Teknolojia ya filamu za Avatar inavyotumiwa katika utafiti wa magonjwa

Chanzo cha picha, 20TH CENTURY STUDIOS
Suti za kunasa mwendo zinazowavutia wahusika katika filamu kama vile Avatar zinasaidia watafiti kufuatilia chanzo cha magonjwa ambayo yanayoathiri mwendo.
Mara nyingi, jinsi hali kama hizo zinavyotathminiwa haraka, ndivyo mgonjwa anavyoweza kupata usaidizi na matibabu yanayofaa.
Mfumo mpya hutumia akili ya bandia kuchanganua mienendo ya mwili. Katika vipimo, wataalamu wa Uingereza walipima ukali wa matatizo mawili ya kijenetiki kwa haraka mara mbili kuliko madaktari bora.
Watafiti wanasema inaweza pia kupunguza muda kwa nusu na kupunguza sana gharama inayohitajika kutengeneza dawa mpya katika majaribio ya kimatibabu.
Utafiti huo umechapishwa katika jarida la Nature Medicine. Dkt Valeria Ricotti, wa Taasisi ya Great Ormond Street ya Afya ya Mtoto aliiambia BBC News kwamba "amefurahishwa kabisa na matokeo.
"Athari katika utambuzi na kutengeneza dawa mpya kwa anuwai ya magonjwa inaweza kuwa kubwa kabisa." Dk Ricotti alikuwa miongoni mwa kundi la watafiti katika Chuo cha Imperial na Chuo Kikuu cha London ambao walitumia miaka 10 kuendeleza teknolojia mpya.
Waliijaribu kwa wagonjwa walio na matatizo ya mfumo wa neva na matatizo ya mwendo,Friedreich's ataxia(FA) na hali ambayo husababisha udhaifu wa mifupa na misuli ya moyo, Duchenne Muscular Dystrophy (DMD) katika tafiti mbili tofauti.
Watafiti wanasema inaweza pia kutumika kufuatilia wagonjwa wanaopata nafuu kutoka kwa magonjwa mengine ambayo huathiri mwendo. Hizi ni pamoja na hali yoyote inayohusisha ubongo na mfumo wa neva, moyo, mapafu, misuli, mfupa na magonjwa kadhaa ya akili.

Chanzo cha picha, GREAT ORMAND STREET HOSPITAL
Kufuatilia ukali na uwezekano wa kuendelea kwa magonjwa kama haya kwa kawaida huhusisha kupima katika kliniki kasi na usahihi ambayo wagonjwa hufanya mwendo sanifu.
Tathmini hiyo muhimu katika kufahamu ni usaidizi na matibabu gani mgonjwa anahitaji inaweza kuchukua miaka.
Tafiti mbili zilizochapishwa Alhamisi zinaonesha kuwa mfumo wa kunasa mwendo unaweza kufanya hivi haraka na kwa usahihi zaidi.
Ilichukuliwa kutoka kwa teknolojia inayotumiwa na watengenezaji filamu kunasa mienendo ya waigizaji katika filamu za Avatar ili kuunda kinachofanana na maisha kwenye skrini.
Prof Aldo Faisal wa Chuo cha Imperial, ambaye alikuwa mmoja wa wanasayansi waliotoa wazo hilo, alisema ni uboreshaji mkubwa. "Mtazamo wetu mpya hugundua mienendo ambayo wanadamu hawawezi kuifanya," alisema. "Ina uwezo wa kubadilisha majaribio ya kliniki na pia kuboresha utambuzi na ufuatiliaji wa wagonjwa."

Chanzo cha picha, THMOAS ANGUS/IMPERIAL COLLEGE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
FA kwa kawaida huonekana katika hatua za awali na huathiri mtu mmoja kati ya 50,000, ambapo DMD huathiri watoto 20,000, wengi wao wakiwa wavulana, duniani kote kila mwaka.
Kwa sasa hakuna tiba ya hali hizo zote. Timu katika Chuo cha Imperial ilijaribu kwanza suti za sensor ya mwendo kwa wagonjwa walio na FA. Waligundua kuwa akili bandia inaweza kutabiri kuongezeka kwa ugonjwa huo kwa muda wa miezi kumi na mbili, nusu ya muda ambao kawaida ungechukua mtaalamu.
Timu tofauti katika Great Ormond Street ilijaribu teknolojia kwa wavulana 21 walio na DMD kati ya umri wa miaka mitano na 18. Ilitabiri jinsi mwendo wao ungeathiriwa miezi sita katika siku zijazo kwa usahihi zaidi kuliko daktari.
Watafiti wanaamini kuwa mfumo wao unaweza kutumika kuharakisha na kupunguza gharama ya majaribio ya kliniki ili kujaribu dawa mpya kwa hali anuwai. Hasa, inaweza kufanya majaribio ya dawa mpya kwa matatizo ya nadra ya maumbile kuwa na gharama zaidi.

Chanzo cha picha, THOMAS ANGUS/IMPERIAL COLLEGE
Profesa Paola Giunti, Mkuu wa Kituo cha Ataxia cha UCL alisema: "Tutaweza kujaribu dawa nyingi na wagonjwa wachache kwa gharama ya chini." Kwa upande wa DMD angalau wagonjwa 100 wanahitajika katika kipindi cha takriban miezi 18 ili kupata matokeo muhimu ya kitakwimu yanayohusiana na ufanisi wa dawa mpya.
Utafiti huo ulionesha kuwa kwa kutumia mfumo huo mpya inaweza kufanyika kwa wagonjwa 15 katika kipindi cha miezi sita.
Takribani magonjwa 6,000 adimu ya kijenetiki huathiri jumla ya mtu 1 kati ya 17 nchini Uingereza.
Idadi ya wagonjwa walio na kila ugonjwa inaweza kufikia mia chache au chini.
Hilo ni pingamizi kwa kampuni za dawa kufanya majaribio ya kliniki ya gharama kubwa ili kuunda dawa mpya za kuzitibu.
Mabadiliko makubwa
Profesa Richard Festenstein kutoka Taasisi ya Sayansi ya Tiba ya Baraza la Utafiti wa Matibabu la London, aliiambia BBC News kwamba teknolojia ya suti, ambayo alisaidia kuendeleza, ilikuwa na uwezo wa kubadilisha uchumi wa ugunduzi wa dawa.
''Hii itavutia tasnia ya dawa kuwekeza katika magonjwa adimu," alisema.
"Walengwa wakuu wa utafiti wetu watakuwa wagonjwa, kwa sababu teknolojia itaweza kuja na matibabu mapya kwa haraka zaidi."
Watafiti tayari wanatafuta idhini ya matumizi ya kunasa mwendo kwa majaribio ya dawa ya kutibu FA na DMD, ambayo yakifaulu yanaweza kuanza baada ya miaka miwili. Pia wanakusanya data kwa matumizi yake kwa matatizo ya ubongo ambayo husababisha mwendo usiotarajiwa au zisizoweza kudhibitiwa, kama vile kutetemeka, kukakamaa (Parkinson's), matatizo ya akili (Alzheimer's) na ugonjwa unaoweza kulemaza ubongo na uti wa mgongo (Multiple sclerosis ,MS).













