Namna kuku wa kienyeji walivyogeuka benki ya Kaya na kitoweo cha ndoto

    • Author, Eagan Salla
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

"Niliuza kuku, nikalipa mahari"

Si hadithi ya kufikirika, si fumbo la kitabu cha fasihi, bali ni simulizi hai ya mwanaume halisi, Juma Hamis Sakume, mkazi wa Singida, ambaye manyoya ya kuku wa kienyeji yalimfungulia mlango wa ndoa. Wakati wengine wakishikilia bahasha au mikoba, yeye alishikilia kikapu cha kuku watano na hatimaye akaweka historia kwenye ukoo wake.

Kuna Methali ya Kiswahili inayosema: "Usimdharau mwenye manyoya, hujui alikopitia." Kwa wakazi wa Singida, kuku si kiumbe wa kupita tu, ni sehemu ya asili yao, ni urithi wa vizazi, na ni maisha yenyewe. Hakika kila jogoo anayewika asubuhi huamsha matumaini mapya kwa familia.

Kwenye kaya nyingi vijijini mkoani Singida, kuku wa kienyeji wamekuwa ni hazina ya iliyo mikononi mwao yenye uwezo wa kujitegemea bila kupiga hodi benki. Wakati mwingine ni ada ya mtoto, wakati mwingine ni majibu ya dharura ya ugonjwa au mahitaji mengine ya shuleni. Kwa wengi, kuku wamekuwa "bima ya maisha bila karatasi."

"Mwaka 1985 niliuza kuku watano, kila mmoja shilingi mia tano. Kaka yangu akaniongezea mia tano nikalipa mahari," anasema Sakume

Ni simulizi ya kweli ya namna kuku walivyomjengea maisha mapya, na hadi leo, anawakumbuka kuku wale kwa heshima ya pekee.

Changamoto za asili

Kuku hasa wa asili ni utamaduni wa kizazi na kizazi Singida, tofauti yake ni namna wanavyofugwa tu. Zamani hizo, ufugaji wa kuku haukuhitaji banda wala vifaa vya kisasa. Mfugaji aliwafungulia asubuhi, wakajitafutia riziki porini na kurejea jioni. Kuku walikuwa sehemu ya mazingira, wakitembea kwa uhuru kama wakazi halali wa kijiji au mtaa.

Lakini leo, hali imebadilika. Ardhi imezidi kuwa finyu, watu wameongezeka, shughuli za kibinadamu zimesambaa kila kona. Kuku wa Singida hawezi tena kupiga kelele hovyo bila kuambulia lawama kutoka kwa jirani. Na si hivyo tu wizi wa kuku umekuwa kama janga la kimya kimya, linalopukutisha matumaini ya wafugaji wengi.

"Wanakuja usiku, wanakufungia ndani, wanaondoka na kuku wote. Hata kuku wa mayai hawaachi," Sakume anasimulia kwa masikitiko

"Kuku Festival- Tamasha linaloendeleza alama

Mwaka huu, Singida imekuja na tamasha la kuku. Kusheherekea na kudumisha utamaduni wa ufugaji wa kuku Singida. Mkuu wa Mkoa, Halima Dendegu, alizindua Tamasha hilo kuenzi jogoo na kuku wa kienyeji waliopo ndani ya kaya na mioyo ya watu.

Usiku wa tamasha hilo lililofanyika hivi karibuni, mji uliwaka kama siku ya mavuno. Mbavu zilivunjika kwa vicheko, nyama ikachomwa hadi asubuhi, na jogoo waliheshimiwa kwa ladha yao ya kipekee.

"Tulikesha, hakuna aliyetoka mikono mitupu. Kila mtu alipata paja au kipapatio," anasema Ally Ramadhan

Zaidi ya kuku 500 walichinjwa. Bei zilipanda kutoka shilingi dola 8 mpaka dola 9.50 kama kutoka Shilingi 22,000 hadi 25,000 za Tanzania kwa kuku mmoja.

Wafanyabiashara walipata siku ya neema wale waliokuwa na vifaranga walitamani wawakuze kuku wao kwa masaa na kuwaingiza kwenye tamasha.

"Kuku tuliuza mpaka elfu 25. Mimi nilibeba kuku 150, wote waliisha usiku huo", anasema Shaibu Shabani

Kutokana na uwepo wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mkoani humo, Mei Mosi, tamasha hilo lilihudhuriwa na watu wengi zaidi wakiwemo viongozi mbalimbali na kuongeza chachu na mvuto wa tamasha.

Uhaba wa kuku wa kienyeji

Licha ya tamasha hilo, hali ya kuku wa kienyeji si ya kupendeza wakati wote. Wafugaji wanalalamikia kuchelewa kwa ukuaji, uhaba wa chakula na soko lisilotabirika. Kuku hawa wanahitaji miezi kadhaa kufikia ukubwa, tofauti na wale wa kisasa wanaoweza kuuzwa baada ya wiki chache tu.

Mwalimu Protas Lahi, ambaye alifuga kuku wa kienyeji kwa zaidi ya miaka 30, alifanya uamuzi mgumu:

"Nilihamia kwenye kuku wa kisasa. Mwanzo ilikuwa ngumu, lakini sasa napata faida ya uhakika."

Hii ni sauti ya mabadiliko. Hata urithi huhitaji marekebisho ili usikose mwelekeo wa siku zijazo.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya mkoa Singida, ufugaji unachangia asilimia 11 ya pato la Singida. Pamoja na kilimo cha alizeti, vitunguu, karanga na mahindi, kuku wa kienyeji wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mkoa huo.

Kuku wa Singida hawawiki bure. Wanawika kwa matumaini, historia, uchumi na urithi.