Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waliyoyasema viongozi duniani kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran
- Author, Tom McArthur
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Vikosi vya Marekani na Israel vimefanya mashambulizi katika miji mbalimbali nchini Iran, katika kile ambacho Rais wa Marekani Donald Trump ameelezea kama "operesheni kubwa za kivita."
Trump amewataka wananchi wa Iran kuamka na vikosi vya serikali kujisalimisha kufuatia kile ambacho Israel imeita "shambulizi la kujihami mapema."
Kwa kujibu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) lilisema katika taarifa kuwa linayalenga makambi na mali za Marekani kote Mashariki ya Kati kama sehemu ya operesheni iitwayo "Truthful Promise 4."
Hili linajiri baada ya wiki kadhaa za vitisho na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Hivi ndivyo jumuiya ya kimataifa inavyoitikia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amelaani kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi na kuonya kuwa amani na usalama wa kimataifa vinadhoofishwa.
"Matumizi ya nguvu ya kijeshi na Marekani pamoja na Israel dhidi ya Iran, na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran katika eneo lote, yanadhoofisha amani na usalama wa kimataifa," alisema katika taarifa.
"Natoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kupunguzwa kwa mvutano. Kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha mzozo mpana wa kikanda wenye madhara makubwa kwa raia na uthabiti wa eneo."
Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliitishwa Jumamosi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi, ambaye alikuwa akisimamia mazungumzo ya nyuklia ya wiki hii kati ya Marekani na Iran, alisema amesikitishwa sana.
"Mazungumzo ya dhati na muhimu yamevurugwa tena," aliandika kwenye mtandao wa X, akiieleza Marekani kuwa mashambulizi hayo hayakidhi maslahi yake wala amani ya dunia. "Naisihi Marekani isijikute ikiingia zaidi katika hali hii. Hivi si vita vyenu."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikosoa vikali mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel akiyaita "haramu, na yasiyo halali."
Katika chapisho kwenye X alisema kuwa Donald Trump amebadili kauli mbiu ya "America First" kuwa "Israel First, ambayo daima humaanisha America Last."
Taarifa ya pamoja ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, pia iliitaka Iran "kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo."
Taarifa hiyo, iliyochapishwa kwenye X na Ubalozi wa Ujerumani mjini London, ilisema kuwa nchi hizo zimekuwa zikiitaka mara kwa mara serikali ya Iran kusitisha mipango yake ya nyuklia na makombora, kujiepusha na "shughuli za kuvuruga utulivu," na kukomesha "ukatili na ukandamizaji mbaya dhidi ya wananchi wake."
"Hatukushiriki katika mashambulizi haya," viongozi hao watatu walisema, wakiongeza kuwa wako katika mawasiliano na washirika wa kimataifa, wakiwemo Marekani, Israel na wengine katika eneo hilo.
"Tunausihi uongozi wa Iran kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo. Hatimaye, wananchi wa Iran wanapaswa kuruhusiwa kuamua mustakabali wao," walisema.
Saudi Arabia pia ililaani mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Bahrain, United Arab Emirates, Qatar, Jordan na Kuwait huku ikilaani kwa "maneno makali zaidi uchokozi wa wazi wa Iran."
"Ufalme wa Saudi Arabia unathibitisha mshikamano wake kamili na msaada wake usiotetereka kwa nchi hizo ndugu, na uko tayari kutumia uwezo wake wote kusaidia hatua zozote watakazochukua," wizara ya mambo ya nje ilisema katika taarifa.
Urusi imelaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ikisema kuwa yalikuwa "hatua iliyochukuliwa bila kutazama athari zake."
Wizara yake ya mambo ya nje ilisema, "Mashambulizi haya yanafanywa tena kwa kisingizio cha mchakato mpya wa mazungumzo," ikirejea mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika wiki iliyopita.
Taarifa ya Kremlin pia ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutathmini kile ilichokiita "vitendo visivyo vya kuwajibika vinavyolenga kudhoofisha amani, uthabiti na usalama" katika eneo hilo.
Ingawa Uingereza ilisema haikushiriki katika mashambulizi ya Marekani na Israel, Waziri Mkuu Keir Starmer amesema ndege za Uingereza "ziko angani leo" katika Mashariki ya Kati kama sehemu ya "operesheni za pamoja za ulinzi wa kikanda kulinda watu wetu, maslahi yetu na washirika wetu."
Awali, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema "kuibuka" kwa mgogoro huo kuna "madhara makubwa kwa amani na usalama wa kimataifa," na akaonya kuwa kuendelea kwa ongezeko la mvutano ni "hatari kwa wote."
"Ufaransa pia iko tayari kutumia rasilimali zinazohitajika kuwalinda washirika wake wa karibu," aliongeza.
Taarifa ya Macron pia ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ujerumani ilisema iliarifiwa mapema kuhusu shambulizi hilo, na kwamba Kansela Friedrich Merz alishauriana na mawaziri husika wa usalama.
Kaja Kallas, mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya, (EU), ameyataja matukio ya hivi karibuni kuwa "hatari."
"EU imeweka vikwazo vikali dhidi ya Iran na kuunga mkono suluhisho za kidiplomasia, ikiwemo kuhusu suala la nyuklia," alisema katika taarifa kwenye X, akiongeza kuwa amezungumza na mawaziri wa mambo ya nje wa Israel na wengine katika eneo hilo.
"Ulinzi wa raia na sheria ya kimataifa ya kibinadamu ni kipaumbele."
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, ilisema itashauriana na washirika na viongozi wa eneo hilo ili kuunga mkono juhudi za kupunguza mvutano.
Katika taarifa, serikali ya Brazil ililaani mashambulizi ya Marekani na Israel na kueleza "wasiwasi mkubwa."
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, alisema nchi yake inaunga mkono Marekani "kuchukua hatua za kuzuia Iran kupata silaha ya nyuklia na kuizuia Iran kuendelea kutishia amani na usalama wa kimataifa."
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, alitoa wito wa kujizuia na kuhimiza pande zote "kutumia busara, kupunguza mvutano, na kurejea kwenye meza ya mazungumzo."
"Kama ilivyo kawaida, katika mzozo wowote wa kivita, raia ndio hulipa gharama kubwa zaidi," alisema, akiwakumbusha wahusika kuwa kulinda raia ni jambo la "muhimu sana" chini ya sheria ya kimataifa.
Mapema Jumamosi, Donald Trump alichapisha video ndefu kwenye tovuti yake ya Truth Social, akithibitisha ushiriki wa Marekani:
"Lengo letu ni kuwalinda wananchi wa Marekani kwa kuondoa vitisho vya haraka kutoka kwa utawala wa Iran," alisema, akiongeza kuwa dhamira ya Washington ni "kuhakikisha kuwa Iran haipati silaha ya nyuklia."
Pia aliwaambia wananchi wa Iran wabaki mafichoni na wasitoke majumbani mwao.
"Tutakapomaliza, chukueni serikali yenu," alisema. "Itakuwa yenu kuichukua. Hii huenda ikawa nafasi yenu pekee kwa vizazi vingi vijavyo."
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pia aliwataka wananchi wote wa Iran "kuondoa utawala wa kidhalimu na kuleta Iran huru na yenye amani."
Akimshukuru Trump, alisisitiza tena ujumbe wake kwamba Iran "haipaswi kuwa na silaha za nyuklia ambazo zingeiwezesha kutishia ubinadamu wote."
"Hatua yetu ya pamoja itaunda mazingira kwa wananchi jasiri wa Iran kuchukua hatima yao mikononi mwao," alisema.