Barua kutoka Afrika: Afrika haihitaji tena ushauri wa Marekani

Joe Biden speaking in Kenya

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wakati huo makamu rais Joe Biden wa Marekani akizungumza na raia wa Kenya mwaka 2010 na kuwaeleza kwamba hakuwa amekuja kuwasomea.

Katika mfululizo wetu wa makala zinazoandaliwa na waandishi habari wa Afrika, Waihiga Mwaura anaangazia kile ambacho pengine huenda Afrika ikawa inakitarajia kutoka kwa Rais wa Marekani Joe Biden.

Short presentational grey line

Zulia jekundu lilitandazwa, uwanja ukajaa, usalama ukaimarishwa na Joe Biden akaapishwa tayari kuchukua usukani.

Hii ilikuwa kama ilivyotokea mjini Nairobi mwaka 2010 Wakenya wapojitokeza kumsikiliza wakati huo aliyekuwa makamu rais wa Marekani.

"Ni matumaini yangu kwamba ninavyozungumza haijitokezi kama ambaye nimekuja kuwasomea," Biden alisema.

"La sifanyi hivyo," alisisitiza. "Lakini raslimali zenu nyingi zimepotea kwa ufisadi na hakuna hata afisa mmoja wa ngazi ya juu aliyekamatwa kwa uhalifu huo."

US President Donald Trump and Nigeria"s President Muhammadu Buhari take part in a joint press conference in the Rose Garden of the White House on April 30, 2018 in Washington, DC.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais Trump, akionekana na rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, kulibadilisha mtanzamo wa Marekani kwa nchi za nje

Mwanahabari Wahiga Mwaura alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanasilikiliza hotuba yake wakati huo, Marekani ilikuwa kweli kielelezo cha demokrasia na utawala wa sheria, nchi yenye uhuru, ujasiri na chimbuko la ndoto za kutia matumaini.

Miaka kumi baadaye, mengi yamebadilika.

Je Biden anaweza kuhuruhisiwa kutoa ushauri hata kama ana maono mazuri kiasi gani, iwapo pengine ataamua kutembelea Kenya?

Rais Donald Trump kupitia sera yake ya 'Marekani Kwanza', aliweka wazi picha tofauti ya Marekani nje ya nchi hiyo. Lakini pia muonekano huo uliingia doa kupitia matendo na maneno yake kama vile kupuuza nchi za Afrika kwa kutumia maneno ambayo yalionesha dharau.

Na ingawa ofisi ya rais inaweza kutenganishwa na matendo ya mtu binafsi, Rais Joe Biden atahitajika kuwasiliana na Kenya na nchi zingine Afrika kwa kutumia lugha tofauti kabisa katika kipindi cha miaka minne ijayo.

'Marekani sio tena mji unaong'aa'

Mifano ambayo Trump alibadilisha utaratibu uliokuwepo na maono ya Marekani ni mengi mno.

Lakini mbali na kushindwa kutoa hadharani ripoti yake inayoonesha malipo ya kodi ya mapato, kushusha hadhi ya mashirika ya kijasusi na kuchanganya wanasayansi wakati ambapo dunia inakabiliana na janga la virusi vya corona, tukio la Januari 6, rais alipochochea wafuasi wake kuvamia jengo la Bunge Marekani, Capitol ilionesha kwamba kweli amevuka mpaka.

President Biden signs documents with Vice President Kamala Harris by his side

Chanzo cha picha, Jim Lo Scalzo / Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Joe Biden alianza kazi punde tu baada ya kuapishwa rasmi kama rais wa Marekani

Marekani haukuwa tena mji unaong'aa.

Watu watano walifariki dunia huku waandamanaji wakijaribu kusitisha vikao vya pamoja vya Bunge kuidhinisha ushindi wa Biden, na kusababisha madai ya kuwa rais aliyeondoka madarakani alikuwa anatekeleza jaribio la mapinduzi.

Dunia ilitazama kwa hofu kwasababu kile walichoshuhudia - niseme pengine - kilikuwa kimezoeleka kuonekana katika nchi ambazo bado demokrasia yao iko chini lakini wakati huu walikishuhudia mbele ya macho yao.

Wahariri wa magazeti nchini Kenya hawakuwa peke yao wakielezea tukio hilo kama "vurugu" na "aibu" - na kumuita Bwana Trump "aliyejifedhehesha".

Maelezo ya video, Uchaguzi wa Marekani 2020: Tazama jinsi waandamanaji walivyovamia bunge Marekani

Na maneno kama "taifa lililo feli" na "demokrasia iliyo hatarini" yakaelekezwa kwa Marekani.

Bwana Biden anaingia Ikulu akifahamu fika kuwa dunia haina tena heshima kwa Marekani vile ilivyokuwa nayo.

Na hilo huenda likawa na athari zake katika uongozi kote barani.

Marais hawaichukulii tena Marekani kwa heshima na taadhima kuu na itakuwa rahisi kwao kutupilia mbali wasiwasi wowote utakaoibuliwa na nchi hiyo juu ya demokrasia.

Katika mahojiano na kituo cha Channel 4 nchini Uganda, Bwana Museveni alisema kukakamatwa kwa waandamanaji nchini humo kulilenga kuzuia matukio sawa na yaliyotokea Marekani

1px transparent line

"Rais Biden anaweza kujua mtu anavyohisi kuishi katika nchi ambayo viongozi fulani wanaweza tu kuharibu utamaduni na desturi ambayo imekuwepo", amesema Waihiga Mwaura.

Upande wa jeshi, kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikielezewa kama mlinzi wa dunia nzima na linapokuja suala la kanuni za demokrasia pia imekuwa ikichukuliwa kama nchini iliyobobea katika hilo.

Lakini je sasa hivi, mavuguvugu ya upinzani na makundi ya mashirika ya kiraia yanaweza kutegemea Marekani iwaunge mkono utakapowadia wakati wa uchaguzi?

Mgombea urais wa upinzani katika uchaguzi wa Uganda Bobi Wine alitoa wito kwa Marekani kuwajibisha serikali kwa yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi lakini wengine wanajiuliza kama kweli hilo lingetekelezeka.

Usalama uliimarishwa sana na mabadilishano ya madaraka kukashuhudiwa kwa njia ya amani nchini Marekani, na bunge kurejelea shuhuli zake lakini limesisitiza umuhimu wa kuwa na taasisi zenye uwezo madhubuti zaidi ya nguvu aliyonayo mtu mmoja.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba, sasa hivi Joe Biden atahitajika kuwa makini sana linapokuja suala la uhusiano kati ya Afrika na Marekani na pia atalazimika kupima ni ushauri gani anaotoa.

Presentational grey line