Watu wanaojiita Wanamajumui wa Kiafrika wanavyokuza taarifa za uongo kuhusu mapinduzi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Chiagozie Nwonwu, Mungai Ngige & Olaronke Alo
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mwezi Mei, Mafalda Marchioro aliamka na kupokea jumbe kutoka kwa marafiki wanaoishi ng'ambo wakimuuliza kama yuko salama Abidjan, jiji kubwa zaidi nchini Ivory Coast.
Mitandao ya kijamii ilijaa machapisho yanayodai mapinduzi yanafanyika. Video za askari barabarani zilifurika mitandaoni, huku ripoti zilizotolewa kwa akili mnemba (AI) zikikusanya mamilioni ya watu kuzitazama kwenye YouTube.
"Nilikuwa na wasiwasi sana, nilidhani kuna kitu kimetokea," Marchioro ambaye ni mshauri wa masuala ya uongozi aliiambia BBC.
Lakini madai hayo ya 19 Mei yalikuwa ya uwongo.
Ni mfano wa hivi karibuni zaidi wa uvumi usio wa kweli unaoenezwa kuhusu mapinduzi Afrika Magharibi, na kuongeza hali ya wasiwasi katika eneo ambalo limeshuhudia mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.
Ivory Coast, mojawapo ya nchi chache zinazozungumza Kifaransa ambayo bado ina ukaribu na nchi za Magharibi, inatazamiwa kufanya uchaguzi wa rais baadaye mwaka huu.
Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattarra, yuko tayari kugombea muhula wa nne, na anaonekana kuunga mkono ukaribu na Magharibi - na wakosoaji wake wanamtuhumu kwa kujihusisha na nchi zinazolinyonya bara hilo.
Ni akina nani?

Chanzo cha picha, Youtube
Waziri wa Mawasiliano wa Ivory Coast, Amadou Coulibaly aliiambia BBC, wamefuatilia asili ya habari hizo ghushi na "zinatoka nchi jirani," lakini hakusema zaidi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uvumi huo unaonekana kuibuka kutokana na mtafaruku na Burkina Faso na umekuzwa na watu wanaojiita wafuasi wa Umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism).
Watu hao wanakataa uhusiano na nchi za Magharibi, mara nyingi wanaonyesha kuunga mkono Urusi.
Watu hao pia humsifu kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Capt Ibrahim Traoré, ambaye alichukua mamlaka katika mapinduzi ya 2022.
Traoré anajionyesha kama mwana-majumui wa Kiafrika na ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana katika bara zima, ambao wanamwona kama kiongozi anayepinga Magharibi.
Alex Vines, mkurugenzi wa kitengo cha Afrika katika taasisi ya fikra tunduizi ya Chatham House huko Uingereza, anasema watu hao wanajaribu kupandikiza mashaka kwa serikali zilizopo kwa kueneza au kuongeza uvumi wa mapinduzi, ili kuondoa imani ya umma kwa serikali hizo.
"Wanawalenga wasomaji ambao wanataka kuona viongozi wa Kiafrika wenye uthubutu, ambao wanaleta maendeleo na kuleta amani na ustawi," aliiambia BBC.
Burkinabe na Ivory Coast
Hakuna ushahidi kwamba mamlaka za Burkinabe zilihusika katika uvumi wa mapinduzi ya Ivory Coast lakini watu wanaoishi huko walizidisha madai hayo.
Uhusiano kati ya Burkina Faso na Ivory Coast ulidorora zaidi ya mwaka mmoja uliopita, wakati Traoré alipomshutumu jirani yake kwa kuhifadhi vikundi vya wapiganaji na kuwahifadhi wapinzani wanaoitusi serikali yake waziwazi.
Kisha Aprili iliyopita, Waziri wake wa usalama aliwalaumu wapanga njama walioko nchini Ivory Coast kwa kupanga kumpindua Traoré - tuhuma ambayo ilikuzwa sana mtandaoni.
Kitengo cha BBC cha Kufuatilia Habari za Uongo Ulimwenguni, kilifuatilia ripoti za uwongo juu ya mapinduzi huko Ivory Coast kwenye TikTok, Facebook, X na YouTube - na chapisho la mapema zaidi tulilolipata lilikuwa la tarehe 19 Mei la Harouna Sawadogo, mwanaharakati anayeiunga mkono serikali nchini Burkina Faso ambaye huchapisha maudhui kwa wafuasi wake 200,000 wa TikTok hasa kuhusu Capt Traoré.
Alichapisha video aliyojirikodi kwa lugha ya Kifaransa na Kimooré, lugha ya wenyeji, akisema askari wa Ivory Coast wanapaswa kuinuka kufanya mapinduzi na kuhimiza watu kueneza video yake.
