Waridi wa BBC: 'Saratani si hukumu ya kifo'

Chanzo cha picha, Annah Kilawe, IG
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC News Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ugonjwa wa saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayoleta madhara makubwa kiafya na hata kusababisha vifo kwa mamilioni ya watu ulimwenguni. Kwa wengi, kugundulika na saratani ni kama hukumu ya kifo, lakini kwa Annah Kilawe, ilikuwa mwanzo wa safari yenye changamoto, matumaini, na hatimaye ushindi mkubwa dhidi ya ugonjwa huu.
Annah alikuwa msichana wa miaka 17 mwenye ndoto na maisha yaliyojaa matumaini. Hakuwa na wazo lolote kwamba maisha yake yangepitia mabadiliko makubwa kiasi cha kumlazimu kufanya maamuzi magumu ili aendelee kuishi.
Mnamo, mwaka 2020, Annah alianza kupata maumivu ya mgongo na kiuno. Alijihisi mchovu sana, hali iliyomfanya aonekane mvivu kwa macho ya familia yake. Awali, alihisi huenda ni uchovu wa kawaida, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, aliamua kutafuta msaada wa kitabibu.

Alikwenda hospitalini kwa mara ya kwanza, ambapo alielekezwa kufanya mazoezi ili kupunguza maumivu. Lakini kila alipomaliza mazoezi, hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Baadaye, aliporejea shuleni Biharamulo, baba yake aliwataarifu walimu wake kuhusu hali yake, wakiamini angepata uangalizi wa karibu.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye, hali ilizidi kuwa mbaya. Alipatwa na homa kali, jambo lililomfanya kurudi nyumbani kwa uchunguzi zaidi. Hatimaye, alifikishwa hospitali ya taifa, jijini Dar es salaam, Muhimbili kwa uchunguzi wa kina, alielezwa kuwa matatizo yake yalihusiana na kiuno na kwamba baada ya wiki moja angeruhusiwa kurudi nyumbani.
Saratani na Uamuzi Mgumu

Chanzo cha picha, Annah IG
Siku ya kuchukua majibu ya vipimo ilipowadia, Annah alifuatana na baba yake hospitalini. Alishangaa jinsi baba yake alivyobadilika ghafla na alikuwa mpole kupita kawaida, akimfurahisha na kumnunulia chakula cha gharama kubwa. Lakini Annah hakuwa na hamu ya kula.
Walipofika nyumbani, baba yake aliagiza apewe kila kitu anachotaka na asifanye kazi yoyote. Annah alianza kushuku kuna jambo kubwa linajificha. Siku iliyofuata, alikwenda hospitali na mama yake. Aliona wazazi wake wakiwa karibu sana, hali iliyokuwa tofauti na kawaida yao maana walikuwa hawaishi wote.
Alipowauliza kulikoni, walimwambia kila kitu kitakuwa sawa. Ukweli ni kwamba, madaktari waliwaambia wazazi wake kuwa Annah alikuwa na saratani ya nadra iitwayo Rhabdomyosarcoma, ambayo hushambulia tishu laini za mwili. Zaidi ya hapo, waliambiwa kuwa hata akifanyiwa upasuaji wa kukata mguu, nafasi yake ya kuishi alipewa miezi minne tu ya kuishi, akikatwa au asipokatwa mguu.
Ilipofika usiku wa siku hiyo ya majibu akiwa nyumbani, Annah alisikia mama yake akilia wakati akiongea na simu, akitaja suala la miezi minne. Alishtuka na kumuuliza mama yake, "Kwa hiyo mimi nitakufa?" Mama yake, akiwa na machozi, alimwambia, "Utakuwa sawa."
Kwa kuwa hakuwahi kushuhudia mgonjwa wa saratani, Annah hakuelewa uzito wa hali yake. Alidhani ni ugonjwa tu kama magonjwa mengine na kwamba angesikia nafuu baada ya muda mfupi.
Niliambiwa kuna mtu nilimkataa akakasirika na kunipa Saratani
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Familia yake ilikataa katakata suala la kukatwa mguu, badala yake, walitafuta uponyaji kupitia njia mbadala za maombi, tiba za asili, na hata waganga wa kienyeji.
Baadhi ya watu waliwashauri kwenda kwa daktari mmoja wa tiba asili aliyepo Moshi, wakidai ana uwezo wa kutibu saratani. Annah alipofika huko, mganga alimwambia kuwa kuna mtu aliyemloga, hivyo akawa na kazi ya kutafuta ni nani aliyemfanyia hivyo.
Katika harakati za kutafuta "aliyehusika," Annah alifikiria kuhusu watu aliowahi kuwajibu vibaya, hasa waendesha bodaboda mtaani kwao. Alimkumbuka kijana mmoja aliyekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu akimtaka kimapenzi wakati yuko shule. Alipata namba yake, akampigia simu na kumuomba msamaha, lakini kijana huyo alimwambia hana kinyongo naye na wala hajui chochote.
Siku iliyofuata,daktari huyo wa tiba asili alimwagia maji ya barafu mara alijisikia nafuu kwa siku moja na kila mtu akamwamini.Lakini hali yake Annah ikazidi kuwa mbaya zaidi baadaye.
Mara wakapata taarifa ya daktari mwingine wa tiba asili yuko Arusha, waliamua kwenda huko. Alimsaidia kupata hamu ya kula, lakini saratani iliendelea kumsumbua. Familia yake ilikuwa ikimlipa mganga huyo Sh. 300,000 kila wiki.
Na mara akataka kumpima saratani ya kizazi yeye mwenyewe , kwa kuwa "mtu hawezi kuwa umepata saratani kama hakushiriki tendo la ndoa hivyo nilipokataa tiba yake, wazazi wangu waliamua kunirudisha hospitali.
Uamuzi wa Kukatwa Mguu na Safari Mpya
Hali yake Annah ilizidi kuwa mbaya, alianza kukamaa na uvimbe ukawa mkubwa zaidi. Madaktari waliwahita tena wazazi wke, kuwaambia kuwa walihitaji kukata mguu wake haraka kabla saratani haijasambaa zaidi mwilini.
Ingawa awali Annah alikataa lakini sasa alikuwa tayari. Baada ya upasuaji, alihisi afadhali kuliko alivyotarajia. Maumivu yalipungua, na afya yake ilianza kuimarika taratibu.
Lakini changamoto hazikuisha, Alianza tiba ya mionzi kwa njia ya drip, hali iliyosababisha nywele zake kudondoka, ngozi yake kuwa nyeusi na kucha zake kuharibika.
Pamoja na hayo, hakutaka kurudi nyuma. Alijifunza kuishi bila mguu mmoja, akaanza kujitegemea na kufanya mazoezi. Alipenda kusafiri, kucheza, na kushiriki katika shughuli mbalimbali kama mtu yeyote wa kawaida

