Cristiano Ronaldo na Man Utd – Upi mustakabali wa mshambuliaji huyo?

Baada ya ushindi wa kusisimua wa 2-1 wa Manchester United katika dakika ya majeruhi dhidi ya Fulham Jumapili, Erik ten Hag alijiruhusu kutafakari juu ya maendeleo Old Trafford tangu awe meneja .

"Sasa tumeungana," alisema. "Tuna umoja, kwenye chumba cha kubadilishia nguo, na wafanyakazi, wakurugenzi, klabu nzima na mashabiki.

"Nadhani tuna msingi. Tunaenda katika mwelekeo sahihi. Nadhani utamaduni umebadilika; mtazamo, mawazo yamebadilika na hilo ni suala zuri . Leo, nadhani, ni ishara yake, unapopata kushinda katika sekunde za mwisho za mchezo."

Takriban wakati huo huo, wafanyikazi wa United walikuwa wakifahamishwa kwamba 'pamoja' haikujumuisha kila mtu.

Hawakujua wakati huo - na bado hawajui sasa - kiwango kamili cha shambulio walilopewa na Cristiano Ronaldo. Isipokuwa hali itabadilika, watalazimika kusubiri na watu wengine wote kutazama kwenye televisheni mahojiano ya Piers Morgan na mchezaji wanayemlipa £500,000 kwa wiki.

Katika sehemu ya mahojiano yaliyotolewa Jumapili, Ronaldo alisema anahisi "amesalitiwa" na klabu hiyo, hamheshimu meneja Ten Hag na analazimishwa kuondoka.

Katika kipande kipya cha siku ya Jumatatu, Ronaldo alidai wakurugenzi katika klabu hiyo hawakumwamini aliposema alilazimika kukosa kuanza kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya kwa sababu bintiye na mpenzi wake walikuwa hospitalini.

Mapema Jumatatu, klabu hiyo ilisema katika taarifa: "Manchester United inabainisha taarifa za vyombo vya habari kuhusu mahojiano na Cristiano Ronaldo. Klabu itazingatia majibu yake baada ya ukweli kamili kuthibitishwa."

Mahojiano ya Ronaldo yataonyeshwa kwenye Talk TV kwa muda wa usiku mbili Jumatano na Alhamisi.

Kwa namna fulani, hata hivyo, kwa Manchester United hakuna uamuzi wa kufanya.

Baada ya Ronaldo kukataa kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba wakati wa ushindi dhidi ya Tottenham mnamo Oktoba 19, United waliweka wazi kabisa nyuma ya pazia kwamba wanamuunga mkono Ten Hag kukabiliana na hali hiyo. Alimsimamisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 kwa mechi ya wikendi iliyofuata huko Chelsea.

Imebainika sasa Ronaldo anakubali mwenendo wake usiku huo haukuwa sahihi. Hata hivyo, anabakia kusisitiza uamuzi uliokusudiwa wa Ten Hag ulikuwa ni onyesho la kutomheshimu hadharani.

Katika mahojiano ya redio na Talksport siku ya Jumatatu, Morgan alisema hatua hiyo inakinzana na maelezo ya Ten Hag kwa kushindwa kwake kumleta Ronaldo wakati wa kichapo cha 6-3 katika mechi ya Manchester derby Uwanja wa Etihad wiki mbili na nusu mapema, ambayo alisema, yalikuwa chini ya mazingira, yasio na heshima.

Kulikuwa na tofauti kubwa katika michezo miwili. United walikuwa chini kwa mabao 4-0 katika kipindi cha kwanza. Baada ya dakika 80, matokeo yalikuwa 6-1. Kwa wazi hakukuwa na chochote hatarini zaidi ya kupunguza ukubwa wa kushindwa kwa kufedhehesha.

Dhidi ya Tottenham, waliingia katika dakika 10 za mwisho wakilinda uongozi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya wapinzani wao walio katika nafasi nne za juu baada ya kukimbia kwa kuvuna pointi nne katika michezo mitatu. Christian Eriksen alitambulishwa zikiwa zimesalia dakika tatu usiku huo kuisha, pamoja na kijana Anthony Elanga.

Nahodha wa zamani wa United Gary Neville hakuwa peke yake katika kufikiri kwamba Ronaldo alikuwa amevuka mstari usiku huo na ingekuwa bora kwa pande zote ikiwa mchezaji mwenzake wa zamani angeruhusiwa kuondoka mara moja.

Ten Hag alichukua mtazamo tofauti.

Hata hivyo, katika kueleza msimamo wake katika mkutano uliorefushwa na waandishi wa habari siku mbili baada ya mchezo wa Tottenham, alisema jambo ambalo linaingia kwenye kiini cha suala hilo.

“Lazima nichukue maamuzi kwa maslahi ya klabu na timu hasa, hiyo ndiyo kazi yangu,” alisema. "Haijalishi ni nani, umri au sifa."

Kwa maneno mengine, haijalishi kwamba Ronaldo ameshinda kila heshima kwenye mchezo mara nyingi, ametawazwa mshindi wa Ballon d'Or mara tano na anatambulika kwa wingi kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea.

Kwa macho ya Ten Hag, yeye ni mchezaji mwingine tu. Na ukweli wa kikatili ni kwamba, msimu huu, hajatoa, iwe kwa suala la mabao ya kufunga au mchango wa jumla.

Siku ya Jumatatu, Ronaldo alituma ujumbe kwenye Twitter kwamba alikuwa anaangazia kikamilifu Kombe la Dunia akiwa na Ureno.

