Mapinduzi ya Niger: Rais Bazoum aonesha ukaidi baada ya kuondolewa madarakani

Rais wa Niger Mohamed Bazoum ametoa ujumbe wa kuonesha ukaidi kwenye Twitter baada ya wanajeshi kutangaza mapinduzi usiku kucha katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Matatizo yalianza mapema Jumatano wakati wanajeshi kutoka kwa walinzi wa rais walipomchukua mateka.

Waziri wake wa mambo ya nje amesema mapinduzi hayo hayaungwi mkono na jeshi zima, lakini mkuu wa jeshi sasa amesema anaunga mkono utawala wa kijeshi.

Bw Bazoum ni mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu.

Marekani na Ufaransa zote zina kambi za kijeshi katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini ya uranium - na zimelaani mapinduzi hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alimpigia simu Bw Bazoum akiahidi "uungwaji mkono usioyumba" wa Marekani na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wametaka rais huyo aachiliwe mara moja.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 64, ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Niger miaka miwili iliyopita, aliandika kwenye mtandao wa Twitter siku ya Alhamisi asubuhi na kusema: "Mafanikio yaliyopatikana kwa bidii yatalindwa. Wananchi wote wa Niger wanaopenda demokrasia na uhuru watashuhudia hilo."

Mji mkuu, Niamey, kwa sasa hauna watu, lakini hii ni kwa sababu mvua imekuwa ikinyesha asubuhi yote.

Hata maandamano yaliyopangwa na wanaounga mkono mapinduzi hayajafanyika.

Lakini watu nchini Niger wamegawanyika vikali kuhusu mabadiliko ya matukio.

Wengine wameshtuka na kufadhaika na ilipokuwa ikiendelea siku ya Jumatano, mamia ya wafuasi wa rais walikaidi wanajeshi hao kwenda mitaani na kuwataka wanajeshi kurejea kambini.

Walitawanyika baada ya risasi kurushwa kama onyo - milio ya risasi pekee iliyosikika katika mapinduzi haya ya mamlaka bila kumwaga damu.

Wamesema hawatakubali mapinduzi hayo lakini haijabainika watayapinga vipi.

Hawajaitisha maandamano yoyote mitaani kwa wakati huu.

Wengine wamefurahishwa na hatua za jeshi, wakishutumu chama tawala kilichoondolewa madarakani kwa ufisadi na kutofanya vya kutosha kuboresha hali ya usalama na kumaliza uasi wa muda mrefu wa wanajihadi.

Nchi mbili jirani, Mali na Burkina Faso, zimekumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya wanajihadi katika miaka ya hivi karibuni.

Katika nchi zote mbili viongozi hao wapya wa kijeshi wamesogea karibu na Urusi baada ya kutofautiana na Ufaransa, mkoloni wa zamani, ambayo pia ilitawala Niger zamani.

Uchambuzi na Frank Gardner

Mapinduzi haya bado ni habari mbaya zaidi kwa juhudi za Ufaransa na Magharibi kurejesha utulivu katika eneo la Afrika Magharibi linalojulikana kama Sahel.

Wakati nchi jirani ya Mali ilipochagua kushirikiana na Kundi la Wagner la Urusi badala ya Wafaransa, Ufaransa ilihamisha kituo cha kuendesha shughuli zake katika eneo hilo hadi Niger.

Mapinduzi haya, hata kama yatatokea kuwa ya muda mfupi, yameonyesha kwamba hata Niger haiwezi kutegemewa kuwa msingi salama wa kudumu.

Ushawishi wa Magharibi katika eneo hilo unapungua kama bwawa la maji wakati wa kiangazi.

Serikali za Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Mali zote zimeamua kwamba zingependelea kufanya kazi na mamluki wakatili wa Wagner wa Urusi kuliko jeshi lolote la Magharibi.

Maslahi ya msingi ya Wagner barani Afrika yameonekana kuwa zaidi ya kujitajirisha na kupanua ushawishi wa Kremlin kuliko kufuata malengo ya Magharibi ya kujaribu kukuza utawala bora.

Kwa makundi mawili makubwa ya waasi katika kanda, yale yanayohusishwa na kile kinachoitwa Islamic State na al-Qaeda, hii ni habari njema.

Wanastawi kwa kukosekana kwa utulivu, utawala mbovu na chuki za serikali za mitaa.

Kwa hivyo mapinduzi nchini Niger huenda yakatatiza zaidi juhudi za kuyadhibiti.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger Hassoumi Massoudou ametoa wito kwa wakazi kupinga mapinduzi hayo.

Katika mahojiano na France24, alisema kuwa hali hiyo bado inaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na kusema wajumbe waliotumwa kutoka nchi jirani ya Nigeria walikuwa wakizungumza na jeshi.

Rais wa Benin Patrice Talon pia yuko kwenye ujumbe wa upatanishi kwa niaba ya jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas.

Kwa sasa, haijulikani ni nani anayesimamia.

Unyakuzi huo ulitangazwa na msemaji, Kanali Maj Amadou Abdramane, ambaye alisema unyakuzi huo ulichochewa na kuzorota kwa hali ya usalama "na utawala duni wa kiuchumi na kijamii".

Kwa sasa, hakuna dalili ya kuhusika kwa Urusi katika mapinduzi haya, au ushawishi fulani nchini Niger.

Nchi hiyo kubwa kame kwenye ukingo wa jangwa la Sahara – moja ya mataifa maskini zaidi duniani - imekumbwa na mapinduzi manne tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, pamoja na majaribio mengi ya mapinduzi.