Wakenya wahadaiwa kuwa walaghai wa 'mapenzi' bila kujua

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika msururu wa barua zetu kutoka kwa wanahabari wa Kiafrika, Waihiga Mwaura kutoka runinga ya Citizen ya Kenya anaangazia jinsi Wakenya wanavyotapeliwa na mashirika ya magendo yanayojifanya kuwa mawakala wa kuajiri.

Ikiwa kitu kinaonekana kuwa kizuri sana fikiria mbara mbili.

Huo ndio ujumbe kutoka kwa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Kenya ilipowaonya wanaotafuta kazi ambao walivutiwa na ahadi ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi kusini-mashariki mwa Asia.

Inafuatia kuokolewa kwa zaidi ya Wakenya 60 kutoka Myanmar na Laos katika kipindi cha miezi michache iliyopita - baada ya kutuma maombi kwa kazi za mauzo na huduma kwa wateja nchini Thailand kugeuka kuwa kificho kwa uhalifu wa mtandaoni, ukahaba na hata wizi wa viungo. "

"Tayari kijana mmoja Mkenya amefariki kutokana na upasuaji duni wa madaktari matapeli wanaofanya kazi katika viwanda vinavyomilikiwa na Wachina nchini Myanmar," wizara hiyo ilisema wiki jana.

Nilizungumza na wanawake wawili kuhusu uzoefu wao wa hivi majuzi.

Akiwa ameomba jina lake lisitajwe, kijana mwenye umri wa miaka 31, ambaye ana diploma ya usimamizi wa hoteli, na mhitimu wa shule ya upili mwenye umri wa miaka 35 aliniambia jinsi walivyoondoka kwenda kazini nchini Thailand mnamo Agosti kwa ahadi ya mshahara wa kila mwezi wa $800 ( Pauni 675).

Mwezi mmoja kabla ya kuondoka kila mmoja wao alikuwa amekopa karibu dola 2,000 ili kuwalipa mawakala wao kwa ajili ya safari hiyo na wakapitia kipindi kifupi cha mafunzo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo walipofika Thailand wahudumu wao waliwachukua kwa safari ndefu kwa njia ya barabara, hatimaye wakavuka mto hadi Laos iliyo jirani.

Waliishia kwenye jengo la orofa 15, ambalo lilikuja kuwa makazi yao ya wakati wote - ingawa hawakujua walikuwa katika mji gani au jiji gani.

Hapa ndipo walipojifunza kuwa badala ya majukumu ya huduma kwa wateja, walikuwepo kushiriki katika shughuli za uhalifu mtandaoni - yaani kuwalenga Wamarekani kwa kuunda wasifu unaovutia kwenye Tinder, Instagram na Facebook.

"Wanakupenda na unaweza kuwaambia kuhusu pesa za kidijitali za crypto-currency. Unaanza kuwaibia" mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 31 alisema, akielezea kwa Kiswahili jinsi wote wawili walilazimishwa kufanya kazi katika kituo kikubwa cha simu kama ukumbi na mamia ya watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Hakuna hata mmoja wao aliyepokea mshahara alioahidiwa na badala yake walitishwa na kazi ya ngono au kuchukuliwa viungo vyao vya mwili ikiwa wangekosa kuwavutia waathiriwa wa kutosha mtandaoni.

"Kama mwanamke unaweza kulazimishwa kufanya biashara ya ngono. Ikiwa hiyo haitafanya kazi wanaweza kuchukua viungo vyako vya mwili na kuviuza ili kurejesha gharama zao," alielezea, mwenzake akikubali alipokuwa akizungumza.

"Walituambia: Lazima ulipe shilingi za Kenya 1.2m ($10,000) kununua uhuru wako kwa sababu tunakumiliki."

'Ulaghai wa kiviwanda'

Kwa bahati wawili hao walifanikiwa kuwasiliana mtandaoni na shirika la Uhamasishaji Dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (Haart), shirika la msaada la Kenya ambalo huwasaidia wahamiaji walio katika matatizo, na hatimaye waliokolewa na kurudishwa nyumbani kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za Kenya.

Hadithi yao inalingana na ya Wakenya wengine wanaoshikiliwa katika kile wizara ya mambo ya nje imekiita "ulaghai wa kiviwanda" na "kambi za kazi za kulazimishwa" ambapo "pasipoti zao za kusafiria huchukuliwa na kusalia chini ya genge la wahalifu".

Ilisema ingawa wengi wa maajenti wa kuajiri walikuwa wakisakwa na polisi, bado walikuwa wakitangaza kazi ambazo hazipo nchini Thailand na Wakenya waliendelea kunaswa na matapeli hao.

Baadhi ya waliookolewa walikuwa wamerejea nyumbani kwa magongo wakiwa wamevunjika miguu na mikono "baada ya kupigwa vikali na hadi watu 20 wa genge hilo wanaofanya kazi katika viwanda hivyo".

Kwa mujibu wa taarifa ya hivi punde ya wizara ya mambo ya nje, baadhi ya Wakenya nchini Myanmar wanaonekana kuwa katika jimbo la Kachin, ambako waasi wanaojitenga wanapambana na jeshi - jambo ambalo lilikuwa likikwamisha juhudi za uokoaji.

"Operesheni za hivi majuzi za jeshi ziliua zaidi ya watu 60 katika eneo linalodhibitiwa na makundi ya waasi, ambao hutoa ulinzi kwa makundi ya Kichina," wizara ilionya.

Kwa jumla waathiriwa 76, wakiwemo Waganda 10 na Mrundi mmoja, wamerudishwa makwao tangu mwezi Agosti kwa usaidizi wa maafisa wa ubalozi wa Kenya nchini Thailand.

Ni vijana na wasomi wa Kiafrika ambao walikuwa wakilengwa na mashirika hayo kwani wanachukuliwa kuwa bora zaidi kuweza kufanya kazi ya uhalifu wa mtandaoni.

Hii inaashiria ukosefu mbaya wa nafasi za ajira katika bara hili na jinsi serikali zinazofuata zinavyoahidi ajira kwa watu wao lakini zinashindwa kutimiza.

Benki ya Maendeleo ya Afŕika inakadiria kuwa wakati zaidi ya vijana milioni 12 wanaingia katika nguvu kazi baŕani Afŕika kila mwaka, ni ajiŕa rasmi milioni tatu pekee zinazotolewa kila mwaka.

Kulingana na utafiti wa Wakfu wa Mo Ibrahim, asilimia 80 ya Waafrika wanaoondoka barani humo - hasa wale wanaoelekea Ulaya - hufanya hivyo kutafuta kazi.

Wale ambao wamebahatika kupata kazi wanaweza kutuma pesa nyumbani kusaidia wanafamilia.

Hata hivyo, mara nyingi sana wanaishia katika hali ngumu.

Kufichuliwa kwa ulaghai wa kazi katika eneo la kusini-mashariki mwa Asia kufuatia ripoti zinazoendelea za unyanyasaji wa wahamiaji wa Kiafrika katika Mashariki ya Kati.

Wasichana wawili niliozungumza nao sasa wamesalia na madeni makubwa - na wako katika hali mbaya zaidi kuliko walivyokuwa miezi mitano iliyopita.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 35 amepata kazi katika saluni ya nywele, lakini mwenzi wake bado hajapata kazi nyingine.