Chanzo cha picha, Annah IG

Chanzo cha picha, Annah IG
Annah: Rafiki yako wa mitandaoni
Kabla hajakatwa mguu, Annah hakupenda kupigwa picha. Lakini baada ya safari yake ya saratani, aliamua kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wengine, kupinga unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu na kuelimisha jamii kuhusu saratani.
Aliamua kujiita "rafiki wa mtandaoni" kwa wale waliokuwa wakipitia changamoto kama zake. "Ukiwa na mawazo au unataka kuzungumza na mtu, niambie mimi," alisema.
Licha ya ndoto yake ya awali ya kuwa daktari wa kawaida kuzimwa kutokana na ulemavu wake, hakukata tamaa. Aliamua kusomea udaktari wa macho baada ya kukataliwa kusomea udaktari wa kawaida.
Leo, Annah ni mfano wa ushindi dhidi ya saratani na ushahidi kwamba maisha yanaweza kuendelea hata baada ya changamoto kubwa.

Chanzo cha picha, Annah IG
Katika harakati za kujikubali na kuwahamasisha wengine, Annah aliamua kushiriki safari yake kwenye TikTok. Kwa mara ya kwanza, alitupia video yake akicheza kwa mguu mmoja, akidhani itakuwa tu burudani ya kawaida. Lakini hakutarajia majibu makubwa kutoka kwa watu – video yake ilivuma haraka, ikipata maelfu ya maoni na wafuasi.
"Niligundua kuwa kupitia TikTok, ninaweza kusaidia watu kuelewa kuwa ulemavu si mwisho wa maisha. Ninaweza kushiriki safari yangu, kuwasaidia watu wanaopitia changamoto kama zangu, na pia kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu," alisema Annah.
Leo hii, Annah ana zaidi ya nusu milioni ya wafuasi kwenye mitandao yake ya kijamii, ambako anatumia jukwaa lake kutoa ushauri kwa wagonjwa wa saratani, kushiriki uhalisia wa maisha yake, na kuwahamasisha vijana wasikate tamaa.
changamoto wanazokumbana nazo watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, na ajira.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya watu milioni 3.3 nchini Tanzania wana ulemavu, huku wanawake wengi zaidi. Hata hivyo, bado kuna changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi zinazowakabili. Kupitia kazi yake kama mshawishi wa mitandao ya kijamii, Annah anatoa mwanga juu ya changamoto hizi na kusisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo.












