Panda shuka za Kinana ndani ya CCM

k

Chanzo cha picha, CCM Tanzania

Maelezo ya picha, Abdulrahman Kinana
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Abdulrahman Kinana ni mwanasiasa mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania. Amezitumikia nyadhifa mbalimbali, zile za serikali na za chama chake, hadi kuwa mwanasiasa maarufu na mwenye ushawishi.

Siku ya Jumatatu, ilibainika kuwa Kinana amejiuzulu wadhifa wake kama Makamu Mwenyekiti wa CCM. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, inaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan ameridhia Kinana kung’atuka.

Sehemu ya barua hiyo inasema, “ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako.”

Ameihudumia nafasi hiyo kwa takribani miaka miwili na miezi mitatu, tangu kuchaguliwa kwake mwezi Aprili 2022. Ni baada ya kuwa na nyakati mbaya ndani ya CCM, katika kipindi cha utawala wa hayati Rais John Pombe Magufuli.

Pia unaweza kusoma

Kinana na wakati wa mivutano

d

Chanzo cha picha, CCMtanzania

Maelezo ya picha, Hayati John Pombe Magufuli na Abdulrahman Kinana

Mei 30, 2018 mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo hayati Magufuli, alisema Kinana aliomba mara nyingi ajiuzulu tangu 2016, hadi alipokubali ombi hilo Mei 2018.

Mvutano kati ya Kinana na utawala wa Magufuli ulionekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya Kinana na Katibu Mkuu wa chama hicho mwaka 2006 hadi 2011, Yusuf Makamba kuandika waraka ulioanza kusambaa Julai 14, 2019, wakilalamika kuchafuliwa na mmiliki wa magazeti yaliyokuwa yakitetea utawala wa Magufuli, ndugu Cryprian Musiba.

Aya moja ya waraka huo inasema, "tumetafakari kwa kina kabla ya kuamua kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na uzushi alioutoa Cyprian Musiba dhidi yetu katika nyakati mbili tofauti."

Katika kile kilichoonekana kukuwa kwa mvutano ndani ya chama, siku nne baada ya waraka huo, sauti za mazungumzo ya simu ya wanasiasa hao zilivuja, wakimpiga vijembe Rais Magufuli. Sauti za wana CCM wengine zilizovuja ni January Makamba, Nape Nnauye na Bernard Membe.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Februari 2020, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, ilimpa onyo Abdulrahman Kinana na adhabu ya kumfukuza uanachama hayati Bernard Membe na kumsamehe Yusuf Makamba kutokana na madai ya kukiuka maadili ya chama hicho.

Halmashauri Kuu pia iliwasamehe na kuwaonya January, Nape na William Ngeleja, ambao kwa nyakati tofauti inaelezwa walimuomba radhi Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo, Rais John Pombe Magufuli.

Kuna swalia limeibuka: Je, kujiuzulu Kinana kuna uhusiano wowote na kufutwa kazi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wiki moja iliyopita?

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Thomas Kibwana anasema, “naamini kabisa upo uhusiano. Kwa sababu kwenye siasa huwa hakuna sadfa, na sasa ni mara ya pili Kinana anajiuzulu kutoka nafasi ya juu ya CCM mara baada ya wawili hawa kuondolewa katika nafasi zao za uwaziri.

“Naamini kuna safisha safisha inaendelea ndani ya serikali na chama na Kinana ni mmoja wa watu ambao wamekubwa na fagio hili japo yeye kaondolewa kiheshima zaidi na kuruhusiwa kujiuzulu.”

Anaendelea kwa kusema, “January na Nape walikua sehemu muhimu ya timu ya kampeni ya 2015 iliokua chini ya Kinana. Yawezekana kuwa mtazamo wa mamlaka, ukaribu wa Kinana na vijana wake January na Nape unamfanya na yeye ahusishwe na chochote kile kilicho sababisha wawili hao waondolewe kwenye uwaziri.”

Urithi wake ndani ya CCM

cx

Chanzo cha picha, HabariLeo

Kinana mwenye umri wa miaka 73, ni mwanajeshi aliyepanda cheo hadi Kanali. Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mnamo mwaka 1972 na kulitumikia hadi mwaka 1992 alipostaafu.

Ni msomi wa shahada ya kwanza katika Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Ljubljana iliyokuwa Yugoslavia na Shahada ya Uzamili katika Uongozi na Utawala aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.

Amehudumu kama Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka 2001 hadi 2006. Na Katibu Mkuu wa CCM kutoka 2012 hadi 2018. Vilevile amekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Ulinzi na Naibu Waziri wa Ulinzi. Pia alikuwa Mbunge wa Arusha kwa tiketi ya CCM kwa mwongo mmoja.

Akiwa Katibu Mkuu wa chama, alizunguka mikoa ya Tanzania kwa sehemu kubwa ya uongozi wake akiitangaza CCM katika miji na vijiji. Na hii ni moja ya urithi wake mkubwa kwa chama hicho.

Ameongoza kampeni nne za urais kwa mafanikio; mwaka 1995 na 2000 akiwa Meneja wa Kampeni wa mgombea wa CCM hayati Benjamin Mkapa, pia meneja wa kampeni wa Jakaya Kikwete mwaka 2010 kabla ya kusimamia kampeni za hayati Magufuli 2015 akiwa Katibu Mkuu.

Baada ya mvutano wa wakati wa Magufuli, Kinana alirudishwa katika shughuli za kila siku za CCM na Rais Samia, na ilionekana kwamba angedumu katika wadhifa huo kumsaidia Rais Samia katika uchaguzi mkuu wa 2025, hasa kutokana na uzoefu wake na chaguzi kuu.

Lakini kwanini kujizulu kwake kumekubaliwa muda huu, wakati 2025 ni uchaguzi mkuu? Thomas Kibwana, anasema: “Tunacho ona sasa ni kwamba Rais Samia hatimaye anajenga timu yake mwenyewe, kitu ambacho kila rais huko nyuma amekua akikifanya mara baada ya kuapishwa kuwa rais.”

Kutokana na mazingira yaliomuingiza Rais Samia madarakani, amechelewa kufanya hivi na kwa muda mrefu kabaki na timu ya kurithi kutoka kwa watangulizi wake, ila sasa inaelekea ndio anajenga watu wake ambao anaamini watamsaidia kwenye kazi ikiwa ni pamoja na kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.”

Pia unaweza kusoma

Imehaririwa na Munira Hussein