Vita vya Gaza: Je, uwepo wa jeshi la Israel katika eneo la Philadelphi ni mafanikio kwa Netanyahu?

xc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa jeshi la Misri wakishika doria kwenye eneo la Philadelphi mwezi Machi
    • Author, Muhannad Tutunji
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kubaki au kuondoka kwa jeshi la Israel katika eneo la Philadelphi kwenye mpaka wa kusini wa Ukanda wa Gaza, ndilo jambo linaloleta mzozo kati ya Israel kwa upande mmoja na Misri na harakati ya Hamas kwa upande mwingine, jambo hilo linatishia kushindwa kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anashikilia msimamo wake wa kukataa kuondoa jeshi kwenye eneo hilo ambalo ni mpaka kati ya Misri na Gaza.

Afisa wa ngazi ya juu wa serikali amethibitisha kwa vyombo vya habari vya Israel, kuwa Netanyahu hajabadilisha msimamo huu, licha ya ripoti zikieleza amebadilisha msimamo baada ya simu ya hivi karibuni kati yake na Rais wa Marekani Joe Biden.

Kubakisha vikosi huko Philadelphi huenda kukakwamisha mazungumzo juu ya makubaliano ya kuachiwa kwa mateka wa Israel na Wapalestina wanaoshikiliwa na Israel. Kwa upande mwingine, Hamas inashikilia msimamo wake wa kukataa uwepo wowote wa jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza, hasa katika eneo la Philadelphi na eneo la Netzarim, linalotenganisha kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kusini.

Pia unaweza kusoma

‘Netanyahu anatibua mapatano’

vc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moshi angani wakati wa operesheni za kijeshi za Israel huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza

Meja Jenerali mstaafu Itzhak Brik wa jeshi la Israel anasema, “Netanyahu anadanganya umma anapofikiria kudhibiti eneo hilo ndio mafanikio makubwa na ya lazima.”

“Jeshi lipo juu ya ardhi kwenye eneo hilo, lakini mita 50 chini ya ardhi kuna mahandaki, na jeshi haliwezi kuyafikia.”

Anaamini Netanyahu anahujumu mazungumzo hayo anapong'ang'ania wazo la kubaki kijeshi katika eneo hilo, ili vita katika Ukanda wa Gaza visiishe kwa sababu mwisho wa vita unamaanisha mwisho wa mustakabali wake wa kisiasa.

Netanyahu anaona kudhibiti Philadelphi, ukanda wenye urefu wa kilomita 14 kwenye mpaka kati ya Misri na Ukanda wa Gaza, ni miongoni mwa mafanikio ya Israel katika Ukanda wa Gaza, kwa vile Israel inauchukulia ukanda huo kuwa njia ya uhai wa vuguvugu la Hamas.

Lakini jeshi halikubaliani na Netanyahu juu ya wazo la kubaki kijeshi katika eneo hilo, na viongozi wa kijeshi wanathibitisha kuwa suluhisho bora la kuwarudisha mateka ni mazungumzo na Hamas.

Tangazo la Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant la kusambaratishwa kwa Brigedi ya Rafah ya harakati ya Hamas na uharibifu wa mahandaki zaidi ya 150 katika mji huo, akiwa katika eneo la Philadelphi, kwa baadhi ya wachambuzi wanaamini huo ni ujumbe kwa Netanyahu kuwa operesheni kubwa za kijeshi huko Gaza zimemaliza.

Wataalamu wa Kijeshi

dfxc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri wa Ulinzi wa Israel atembelea vitengo vya jeshi katika Ukanda wa Gaza karibu na mji wa Rafah
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jenerali wa akiba wa IDF, Gershon Hacohen anasema hakuna brigedi ya Hamas iliyosambaratishwa moja kwa moja, lakini kusambaratishwa kwa asilimia 30-50, kwa mtazamo wake wa kijeshi, kunamaanisha kuwa kikosi cha mapigano kilichotajwa hapo awali hakifanyi kazi tena.

Hacohen anaamini jeshi kwa sasa limepumzika likisubiri tangazo la kusitisha mapigano.

Mtafiti Elhanan Miller, kutoka Taasisi ya Shalom Hartman, anaamini Netanyahu amefikia malengo yote ya kivita na inaonyesha mwisho wa operesheni kali za kijeshi katika Ukanda wa Gaza unakaribia.

Miller anaamini siku zijazo zitashuhudia jeshi likiondoka kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuelekea kaskazini kwenye mpaka na Lebanon

Mkuu wa zamani wa Kitengo cha Ujasusi cha Jeshi la Israel, Amos Yadlin, aliambia BBC, operesheni hiyo ya kijeshi haitaisha hadi makubaliano ya amani yatiwe saini.

Anasema brigedia ya Rafah imevunjwa kama kikosi cha kijeshi, lakini hakuna shaka kuna baadhi ya magaidi bado wapo katika eneo hilo na baadhi ya mahandaki bado hayajaharibiwa kabisa.

Lakini anaamini hitajio la kiusalama sasa ni uhamisho wa vikosi kutoka Ukanda wa Gaza, ili kujiandaa kwa hali yoyote kwenye mpaka wa kaskazini na Lebanon.

Kuhusu eneo la Philadelphi, Yadlin anaona eneo hilo ni muhimu na inawezekana kukubaliana na Marekani na Misri, kufunga njia za kuingia Misri na anaamini jeshi la Israel lina masuluhisho mengi katika suala hili katika siku zijazo.

Israel kwenyewe

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapalestina wa Gaza wanatembea kwenye eneo la Netzarim katika Ukanda wa Gaza

Miller aliiambia BBC, anatarajia maafisa wengi wa jeshi watajiuzulu na hilo litatoa uwezekano wa umma wa Israel kuingia mitaani kwa wingi zaidi. Na mzozo kati ya Netanyahu na Gallant utasababisha kufukuzwa kazi Gallant.

Lakini inaonyesha Netanyahu hataki kumfukuza kazi sasa kwa kuhofia kuongezeka kwa maandamano dhidi yake katika mitaa ya Israel, na wasiwasi wa mashambulizi ya kijeshi ya Hezbollah au Iran.

Katikati ya haya, kila mtu anasubiri mabadiliko katika misimamo ya Netanyahu kuhusu masuala yaliyosalia. Vyombo vya habari vya Israel, ikiwa ni pamoja na Channel 12, vinasema sehemu ya mazungumzo ya Cairo hayalengi tu makubaliano ya Israel na Hamas juu ya eneo la Philadelphi, bali pia kufikia maelewano na Misri.

Kuhusu uwepo wa Israel kijeshi katika eneo hilo, na kujadili uwezekano wa kufanya marekebisho kwenye Makubaliano ya Camp David, ambayo yanazuia kabisa uwepo wa jeshi la Israel katika eneo hilo.

Lakini hakuna vyanzo rasmi vya Israel ambavyo vimethibitisha uwepo wa majadiliano ya marekebisho hayo, kama habari inavyosambaa.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi