Wanamichezo wa kiume na wa kike waliotia fora mwaka 2023

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili
Licha ya ulimwengu kukumbwa na misukosuko chungu nzima mwaka huu ikiwemo ongezeko la bei ya bidhaa, mabadiliko ya tabianchi , majanga mbalimbali pamoja na vita kati ya Israel na Gaza, vilevile kuna mazuri yalioshuhudiwa.
Baadhi ya wanamichezo walipuuzilia mbali hali hiyo na kuonesha umahiri wao.
Baadhi yao ni Victor Omsihen na Faith Kipyegon wa Kenya walioshinda mataji ya mchezaji bora wa Caf na mwanariadha bora duniani miongoni mwa wanawake.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji walioshamiri mwaka huu na wanatarajiwa kufanya vyema zaidi mwaka ujao.
Lionel Messi
Kuanzia uchawi wake uwanjani hadi pesa zake na uwepo wake mzuri nje ya uwanja, Messi anatawala kama mtu mwenye ushawishi katika mchezo maarufu zaidi ulimwenguni.
Hakuna mchezaji anayemiliki zaidi ya mataji 43 ambayo amejikusanyia katika maisha yake yote ya soka, ambayo ni pamoja na mataji 12 ya ligi kati ya Barcelona na Paris St.-Germain, tuzo saba za Ballon d'Or na Kombe la Dunia la 2022 ambazo huenda zikamfanya kuwa mchezaji bora zaidi wa muda wote.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 ameorodheshwa kwenye orodha ya tatu bora ya wanamichezo wanaolipwa pesa nyingi zaidi na jarida la Forbes kwa miaka minane mfululizo, na jezi yake inaweza kupatikana kila kona ya dunia-baada ya kuondoka PSG na kusajiliwa na Inter ya MLS.
Nestor Irankunda

Chanzo cha picha, Reuters
"Bayern" ilitangaza kwenye tovuti yao rasmi kumsajili kiungo wa kati wa Australia mwenye umri wa miaka 17.
Klabu hiyo ya mjini Munich ilitangaza kumsajili mchezaji huyo mnamo tarehe 14 mwezi Novemba kutoka klabu ya "Adelaide United". Hatahivyo mchezaji anatarajiwa kujiunga na klabu ya "Bayern" mnamo Julai 1, 2024, baada ya kufikisha miaka 18.
Imebainika kuwa Irankunda ambaye tayari ameshapokea mwito kwenye timu ya taifa ya Australia alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania.
Wazazi wake wanatoka Burundi lakini walilazimika kuondoka nchini kutokana na ugonjwa wa binti yao na kuongezeka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyomalizika mnamo 2005.
Aitana Bonmati

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mshindi wa tuzo ya Golden Ball wa Kombe la Dunia la FIFA miongoni mwa Wanawake, Aitana Bonmatí pia alishinda tuzo ya kifahari ya Ballon D'Or mjini Paris akimrithi mchezaji mwenzake wa FC Barcelona, Alexia Putellas. Putellas alishinda miaka miwili iliyopita.
Katika upigaji kura, Aitana alimaliza mbele ya Sam Kerr wa Chelsea na Australia na wachezaji wenzake wawili wa FC Barcelona, Salma Paralluelo na Fridolina Rolfö ambao.
Walimaliza katika nafasi za tatu na nne mtawalia. Katika hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo, Aitana alisema “kama watu wa kuigwa tuna wajibu ndani na nje ya uwanja, tunapaswa kuwa zaidi ya wanariadha.
Endelea kuongoza kwa mfano na endelea kupigana pamoja kwa ajili ya ulimwengu bora, wenye amani na usawa.
Tuzo hiyo ya Ballon D'Or 2023 inamaanisha kuwa wachezaji wanaowakilisha klabu ya FC Barcelona na Uhispania sasa wameshinda tuzo hizo kwa miaka mitatu mfululizo.
Mshindi wa Kombe la Dunia la FIFA miongoni mwa Wanawake Uhispania imekuwa taifa la kwanza kutoa washindi wawili tofauti wa Ballon D'Or ya wanawake katika historia yake ya miaka sita.
Kylian Mbappé

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakielekea katika siku zao za mwisho za uchezaji soka, kandanda haitalazimika kusubiri kwa muda mrefu kumpata mrithi wa magwiji hao wawili.
Mbappé ndiye sura ya mustakabali wa mchezo huo, kama mfungaji bora wa muda wote wa PSG na mmiliki wa mkataba mnono zaidi wa soka barani Ulaya, akilipwa dola milioni 100 kwa mwaka. Akiwa na umri wa miaka 24, tayari ana wafuasi wengi zaidi nchini Ufaransa katika mitandao ya kijamii.
Mchezaji huyo kwasasa anakamilisha kandarasi yake iliosalia katika klabu ya PSG na anapigiwa upatu kujiunga na timu ya Real Madrid ambapo anapania kushinda taji la klabu bingwa Ulaya mbali na mwanasoka bora wa mwaka 2024.
Faith Kipyegon

Chanzo cha picha, Getty Images
Kipyegon alizima ushindani mkali na kushinda tuzo hiyo iliyotamaniwa sana, huku Wakenya wenzake Faith Cherotich na Emmanuel Wanyonyi wote wakishinda tuzo za nyota chipukizi wa mwaka .
Akiwa mshikilizi wa rekodi ya dunia mara mbili Faith Kipyegon amekuwa Mkenya wa kwanza kushinda taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka miongoni mwa Wanawake Duniani katika riadha baada ya kufurahia msimu mzuri wa 2023 .
Kipyegon aliweka rekodi za dunia katika masafa matatu ya ajabu katika msimu ambapo pia alipata medali ya dhahabu maradufu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia huko Budapest.
Kwanza, Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 29 aliboresha rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 hadi 3:49.11 mjini Florence.
Wiki moja tu baadaye, na licha ya kuwa alikimbia mbio za mita 5000 mara mbili tu hapo awali, aliboresha rekodi ya dunia ya mbio hizo akitumia dakika 14:05.20 mjini Paris na kunyoa sekunde 1.42 kutoka kwa rekodi ya awali. Rekodi yake ilivunjwa baadaye na Gudaf Tsegay wa Ethiopia.
Victor Osimhen

Chanzo cha picha, Getty Images
Victor Osimhen wa Nigeria ametawazwa Mwanasoka Bora wa Afrika 2023 katika hafla ya utoaji wa tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mjini Marrakesh.
Mchezaji huyo wa Napoli aliwashinda Mmisri, Mohamed Salah na Achraf Hakimi wa Morocco katika tuzo hiyo ya kifahari - hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mnigeria kutwaa taji hilo tangu Nwankwo Kanu mwaka 1999.
Nigeria ilifurahia mafanikio maradufu huku Asisat Oshoala akihifadhi tuzo ya upande wa wanawake - ikiwa ni mara ya sita kwa nyota huyo wa Barcelona kushinda tuzo hiyo.
Washindi hupigiwa kura na jopo linalojumuisha kamati ya ufundi ya Caf pamoja na wanahabari wa Afrika, makocha wakuu na manahodha.
Vilabu vinavyoshiriki katika hatua ya makundi ya mashindano ya bara Afrika pia vina usemi kuhusu mshindi wa tuzo hiyo.
Shelly -Ann Fraser Pryce
Bingwa wa dunia wa mbio za mita 100 miongoni mwa wanawake Shelly-Ann Fraser-Pryce alitawazwa kuwa Mwanaspoti Bora wa Dunia wa Laureus mwaka huu katika Tuzo za kifahari za 2023 mjini Paris.
Washindi wote wanane wa tuzo hiyo walikuwa katika mji mkuu wa Ufaransa kusherehekea mwaka wa ajabu wa riadha.
Fraser-Pryce alishinda rekodi ya tano ya dhahabu ya mita 100 katika Mashindano ya Riadha ya Dunia ya Oregon22, miaka 13 baada kushiriki mashindano yake ya kwanza.
Ana mataji mengi ya mbio za dunia kuliko mwanariadha mwingine yeyote, na mnamo 2022 alikimbia chini ya 10.7 kwa mita 100 mara saba, ikiwa ni mara tatu zaidi ya mwanariadha wa kike katika mwaka mmoja
Letsile Tebogo
Akiwa na umri wa miaka 20, Letsile Tebogo wa Botswana alilipatia bara la Afrika medali yake ya kwanza kabisa ya dunia katika mbio za mita 100, miongoni mwa wanaume mjini Budapest.
Muda bora zaidi wa Tebogo wa sekunde 9 nukta 88 katika mashindano ya Hungary ulishindwa na ule wa Noah Lyles.
Mafanikio hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba yalipotangazwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, yalipigiwa makofi na Lyles na mwanariadha wa tatu kwenye jukwaa, Zharnel Hughes wa Uingereza.
Tebogo amekuwa tegemeo la bara la Afrika siku zijazo kutokana na umri wake mdogo na juhudi zake za kutaka kushinda.
Amekuwa bingwa wa dunia wa vijana mara mbili katika mbio za mita 100 na mshindi wa pili wa mbio za mita 200 mwaka wa 2021 na 2022
Asisat Oshoala

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota wa Nigeria Asisat Oshoala amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa CAFSwomen kwa rekodi ya mara ya sita baada ya kuiwezesha Barcelona kutwaa ubingwa wa ligi ya Primera.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 29 aliwashinda Thembi Kgatlana wa Afrika Kusini na Zambia Barbara Banda kwenye tamasha huko Marrakech.
Oshoala alikuwa mfungaji bora wa Barcelona msimu uliopita, akifunga mabao 27 katika mashindano yote huku wababe hao wa Uhispania wakishinda mataji mawili ya Uhispania.
Magoli yake yaliisaidia Barcelona kuhifadhi taji lao la daraja la kwanza na kuishinda Lyon hatua iliowafanya watawazwe kuwa mabingwa wa ligi kuu ya Ulaya huko Turin.
Na Oshoala mchezaji wa kwanza wa Kiafrika kushiriki katika makombe matatu ya dunia - pia aliandikisha historia yake katika soka la Uhispania.
Alikua mchezaji wa kwanza wa kike kupokea tuzo ya mfungaji bora zaidi katika ligi kuu ya Uhispania baada ya kufikisha mabao 20 kwenye ligi.












