kushoto Noussair Mazraoui (Bayern Munich) na beki wa kati Nayef Aguerd (West Ham) - walichaguliwa pamoja na nahodha na anatumai uimara wa safu ya ulinzi utaendelea kwenye Afcon.
“Nina ushirikiano mzuri na Nayef kwa sababu nimemfahamu kwa miaka mingi na nimemuona akikua,” anasema Saiss.
"Tuna uhusiano mzuri sana nje ya soka na hilo ni muhimu kwangu. Tunazungumza sana kuhusu michezo na kujaribu kuboresha ushirikiano wetu.
"Timu [nzima] ilikuwa ikifanya kazi kwa bidii [kwenye Kombe la Dunia] na tunaweza kuona jinsi ilivyo muhimu kutoruhusu mabao katika mashindano makubwa. Tukikaa imara, tunaweza kufika mbali sana kwenye mashindano."
Kocha ni kama Kaka Mkubwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Saiss pia amemzungumzia kocha wa Atlas Lions, Regragui kuhusu mafanikio ya hivi karibuni ya Morocco, "ni mtu ambaye yuko karibu sana na wachezaji. Ana urafiki na viongozi wa timu, kuanzia mdogo hadi mkubwa, yuko karibu na kila mtu.
"Ni kama kaka mkubwa au mjomba na anakufanya ujiamini. Kila mara hutupa maneno ya hamasa" anasema nahodha.
Nchi hiyo imewekeza pakubwa katika miundombinu ya kandanda baada ya majaribio matano kufeli, Morocco ilitangazwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la 2030 pamoja na Ureno na Uhispania.
Wakati Saiss akifurahia habari hizo, atakuwa na umri wa miaka 40 wakati mashindano yatakapo fanyika Afrika Kaskazini kwa mara ya kwanza.
Beki huyo anapofikiria kitakachofuata baada ya maisha yake ya uchezaji kumalizika. Je, kuna nafasi yoyote ya kuwa sehemu ya timu hiyo mwaka 2030?
"Inawezekana," Saiss anatabasamu.
"Ninajiuliza nini nataka kufanya baada ya mpira wa miguu, kusema ukweli, sijui. Nina mapenzi na mpira wa miguu na naweza kutazama mechi tano au sita kwa siku - kwa sababu napenda. Mchezo huu ni sehemu kubwa ya maisha yangu.
"Ninavutiwa sana na kufundisha. Ndiyo maana napenda kuwa na uhusiano mzuri na kocha wangu ili nijifunze mambo mapya."
Saiss huenda akashiriki Kombe lijalo la Mataifa ya Afrika, litakaloandaliwa nchini Morocco 2025. Kwa sasa, yeye na wachezaji wenzake wanalenga kumaliza ukame wa muda mrefu wa kombe la Afcon na kuhakikisha wanaingia kwenye mashindano ya 2025 katika ardhi ya nyumbani kama mabingwa watetezi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












