Je, serikali za Afrika Mashariki zinaungana kuwanyamazisha wapinzani?

h

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, Ukandamizaji wa Kenya dhidi ya waandamanaji mwaka jana umechafua taswira yake kama mwanga wa demokrasia
Muda wa kusoma: Dakika 7

Kenya imekumbwa na wimbi la ukandamizaji wa hivi majuzi, na kuharibu sifa yake ya kuwa kinara wa demokrasia Afrika Mashariki.

Wakosoaji wanahofia kwamba inafuata mkondo wa majirani zake - Uganda na Tanzania, ambazo zina zinatajwa kuwakandamiza wapinzani.

Sheria za Kenya zinachukuliwa kama sheria endelevu - hasa katika kulinda uhuru wa kimsingi kama vile haki ya kuandamana.

Lakini Kenya imeshuhudia ongezeko la ukandamizaji dhidi ya maandamano - mfano wa hivi punde zaidi ukiwa mauaji ya takriban watu 10 katika maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali ya Rais William Ruto wakati ilipojaribu kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya televisheni na redio kuhusu maandamano hayo.

"Utawala wa Walaghai" - kilitangaza kichwa cha habari cha gazeti linaloheshimika la Standard nchini Kenya likieleza kwamba vijana walikuwa wamefurika barabarani wakiwakumbuka watu waliouawa kwa kupigwa risasi mwaka mmoja uliopita katika maandamano ya kupinga ushuru lakini "Badala ya kusikilizwa walikutana na kizuizi cha waya unaokata, malori ya kivita na ukandamizaji".

Lakini kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen, polisi walionyesha "ustahimilivu wa ajabu" walipozuia "jaribio la mapinduzi".

"Tunawalaani wahalifu kwa uhalifu ambao kwa jina la maandamano ya amani walianzisha wimbi la vurugu, uporaji, unyanyasaji wa kijinsia na uharibifu kwa watu wetu," alisema, akiwashutumu waandamanaji kwa kushambulia vituo vya polisi na kujeruhi askari 300.

Hata hivyo, Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kiliishutumu polisi kwa namna ilvyoshughulikia maandamano hayo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Uchokozi usio wa lazima na nguvu za kikatili ambazo ziliishia katika upotevu usio na maana wa maisha na uharibifu usio na maana wa mali hauna nafasi katika jamii huru ya kidemokrasia," ilisema.

Ukandamizaji huo ulikuja wiki chache baada ya mwanablogu na mwalimu mwenye umri wa miaka 31, Albert Ojwang, kufariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi . Alikamatwa baada ya kushutumiwa kwa kumkashifu afisa mkuu wa polisi - na alikufa akiwa kizuizini kwa majeraha ya kushambuliwa, uchunguzi wa maiti ulieleza.

Kifo chake kilisababisha maandamano madogo katika mji mkuu, Nairobi, ambayo polisi w pia mchuuzi wa barabarani, ambaye alijipata katika mapigano hayo - alipigwa risasi kwa karibu, na sasa amelazwa hospitalini akiwa mahututi.

LSK ililaani kupigwa risasi kwake na kusema hakufai kwa "demokrasia yoyote iliyo timamu".

Maoni yake yaliweka wazi ukweli kwamba Kenya ina hatari ya kupoteza hadhi yake kama demokrasia ambayo Watanzania wengi na Waganda waliihusudu - na kupata msukumo kutokana nayo.

Mchambuzi wa siasa za Tanzania Nicodemus Minde alisema kwa muda mrefu kumekuwa na "kuthamini" kati ya Watanzania juu ya uwezo wa Wakenya "kuzungumza ukweli kwa mamlaka".

Ni maoni ya kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ambaye aliiambia BBC mwaka jana kwamba "Hatujasisitiza vya kutosha kuleta mageuzi ya kidemokrasia".

"Kile Kenya ilichokifanya kujenga nafasi yake ya kidemokrasia ni jambo tunalohitaji kufanya," alisema.

Baada ya kunusurika kimiujiza jaribio la kuuawa baada ya kupigwa risasi 16 mwaka 2017, Lissu amekuwa ishara ya ukandamizaji wa serikali nchini Tanzania.