Zaidi ya kusema wanahitaji kubaini ukweli kamili wa mahojiano hayo, ambayo Ronaldo hakuwa na ruhusa nayo, United wanaweka kila kitu siri.

Kwa faragha hawajafurahishwa na baadhi ya madai mahususi ambayo Ronaldo anayatoa kuhusu maisha nyuma ya pazia katika klabu hiyo, wakisema kuwa mgahawa na menyu zimefanyiwa marekebisho, maboresho yanafanywa kwenye gym na kwamba uwanja wa mazoezi ni tofauti na mmoja ambao Mrenohuyo aliuacha mwaka wa 2009.

Pia kuna hali ya kutofurahishwa na madai ya Ronaldo kwamba analazimishwa kutoka na 'watendaji' ikizingatiwa kwamba alipewa likizo ya huruma na kuruhusiwa kukosa ziara ya majira ya joto ya Thailand na Australia na viongozi waandamizi katika klabu hiyo, hata wakati hatua hiyo ilipokuwa ikihojiwa na wengine.

Kumekuwa na uvumi kwa muda sasa kwamba Ronaldo - anayeonekana sana kama mtaalamu wa uber - amekuwa sio mwongozo mwema kwa wachezaji wachanga kama ilivyotarajiwa.

Pia hakuna shaka kwamba Ronaldo alitaka kuondoka katika majira ya joto. Vyanzo vya United vinasisitiza kwamba, zaidi ya ofa kutoka Saudi Arabia, hakuna mpango wowote uliowekwa ambao haukuwahusisha kulipa sehemu kubwa ya mshahara wake.

Kutokana na hali hii, United lazima iamue nini cha kufanya baadaye.

Haiwezekani kufikiria tena Ronaldo akicheza chini ya Ten Hag na haiwezekani kuwa uongozi wa United unaweza kumdhoofisha meneja wao kwa kumuunga mkono mchezaji huyo.

Ten Hag atahitaji kuzungumza na mkurugenzi wa soka John Murtough, kabla ya mtendaji mkuu Richard Arnold na mwenyekiti mwenza Joel Glazer kuhusika.

Ikiwa yaliotokea awali ni mwongozo , subra na uvumilivu utahitajika kwa matokeo ya baadaye.

Ndivyo ilivyokuwa miaka 17 iliyopita. Upepo ulirudi Oktoba 2005, wakati United ilipofungwa 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza huko Middlesbrough. Mara tu baada ya mechi hiyo, nahodha Roy Keane alifanya mahojiano ya MUTV akiwalaani sana wachezaji wenzake hivi kwamba hayakuonyeshwa kamwe.

Siku kumi na nane baadaye baada ya kufanya mahojiano hayo, Keane aliondoka United kwa "makubaliano ya pande zote". Katika umri wa mitandao ya kijamii, siku 18 huhisi kama maisha.

Lakini, haijalishi inachukua muda gani, inaonekana Ronaldo hatimaye atapata matakwa yake na kuruhusiwa kuondoka. Jinsi yote hayo yatakavyoamulia ndio muhimu

'Siwezi kumtetea Ronaldo ‘

Nahodha wa zamani wa Manchester United Rio Ferdinand alisema hawezi kumtetea Ronaldo.

"Haya yote yameandaliwa kwa kitu kimoja - na hiyo ni kwa ajili yake kuondoka kwenye klabu," alisema kwenye Vibe yake ya podcast.

"Hadi kufikia mahojiano haya, ningemtetea lakini mapenzi haya na Manchester United ambayo Cristiano amekuwa nayo yameisha machoni mwangu.

"Sihisi kama kuna njia yoyote ya kurudi. Sihisi klabu itamrudisha na sidhani kama anataka kurejea. Hii yote imeandaliwa kwa sababu hiyo."

Akiongea kwenye BBC Radio 5 Live usiku wa |Jumatatu, mshambuliaji wa zamani wa Blackburn na Chelsea Chris Sutton alisema Ronaldo "ameshuka kwa viwango na ametoboa yake yote

Sutton alisema: "Ronaldo hawezi kumchezea Ten Hag tena. Hawezi kuichezea Manchester United tena. Inaweza kuwa hatua nzuri sana kwa Ten Hag. Mahojiano haya yote hayakuwa ya lazima kabisa, yameharibu sifa zake.

"Washauri wake lazima walijua athari ambayo mahojiano haya yangekuwa nayo."

Mshambulizi wa zamani wa Brighton Glenn Murray aliongeza: "Manchester United walijua walipomleta alikuwa na shauku kubwa ya kuendana na ubora wake. Hili lingetokea kila mara. Hangeweza kuondoka bila vita.

"Ni wazi kila mtu anamtaka aondoke katika klabu hiyo. Hicho ndicho alichokitaka kwenye mahojiano. yalikuwa ya kujifurahisha tu. Hakuna njia ya kurudi kwake sasa."Andy Mitten, editor wa jarida la United We Stand magazine, awali aliiambia BBC Radio 5 Live: "Hajalazimishwa kuondoka. Alitaka kuondoka wakati wa kiangazi na alidhani anaondoka, lakini kulikuwa na uhaba wa timu zilizomuhitaji.

"Amefanya mahojiano ambayo ni toleo lake la ukweli na mara nyingi kuna zaidi ya toleo moja la ukweli maishani.

"Sidhani kama mashabiki wa United wangekuwa na wasiwasi mkubwa kama hangeichezea klabu tena."