Mahali pabaya zaidi duniani kuwa mtoto

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo barani Afrika ndiyo sehemu mbaya zaidi ya kuwa mtoto na hali inazidi kuwa mbaya.

"Ukilinganisha takwimu za mwaka jana na mwaka huu, kuna ongezeko la asilimia 47 ya ukatili wa kijinsia. Hili ni kubwa," anasema Sheema Sen Gupta.

Yeye ni mkurugenzi wa ulinzi wa watoto katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef ​​na alizungumza na BBC baada ya kutembelea kambi za wakimzi za mashariki mwa nchi mwishoni mwa Septemba.

"Ukiangalia eneo la mashariki mwa nchi, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini pekee, wasichana wanne kati ya watano wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia," anasema.

Nchi hiyo ina ukubwa wa Ulaya Magharibi na nyumbani kwa watu milioni 100, pamoja na hifadhi kubwa ya madini.

Mwaka wa 2022, Unicef ​​ilirekodi visa 3,400 vya 'ukiukwaji mkubwa' dhidi ya watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ni pamoja na watoto 1,600 kuingizwa kwenye vikundi vyenye silaha, 700 kuuawa katika vita na karibu visa 290 vya unyanyasaji wa kijinsia.

"Nikiwa katika kitengo cha ulinzi wa watoto, ninafahamu kinachoendelea. Lakini unapoenda huko na kukutana na watoto na vijana, hali unayopatana nayo inakugusa sana. Nilisikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto hawa.

"Tangu mwanzoni mwa 2023, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kufanya jumla ya waliokimbia makazi yao kufikia zaidi ya milioni 6.1.

Machafuko na kutokuwa na utulivu

Mzozo huo ulizuka miongo mitatu iliyopita na kusababisha vifo vya zaidi ya milioni sita.

Katika mwaka uliopita, ghasia zimeongezeka huku vikosi vya usalama vikipambana dhidi ya zaidi ya makundi 100 yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo, licha ya kuwepo kwa operesheni kubwa ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.

Tangu Februari, kundi la waasi la M23 limekuwa likiteka eneo.

Kundi hilo lilibuniwa muongo mmoja uliopita na linadai kutetea masilahi ya jamii ya Watutsi wanaoishi DR Congo dhidi ya wanamgambo wa Kihutu. Mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono.

Watu waliofurushwa katika vijiji vyao mara nyingi huishia kwenye kambi kubwa kama vile Rhoe aliyotembelewa na Sen Gupta.

Iko kilomita 45 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Bunia na inalindwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, inatoa ulinzi mdogo kwa wasichana wengi wachanga.

Sylvia (jina limebadilishwa) ana umri wa miaka 16 tu lakini tayari ni mama wa mtoto wa miezi 10 aliyezaliwa baada ya tukio la ubakaji. BBC ilizungumza naye mbele ya mwalimu wake kupitia mfasiri wa Unicef.

"Nilishambuliwa ndani ya kambi nilipokuwa nikirudi baada ya kuchota maji," aliambia BBC. " kisa hicho kilitokea baada ya jua kutua. Simjui mshambuliaji. Kulikuwa na giza sana."

Baadaye, watu walikusanyika karibu naye lakini hakuna aliyemsaidia. Anadhani mbakaji wake bado anaranda randa kambini.

"Nina hasira na hofu. Vijana wote wanahofia usalama wao."

Baada ya pengo la miaka mitatu, sasa amerejea shuleni kama sehemu ya mchakato wa ukarabati.

"Nikiwa shuleni, mama yangu humtunza mtoto wangu. Ninaporudi nyumbani, namtunza," anasema Sylvia.

Makazi yake yametengenezwa kwa fiti za mianzi na matope yaliyowekwa juu na karatasi ya turubai. Haina umeme. Kuna choo kimoja tu cha watu wapatao 50.

"Giza linapoingia sio salama kuingia kambini. Hakuna chakula cha kutosha," Sylvia anaendelea.

"Sina baba. Niko na mama yangu. Sina mwanamume wa kulinda familia yetu. Kuondoka kwenye makao yetu baada ya jioni kwenda kuchota maji kunaweza kuwa hatari kwa wasichana."

Sylvia alipokea ushauri nasaha ili amkubali mtoto wake.

Mtoto wake alipiga kelele sana wakati nikizungumza na mama Sylvia Georgina.

"Wiale ni mzima wa afya, mcheshi na ana uchu wa kujua," anasema bibi wa miaka 40 Georgina.

Georgina anapata pesa kwa kuwafanyia wengine kazi za ndani. Yeye ni mjane na anahisi kutengwa.

"Ni vigumu kwa mama yake kumtunza mtoto. Yeye (Sylvia) ni mtoto poa," Georgina anasema.

Maisha kambini

Sylvia na mama yake Georgina walitimuliwa miaka mitatu iliyopita kutoka katika kijiji cha jirani ambacho kilivamiwa na wanamgambo. Hawajui ni lini watarudi nyumbani.

"Binti yangu mara nyingi hukasirika. Yeye huwaza juu ya shambulio hilo. Pia huwa na hali ya kubadilika-badilika na kutojali."

Mkuu wa shule hiyo, Lonu Bauojo Innocent, ndiye aliyemchochea Sylvia kuhudhuria darasani.

"Kuna wengi kama yeye hapa. Ni mwerevu sana na kuhudhuria shule kutamsaidia kurejea katika maisha ya kawaida."

Kwa kuwa wasichana wengi hubakwa baada ya giza kuingia, matangi mapya ya maji yamewekwa ndani ya kambi hiyo ili kupunguza hatari hiyo. Wanawake pia hutembea kwa makundi ili kuimarisha usalama wao.