Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, unazijua nchi tano zisizo na viwanja vya ndege?
Takribani nchi zote duniani zina zaidi ya kiwanja kimoja cha ndege. Lakin kuna nchi tano ambazo hazina uwanja hata mmoja wa ndege. Nchi zote hizo ziko barani Ulaya. Ni nchi gani hizo?
Andora
Andorra ni nchi isiyo na bahari kati ya Uhispania na Ufaransa, na ndiyo nchi kubwa zaidi kwenye orodha ya nchi zisizo na uwanja wa ndege.
Ukubwa wa Andorra unakadiriwa kuwa kilomita za mraba 468 na ina wakazi 100,000. Viwanja vya ndege vya karibu zaidi ni Uwanja wa ndege wa Barcelona, El Prat nchini Uhispania na Toulouse nchini Ufaransa.
Viwanja vya ndege vya Toulouse na Barcelona vyote vipo umbali wa masaa matatu kutoka Andorra.
Liechtenstein
Liechtenstein ni nchi isiyo na bahari iliyoko kati ya Uswizi na Austria. Eneo lake ni kilomita za mraba 160 au maili za mraba 62, na ina wastani wa watu 35,000.
Uwanja wa ndege wa karibu zaidi na Lichtenstein ni uwanja wa ndege wa Zürich nchini Uswizi ambao uko umbali wa kilomita 130 au maili 80.
Uwanja wa ndege mwingine wa karibu ni St. Gallen, ambao pia uko Uswizi na uko umbali wa kilomita 50 au maili 30. Liechtenstein ina uwanja wa ndege mmoja mdogo kwa matumizi ya helikopta ambao uko Balzers.
Monaco
Monaco inapakana na Ufaransa kwa pande tatu na bahari ya Mediterania upande mmoja.
Monaco ni nchi ya pili kwa udogo duniani ikiwa na eneo la ardhi la kilomita 2.02 tu au maili za mraba 0.78, na idadi ya watu 36,371.
Uwanja wa ndege wa karibu zaidi na Monaco ni uwanja wa ndege wa Côte d'Azur huko Nice, Ufaransa. Monaco ina uwanja mmoja mdogo katika wilaya ya Fontvieille.
San Marino
San Marino ni nchi ndogo isiyo na bahari iliyozungukwa pande zote na Italia. Eneo la ardhi la San Marino ni takriban kilomita za mraba 61 au maili za mraba 24, na inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 30,000.
Uwanja wa ndege wa karibu ni uwanja wa kimataifa wa Federico Fellini huko Rimini, Italia.
San Marino ina uwanja wa ndege mmoja wa kibinafsi huko Torraccia na uwanja mdogo wa ndege huko Borgo Maggiore.
Vatican
Vatican ndio nchi ndogo zaidi ulimwenguni, yenye eneo la hekta 44 na idadi ya watu takriban 840.
Ikizungukwa kabisa na mji mkuu wa Roma, Italia, Vatican haina uwanja wa ndege au barabara kuu. Ina uwanja mmoja mdogo ambao hutumiwa na Papa na viongozi wageni.