Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Richarlison ni nani na kwa nini anaweza kuwa nyota ajaye wa Brazil
Bao lake la pili dhidi ya Serbia lilielezewa na vyombo vya habari vya kimataifa kama "kitu bora", "kikubwa", "sarakasi", na "wakati wa muujiza".
Ulimwengu ulikuwa ukifuatilia kwa hamu kila hatua ya nyota tofauti, Neymar (aliyeumia na kutolewa uwanjani kipindi cha pili), lakini Richarlison mwenye umri wa miaka 25 ndiye alipanda na kuwa mchezaji bora wa mechi katika mchezo Alhamisi dhidi ya Serbia.
Richarlison ndiye mfungaji pekee Brazil iliposhinda mchezo huu wa ufunguzi wa makundi kwenye Kombe la Dunia la Qatar, na mchezaji wa Tottenham Hotspur akawa mada inayovuma nchini Brazil wakati wa mechi. Huku uchezaji wa Richarlison ukisifiwa, mashabiki pia walipongeza uchezaji wa mwanasoka huyo nje ya uwanja.
Lakini ni nini kinachomtofautisha mwanasoka huyu wa Brazil na wengine wengi?
Utambuzi wa mapema
Maisha yake ya soka yanatofautishwa kutokana na ustadi wake, lakini anashiriki mengi sawa na wachezaji wengine wa Brazil.
Alizaliwa katika familia maskini katika mji mdogo wa madini, aliacha shule akiwa na umri wa miaka 16 ili kuanza maisha yake ya soka na kuwasaidia wazazi wake na ndugu zake kujikimu kimaisha.
Alicheza kama mshambuliaji wa Atletico Mineiro na Fluminense na kuhamia Uingereza mnamo 2017 - ambapo alitua katika viwanja vya Watford na Everton kabla ya kujiunga na Tottenham mnamo 2022.
Lakini ni utetezi wake wa sayansi, mazingira na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi ambayo yanamtambulisha, na alipokea tuzo ya Bingwa wa Jumuiya ya Chama cha Wachezaji Soka wa Kulipwa nchini Uingereza mnamo 2020, kama sifa ya kazi zake za hisani nchini Brazil.
Covid na chanjo
Kuna msemo maarufu nchini Brazil unasema: "Soka haichanganyiki na siasa". Isipokuwa baadhi - hasa Neymar akimuunga mkono Rais wa Brazil Jair Bolsonaro - wanasoka wengi kihistoria hawapendi kujadili masuala ya kisiasa hadharani.
Richarlison, hata hivyo, anafurahia kusema mawazo yake. Alizungumza haswa juu ya umuhimu wa chanjo katika kilele cha mzozo wa Covid huko Brazil, ambapo karibu watu 700,000 wamekufa kutokana na ugonjwa huo.
Mwaka 2021, wakati Bolsonaro alipokuwa akikosoa hadharani - ijapokuwa hakuwahi kuthibitisha ikiwa alikuwa amepokea au hakuwa amepokea chanjo - Richarlison alitoa wito kwa mamilioni ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii.
"Kutoka moyoni mwangu, ninawaomba ninyi nyote. Tafadhali hakikisheni mmepata chanjo yenu. (...) Chanjo ni yako, ni haki yako. Usipoteze fursa hii."
Baada ya kuwa balozi wa utafiti wa Covid katika Chuo Kikuu cha Sao Paulo, pia alipiga mnada viatu vyake vya mpira wa miguu na kutoa pesa hizo kwa maabara.
"Coronavirus ni adui asiyeonekana na hatari, lakini imetuonyesha nyota halisi ni kina nani. Hawavai viatu vya mpira wa miguu: ni madaktari, wanasayansi na watafiti wanaohatarisha maisha yao kila siku," alisema kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Moto na Msitu wa Amazon
Akiunga mkono lawama za kimataifa za sera za mazingira za Brazil, Richarlison alikosoa moto ulioharibu 30% ya eneo la Pantanal, mojawapo ya mifumo ya ikolojia muhimu zaidi nchini humo.
