Mapuuza ya baba kulisababisha kifo cha msichana mwenye unene kupita kiasi - mahakama

Chanzo cha picha, ATHENA PICTURES
Msichana wa miaka 16 ambaye alifariki dunia baada ya kuwa mnene kupita kiasi wakati wa nchi zilikuwa zinatekeleza masharti ya kutotoka nje kimataifa alitelekezwa sana na wazazi wake, mahakama imearifiwa.
Mwili wa Kaylea Louise Titford ulipatikana kwenye matandiko machafu kweli na polisi wakabaini harufu yenye uvundo "isiyovumilika".
Baba yake Alun Titford, kutoka Newtown, Powys, amekanusha kusababisha mauaji kwa uzembe katika mahakama ya Mold Crown.
Mamake Kaylea Sarah Lloyd Jones hapo awali alikiri shtaka kama hilo.
Caroline Rees KC aliiambia mahakama kwamba Kaylea alikuwa na matatizo ya uti wa mgongo ambao ulimfanya kuwa na hisia kidogo kutoka kiunoni kwenda chini, na kumzuia kutembea, hivyo basi, alikuwa ametumia kiti cha magurudumu tangu umri mdogo.
Alipokutwa amefariki nyumbani kwake alikuwa amenenepa kupita kiasi, akiwa na uzito wa (kilo 146), mahakama iliarifiwa.
Bi Rees alisema: "Kaylea Titford alikuwa akiishi katika mazingira yasiyofaa hata kwa mnyama yeyote, licha ya kuwa msichana wa miaka 16 aliye hatarini ambaye alitegemea kabisa wengine kwa utunzaji wake."
Nywele za Kaylea zilikuwa chafu na zilizochanika na alikuwa hajaoshwa akiwa na ngozi yenye vidonda, mahakama iliarifiwa.

Asubuhi ya Oktoba 10 2020, mahakama iliarifiwa kuwa simu kupitia nambari 999 ilipigwa na mama wa Bw Titford kabla ya wahudumu wa afya kutumwa nyumbani kwake na mwili wa Kaylea kupatikana.
Pamoja na kulala kwenye matandiko machafu, alikuwa na vidonda vingi na maeneo yaliyopata maambukizi.

Chanzo cha picha, ANDREW PRICE/PA WIRE
Bi Rees aliongeza: "Upande wa mashtaka unasema kwamba eneo la tukio - kama lilivyoshuhudiwa na wale waliohudhuria - pamoja na hali ambayo mwili wa Kaylea ulipatikana unaonyesha wazi kwamba msichana huyo aliye katika mazingira magumu, ambaye alitegemea sana wengine kwa mahitaji yake ya ustawi, alitelekezwa sana si mmoja tu bali wazazi wake wote wawili, ambao walikuwa na jukumu la kumtunza."
Ripoti ya mwanapatholojia ilisema hali yake ya mwili ilionyesha kwamba hakuwa ameoshwa vizuri kwa wiki nyingi, mahakama iliarifiwa.
Mwendesha mashtaka alisema Kaylea alikufa kwa sababu wazazi wake walishindwa kutekeleza jukumu lao la malezi na hiyo ilizua hatari kubwa ya kifo.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bi Rees alisema: "Kushindwa kwao kutekeleza majukumu yao kulijificha kutokana na hatua za kutotoka nje kuanzia Machi 2020 kwa sababu ya janga la kimataifa la Covid.
"Tunaendelea kusema kwamba uzembe wa wazazi ulikuwa mbaya sana hadi kutambuliwa kama uhalifu."
Wakati Bw Titford alipohojiwa na polisi, aliwaambia "hakuwa baba mzuri sana" na mkewe alimtunza Kaylea na kufanya kazi za nyumbani, mahakama iliarifiwa.
Alisema binti yake alikuwa amekua mkubwa sana na hakustahili kiti cha magurudumu alichokuwa nacho na hadhani kama aliwahi kumwona kutoka kitandani tangu kuanza kutekelezwa kwa hatua za kukabiliana na ugonjwa wa Covid.
Aliwaambia polisi kwamba familia ilikuwa ikinunua chakula kutoka nje mara tano kwa wiki.
Alipoulizwa mara ya mwisho alipomuuliza Kaylea hali yake, alisema: "Sikumuuliza. Kama ninavyosema, mimi si mtu mzuri sana. Hakuna mtu anayefikiria kwamba mtoto wake ataishia hivyo."
Upande wa mashtaka ulisema kesi ya Bw Titford ni kwamba ingawa aliishi katika nyumba moja, mamake Kaylea alikuwa mlezi mkuu na kwamba hakuwa na habari kuhusu hali ya maisha ya bintiye au kuzorota kwa hali yake ya kimwili.
Kesi inaendelea.