Kwa sasa yuko kizuizini, akishtakiwa kwa uhaini kwa kuwakusanya wafuasi wake chini ya kauli mbiu "Hakuna mageuzi; hakuna uchaguzi".

Serikali iliona hili kama jaribio la Lissu kuanzisha uasi - na ana hatari ya kuhukumiwa kifo ikiwa atapatikana na hatia.

Kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 57 anaona kuzuiliwa kwake kama jaribio la Chama Cha Mapinduzi (CCM) - ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1961 - kusafisha njia yake ya ushindi katika uchaguzi wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika Oktoba.

Mtazamo huo umetiwa nguvu na ukweli kwamba chama chake cha Chadema kimezuiwa kushiriki uchaguzi huo baada ya kukataa kutia saini kanuni ya maadili ya uchaguzi ambayo kiliamini kuwa ingedhoofisha haki yake ya kufanya kampeni kwa uhuru.

Upinzani nchini Uganda unajiona katika hali kama hiyo, ukisema kwamba Rais Yoweri Museveni amekuwa madarakani kwa karibu miaka 40, na - pamoja na mwanawe, Muhoozi Kainerugaba, ambaye anaongoza jeshi - wanakabiliana na wapinzani wa kisiasa katika maandalizi ya uchaguzi wa mapema 2026.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amekuwa kizuizini tangu mwezi Novemba, huku serikali ikitaka kumshtaki kwa uhaini katika mahakama ya kijeshi baada ya kumtuhumu kupanga njama ya kupindua serikali - mashtaka ambayo anayakanusha.

Unaweza pia kusoma:
h

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, ''Tunaangalia mzozo wa kikanda - sio mzozo wa kiuchumi, sio mzozo wa biashara, lakini demokrasia yenyewe''-Martha Karua wakili wa haki za binadamu wa Kenya

Ingawa Kenya ina mahakama huru na hufanya uchaguzi wa mara kwa mara unaosababisha mabadiliko ya mamlaka, Martha Karua - mmoja wa wanasheria wa haki za binadamu anayeheshimika zaidi nchini humo, waziri wa zamani wa sheria na kiongozi wa chama kidogo cha upinzani - anaamini kuwa demokrasia iko hatarini katika mataifa yote matatu ya Afrika Mashariki.

"Tunaangalia mgogoro wa kikanda - sio mgogoro wa kiuchumi, si mgogoro wa biashara, lakini wa demokrasia yenyewe," alisema katika mkutano wa waandishi wa habari hivi karibuni.

Wanaharakati kama yeye wamesikitishwa na ukweli kwamba zaidi ya Wakenya 80 wametekwa nyara mwaka uliopita na watu ambao hawakuwahi kujitambulisha, jambo linalozua hofu kwamba huo ndio ulikuwa mkakati wa hivi punde wa serikali kuzima upinzani baada ya maandamano ya kupinga hatua za kuongeza ushuru huku kukiwa na mzozo wa gharama ya maisha.

Pia kuna ushahidi unaoongezeka kuwa Kenya si mahali salama tena kwa Waganda na Watanzania, huku vyombo vya usalama kutoka mataifa hayo matatu vikionekana kushirikiana kukabiliana na upinzani.

Besigye alikuwa Nairobi kwa ajili ya uzinduzi wa kitabu mwezi Novemba, wakati alitoweka - na kujitokeza siku nne baadaye katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda .

Serikali nchini Uganda ilimshutumu kwa kujaribu kufanya mazungumzo ya mpango wa silaha nchini Kenya ili kuanzisha uasi nyumbani na kusema kuwa alikamatwa katika operesheni ya kuvuka mpaka iliyofanywa na huduma za kijasusi za Kenya.

Awali serikali ya Kenya ilikanusha hilo, ikisema kuwa haifahamu kuhusu operesheni ya Uganda katika ardhi yake, ingawa waziri wa mambo ya nje wa Kenya hivi majuzi aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa "kulikuwa na masuala fulani" kuhusu ziara ya Besigye nchini Kenya na "ilibidi aende". Hakufafanua.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kizza Besigye wa Uganda alitekwa nyara vibaya alipokuwa ziarani nchini Kenya mwezi Novemba na kurudishwa Uganda kujibu mashtaka katika mahakama ya kijeshi.