"Mioto hiyo ilinigusa sana, kwani nilikumbuka siku nilizokaa huko, vijiji nilivyotembelea, ni paradiso na haipaswi kamwe kuteseka na moto, haswa wahalifu," alisema katika mahojiano.
Mnamo Juni 2022, alihimiza mamlaka kuboresha juhudi za kumtafuta mwandishi wa habari wa Uingereza Dom Phillips, ambaye alitoweka katika eneo la Amazon na baadaye kupatikana amekufa, ameuawa baada ya kukemea vitendo haramu katika eneo hilo.
Ubaguzi wa rangi
Mnamo Septemba, Richarlison alirushiwa ndizi uwanjani alipokuwa akishangilia bao katika mechi ya kirafiki dhidi ya Tunisia, jijini Paris.
"Maadamu [mamlaka] wanabaki na "blah blah blah" na haitoi adhabu, itaendelea kutokea hivi, kila siku na kila mahali," aliandika kwenye Twitter.
"Ubaguzi wa rangi ni jambo tunaloishi nalo kila siku," alisema katika mahojiano na kipindi cha siku ya mechi cha Everton mnamo 2020.
"Inaonekana sio tu kwa maneno au kwa vitendo lakini pia kwa kujificha." "Ilikuwa ni ubaguzi wa rangi wakati mimi na marafiki zangu tulipoenda kucheza soka katika jiji langu na mtu fulani akaniita jambazi, wakati sikuwa nimefanya lolote kustahili kuitwa jina hilo. Lakini pia ni ubaguzi wa rangi wakati watu wanabadilisha njia wanapoona mtu mweusi anaingia mahali."
“Haya ni mambo ya hila yanayoonyesha ukubwa wa tatizo,” alisema.
Mwanasoka huyo alisema "alishtuka" na kupatwa na "huzuni" baada ya kuona picha za George Floyd, ambaye alikufa baada ya polisi kupiga magoti kwenye shingo yake huko Minnesota mnamo 2020.
“Ni jambo zuri kwamba ushenzi huu haukuonekana tena na watu wakaamua kuandamana na kuonyesha kutoridhishwa kwao na kitendo hicho,” alisema.
"Tunashuhudia maelfu ya visa kama za George Floyd kila mwaka lakini ni jambo ambalo limekuwa la kawaida. Watu - hasa mamlaka - hawahisi au kuguswa na vitendo hivi."
Mazingira ya umasikini
Richarlison alikulia katika mazingira magumu "umasikini " katika jimbo la Espirito Santo, nchini Brazil.
Akiwa kijana mdogo, alikuwa akiuza peremende na kumsaidia babu yake kuvuna maharagwe ya kahawa.
Alianza maisha yake ya soka kama njia ya kujikimu kimaisha kabla ya kumaliza masoma.
"Hii ndiyo hali halisi ya watoto wengi katika jiji langu na Brazil," alisema baadaye katika mahojiano.
"Wengi huacha shule na kulazimika kufanya kazi ili kusaidia familia zao. Kila ninapoona mtoto anayepaswa kuwa shuleni akilazimika kuacha shule,moyo huvunjika. Bila shaka, nakumbuka utoto wangu ulivyokuwa kama wao."
Sasa, kama mchezaji wa kimataifa aliyefanikiwa na wafuasi milioni 19 kwenye mitandao ya kijamii ya Tiktok, Instagram, Facebook na Twitter, Richarlison anataka kuhamasisha watu mambo mengi zaidi ya ulimwengu wa soka.
"Si kutafuta pesa tu kila wakati, japo ni suala la muhimu pia kuna masuala mengine muhimu tunafaa kuzingatia. Hapo awali nilitaka tu kuwapa wazazi wangu makazi."
"Sasa naona kwamba ninaweza kufanya mengi zaidi ya hayo," anaendelea.
"Naweza kusaidia na ninaweza kuhamasisha watu ndani na nje ya uwanja."