Saa moja baadaye alichapisha video iliyokuwa na picha ya Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara aliyeiweka juu ya video yenye milio ya risasi na kusema mapinduzi yalikuwa yakiendelea - ingawa kipande hicho cha video kilikuwa cha mvutano wa hivi karibuni wa India-Pakistani kuhusu Kashmir.
Siku iliyofuata, watumiaji wa mitandao ya kijamii nje ya Afrika Magharibi ya Francophone walivamia habari hiyo potofu na kuisambaza kwa hadhira inayozungumza Kiingereza nchini Nigeria, Kenya na Afrika Kusini, na kuwahimiza watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii kuieneza.
Wakati BBC ilipomtumia ujumbe Bw Sawadogo wiki chache baadaye, kupitia ukurasa wa Facebook, kuuliza alikotoa taarifa zake, hakujibu zaidi ya kusema "anaomba kwa Mungu Alassane [Ouattara] aangushwe kwa mapinduzi."
Mapinduzi ya Uongo

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwingine ambaye alichukua uvumi huo, na kuandika kwa Kiingereza, ni mturuki aliyezaliwa Afrika Kusini, Mehmet Vefa Dag, ambaye anaendesha Truth and Solidarity Movement - shirika dogo la kisiasa nchini Afrika Kusini.
Alichapisha mara kadhaa kwenye majukwaa tofauti akisherehekea kile alichokiita "mapinduzi ya ndani."
Bw Dag, ambaye alikosolewa siku za nyuma kwa maoni ya kuudhi na ya uongo dhidi ya Wayahudi na watu wa LGBTQ+, tayari aliwahi kutoa mwito wa mapinduzi nchini Ivory Coast tarehe 11 Mei kupitia X.
Alipotafutwa na BBC tarehe 3 Juni, ilipobainika kuwa hakukuwa na mapinduzi, alisisitiza kuwa yalifanyika.
"Tunajivunia sana aliyefanya mapinduzi haya ya kumuondoa Ouattara. Aliuza utu wake kwa mabeberu na alitaka kuiangamiza Burkina Faso, Mali na Niger," alisema.
"Kama wana-majumui hatutawapa nafasi tena. Tutapigania nchi yetu. Hili ni bara letu."
Kulingana na Effiong Udo, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Uyo cha Nigeria na rais wa Taasisi ya Pan-African Dialogue, baadhi ya "watu wenye ushawishi" wanazipenda serikali za kijeshi chini ya kivuli cha uwanamajumui wa Kiafrika – (harakati ya kukuza umoja na ukombozi katika bara) - ili kupata umaarufu na kupata pesa kutokana na maudhui yao.
Lakini aliambia BBC, aina hii ya maudhui yanavutia vijana waliokatishwa tamaa na siasa, na kuongeza: "Naelewa kwa nini wanatia bidii."
Msomi wa Kenya, Karuti Kanyinga anakubali kwamba maudhui ya mitandao ya kijamii yanaleta hamu ya kuwa na viongozi wanaowajibika ambao wanaweza kuibadilisha Afrika, watumie vizuri rasilimali na kuwainua watu kutoka katika umaskini.
"Lakini watu wanaojaribu kutoa taarifa potofu na zisizo sahihi kuhusu Traoré nchini Burkina Faso, au kuhusu mapinduzi ya Ivory Coast sio waumini wa umajumui wa Kiafrika," profesa wa utafiti katika masomo ya maendeleo katika Taasisi ya Mafunzo ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Nairobi aliiambia BBC.
Maudhui yanayovuma
Hakuna shaka Traoré ana watu wengi wanaompenda na kwa waundaji wa maudhui yeye ndiye hadithi ya wakati huu - chochote kinachohusishwa naye na mtazamo wake wa kisiasa hufanya vizuri sana mtandaoni.
MwanaYouTube wa Kenya Godfrey Otieno, ambaye hutoa maudhui juu ya habari zinazovuma, alisema alijikwaa na fomula hii ya kusaka wafuatiliaji miezi kadhaa iliyopita alipochapisha video iliyoripoti madai ya uwongo kwamba Capt Traoré alipigwa risasi na rafiki yake wa karibu.
"Hilo lilivuma sana," aliiambia BBC - na tangu wakati huo maudhui yake karibu yote yamekuwa yanamhusu kiongozi wa Burkinabé.
Alikuwa mmoja wa wale waliochapisha taarifa ambazo hazijathibitishwa kuhusu Ivory Coast mwezi Mei na video yake ilipata maoni zaidi ya 200,000. Baadaye aliomba msamaha na kusema alikosea.
Anakiri kwamba yeye hupata pesa kutokana na baadhi ya maudhui yake, na anasema motisha yake haisukumwi na kupata pesa tu.
Anakubali kwamba, "kuna watu ambao wanatumia taarifa potofu na uongo kukuza wingi wa wafuatiliaji wao," anasema.