Takriban miezi miwili baada ya mateso ya Besigye, mwanaharakati wa Tanzania aliye uhamishoni Maria Sarungi Tsehai alisema alitekwa nyara na watu wenye silaha jijini Nairobi ambao kwa bahati nzuri wakamwachia saa kadhaa baadaye.

Bi Tsehai alisema alishikwa mkono na kubanwa na wavamizi wanne ambao walimlazimisha kuingia kwenye gari .

"Nina hakika kwamba sababu ya kutekwa nyara ilikuwa kupata ufikiaji wa mtandao wangu wa kijamii na [kwa sababu ya] kazi ya kufichua ambayo ninafanya," alisema, huku watekaji nyara wake wakiendelea kuuliza jinsi ya kufungua simu yake.

Bi Tsehai ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na ameishutumu serikali yake kwa kurudisha "udhalimu" nchini, licha ya kuahidi mageuzi alipoingia madarakani mwaka 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli.

Karua alisema licha ya "kurudi nyuma" kwa demokrasia na haki za binadamu katika Afrika Mashariki, kulikuwa na wasiwasi mdogo kuhusu hili kimataifa, na Umoja wa Afrika umekua "kimya", Umoja wa Mataifa ukitoa "maneno - yasiyo ya kurekebisha", wakati Marekani - "iliyojitangaza kuwa bingwa wa uhuru" - ikikabiliana na "maswala yake ya uhuru" chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

Tanzania ilimfukuza Karua na wanaharakati wawili wa Kenya walipoingia nchini mwezi Mei kuonyesha mshikamano na Lissu , huku mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na wakili wa Uganda Agather Atuhaire wakizuiliwa baada ya kuruhusiwa kuingia.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mkenya Boniface Mwangi na Muganda Agather Atuhaire wanadai waliteswa kingono walipokuwa wakizuiliwa nchini Tanzania mwezi uliopita.

Baada ya kuachiliwa, wote wawili walishutumu polisi wa Tanzania kwa kuwadhalilisha kingono.

Polisi wa Tanzania walikanusha shtaka hilo, hata hivyo huku kukiwa na kilio cha kuzuiliwa na kufukuzwa kwa wanaharakati wa kigeni, Rais Samia alitoa onyo kali.

"Kama wamezuiliwa katika nchi yao, wasije kuingilia hapa. Tusiwape nafasi. Tayari wameanzisha machafuko katika nchi yao," alisema.

Kwa masikitiko ya wanaharakati, Rais Ruto wa Kenya alishindwa kukemea madai ya unyanyasaji huo na badala yake, aliomba radhi kwa serikali ya Tanzania.

"Kwa majirani zetu wa Tanzania, ikiwa tumekukosea kwa namna yoyote tusamehe," alisema.

"Ikiwa kuna jambo lolote ambalo Wakenya wamefanya ambalo si sawa, tunataka kuomba msamaha."

Macharia Munene, profesa wa Kenya katika uhusiano wa kimataifa, aliiambia BBC kwamba msamaha wa Ruto ulitokana na "kufikiriwa kushindwa kuwazuia watu [Wakenya]".

Aliongeza kuwa serikali ya Tanzania imekuwa ya "kuchanganyikiwa" na ushawishi unaowezekana wa wanaharakati wa Kenya kwenye uchaguzi wa Oktoba, huku serikali ya Ruto ikiwa chini ya shinikizo la "kujumuisha wasumbufu".

Kwa wanaharakati wa Kenya ukandamizaji unaozidi kuwa mbaya katika nchi hizo tatu umeimarisha azma yao ya kukabiliana na ukandamizaji.

Bw Mwangi, mmoja wa wanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini Kenya alihitimisha kwa kusema: "Ikiwa watu hawa wataungana kuwakandamiza raia wao, basi lazima tushikamane katika kupigania kuwaondoa mamlakani."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi